Tiba sahihi kwa anayewashwa eneo la ndani ya koo

Dk Christopher Peterson

Mwasho ndani ya koo ni moja ya matatizo madogo madogo ya kiafya ambayo huashiria aleji za aina tofauti au maambukizi ya virus (sio lazima viwe vya ukimwi) au maambukizi ya kibakteria.

Muwasho ndani ya koo unatokana na sababu mbali mbali japo kuwa kwa kiasi kikubwa huchangiwa na aleji ya baadhi ya vyakula.

Kupitia aleji hiyo, hutokea wakati kinga ya mwili inapambana na vimelea vya maradhi yaliyomo kwenye vyakula ambavyo huhatarisha afya za miili.

Kwa kawaida kinga za mwili hupambana na vimelea hivyo muda mfupi baada ya mtu kula chakula chenye vimelea vya maradhi.

Lakini kwa watu wengine aleji inaweza kutokea hata siku kadhaa baada ya kula chakula. Inaweza kuwa ya kawaida ikiambatana na dalili chache kama za mwasho ndani ya koo au mdomoni. Hata hivyo mara chache inaweza kuashiria tatizo kubwa kiafya.

Aleji inayotokana na matumizi ya aina mbalimbali za dawa pia inasababisha mwasho ndani ya koo. wengi wanashambuliwa na aleji zinazotokana na matumizi ya dawa hasa za kiantibayotiki.

Aleji hii inapotoke muathirika huanza kupata ishara mbalimbali mwilini ikiwamo mwasho ndani ya koo. Mtu anapokua na mafua makali hasa wakati wa baridi, maumivu na mwasho ndani ya koo huongezeka maradufu ukiambatana na hali ya homa na maumivu ya kifua.

Muasho huu unaweza kudumu kwa muda kadhaa usipopatiwa tiba unaweza kuwa hatari kwa afya.

Kuna maambukizi ya maradhi ambayo mara nyingi hutokea kooni ambayo kwa kitaalamu streptococall au strep throat. Maambukizi haya yanapotokea huambatana na vidonda kwenye koo ambavyo wengi huviita tonsillitis vinavyoambatana na mwasho ndani ya koo hatimae kuongezeka na kuleta maumivu makali kwenye koo.

Baadhi ya virusi vinavyosababisha mafua pia vinaweza kuleta muwasho ndani ya koo.

Ni dhahiri kuwa, kila mmoja anafahamu umuhimu wa maji kwa afya. Ukosefu wa kiwango cha kutosha cha maji husababisha pia tatizo la mwasho ndani ya koo.

Upungufu wa maji mwilini hutokea pale mwili unapopoteza kiwango kikubwa cha maji kuliko kile kinachoingia na mara nyingi hali hii hutokea wakati wa joto kali au baada ya kufanya mazoezi ya mwili au mtu anapougua homa.

Upungufu wa maji mwilini unaweza kusababisha kukauka kwa mdomo, japo hali hii huwa ni ya muda kwa sababu mdomo na koo havipati mate ya kutosha kutokana na upungufu wa maji mwilini na hivyo kusababisha mtu kupata mwasho ndani ya koo.

Utendajikazi wa dawa mwilini pia unaweza kusababisha mwasho ndani ya koo. Baadhi ya dawa nazo zinaweza kusababisha kikohozi kikavu na mwasho ndani ya koo ambayo hayatokani na aleji zinazotokana na dawa.

Hata watu wanaotumia baadhi ya dawa za shinikizo kubwa la damu (ACE inhibitors), wanapaswa kutambua kuwa dawa hizo zinaweza kuwasababishia kikohozi kikavu na mwasho ndani ya koo wakati wa utendaji kazi wake mwilini.

Kwa kawaida dalili hizi hutokea mara tu baada ya kutumia dawa hizo na mara zote haziambatani na dalili zingine tofauti na mwasho ndani ya koo na kikohozi kikavu.

Kukabiliana na tatizo hili katika hatua za awali, mgonjwa anaweza kutumia njia za asili akiwa nyumbani ili kupunguza tatizo kama kulamba kijiko kimoja cha asali, kunywa chai iliyochanganywa na limau na asali pamoja na kunywa maji ya moto yaliyowekwa chumvi.

Aidha, ikitokea tatizo hilo linazidi kwa muda wa siku 10, ni vema kumuona daktari kwa msaada zaidi wa kitabibu.