Tim: wabunifu wanaolia kuwezeshwa kutatua shida ya maji vijijini

Baadhi ya vijana wanaounda kikundi cha Tim, wakiwa katika harakati za kutengeneza kinu cha upepo kinachotumika kuendesha pampu ya kusukuma maji waliyoibuni. Picha na Asna Kaniki

Muktasari:

Waliojitahidi kujitofautisha na wenzao, angalau wameamua kuwa madereva wa bodaboda, kazi ambayo kwa kiasi fulani imesaidia kuwatoa katika kundi la vijana tegemezi mtaani.

Ni kawaida kuona vijana mtaani wakipiga soga pasipo kujishughulisha kutafuta maisha.

Waliojitahidi kujitofautisha na wenzao, angalau wameamua kuwa madereva wa bodaboda, kazi ambayo kwa kiasi fulani imesaidia kuwatoa katika kundi la vijana tegemezi mtaani.

Lakini wengi wanaamini kuwa bila elimu huwezi kufanya kazi yoyote, na hawa ndio wanaozagaa mtaani na mwishowe kuishia katika makundi maovu.

Hata hivyo, wako vijana wachache wanaotambua thamani ya ujana; kwao ujana ndio kipindi cha kujituma na kubuni mambo mbalimbali kwa ajili ya kupambana na maisha kama ilivyo kwa kundi la vijana wanaojiitra kwa kwa jina la TIM.

Vijana hawa waliopo jijini Dar es Salaam, wamebuni mashine ya kuvuta maji kutoka kwenye kisima kwa kutumia upepo.

Kundi hili la vijana 10 lilianza rasmi mwaka 2013 kwa kutengeneza vitu mbalimbali kama vitanda vya chuma na mageti na baadae wakaanzisha mradi wa kutengeneza mashine za kuvuta maji.

Tamimu Kifungu ni mmoja wa wabunifu katika kundi hilo, anayesema waliangalia vitu ambavyo vitaigusa jamii.

“Maji ni moja ya changamoto ambayo Watanzania wengi wanahangaika usiku na mchana hasa maeneo ya vijijini, ‘’anaeleza.

Anasema wamegundua kuwa kuna baadhi ya maeneo hasa vijijini watu wana uwezo wa kuchimba visima, lakini kinachokwamisha ni upatikanaji wa umeme wa kupandisha maji.

Hali hii anasema wakaitumia kama fursa kwa kubuni mashine hiyo inayotumia upepo.

“Kuchimba kisima kunahitaji gharama, kama kundi tukajiuliza je, Mtanzania wa kawaida tena anayeishi kijijini ana uwezo wa kuchimba kisima kwa kutumia umeme? Tukaona ni wachache, hivyo mradi huu utakuwa suluhisho,”anasema.

Ubunifu wa mashine hiyo

Anasema mashine hiyo wameitengeneza kwa kutumia vifaa vya kawaida, kwa kuwa hawana uwezo wa kununua vile vya kisasa.

“Tunatengeneza kifaa kinaitwa ‘gard block’ ambacho tunachanganya saruji na udongo halafu tunaweka chupa ya soda katikati ili kupata tundu litakalotuwezesha kuweka bomba” anaeleza.

Anasema kifaa hicho kinachokaa kwa siku mbili ili kikauke baada ya hapo kinaunganishwa moja kwa moja kwenye mashine.

“Baada ya hapo kuna kamba inatoka juu inaingia ndani ya kisima ambayo tunaiunganisha kwenye gurudumu, hivyo upepo unapokuja gurudumu linazunguka na maji nayo yanapanda,”anaeleza.

Anasema baada ya kupata wazo la kuanzisha mradi huo, walijifunza kwanza jinsi ya kutengeneza Windmli kupitia mtandao wa kijamii wa Youtube na kuona jinsi gani wengine wanavyotengeneza.

Kabla ya kutengeneza mashine hiyo kundi hili hufanya kwanza utafiti katika eneo ambalo mashine hiyo itafungwa, kikubwa wakiangalia upatikanaji wa maji katika eneo hilo.

Baada ya kugundua hali halisi ya eneo hilo, Kifungu anasema huamua aina gani ya mashine itumike kati ya ndogo au kubwa.

Anasema ubunifu wa kutengezeza mashine za kuvuta maji kwenye kisima kwa kutumia upepo unafanywa na kampuni kubwa katika mataifa mbalimbali kama Canada na Marekani.

“Nasi Tanzania kama tutaamua kuwekeza katika teknolojia hii, tunaweza kuingia katika soko la kidunia. Sio tu itatuwezesha kutatua changamoto ya maji, lakini itasaidia kuwatoa vijana katika wimbi la ukosefu wa ajira na kuwa wabunifu mashuhuri duniani”anaongeza.

Kuhusu gharama anasema wanauza kuanzia Sh 25 milioni hadi 50 milioni, huku wateja wao wakubwa wakiwa ni wakulima na wafugaji.

Changamoto

Kifungu anasema changamoto inayowakabili katika kundi lao ni mtaji. Anasema unahitajika mtaji wa kutosha kwa kuwa mradi wao unapitia njia mbalimbali, ikiwamo kutembelea mikoa mbalimbali kuangalia sehemu zenye changamoto ya maji.

“Kama ilivyo hapa, tupo 10, lakini ni vijana wadogo, tunahitaji kuwa na mtaji mkubwa zaidi ili tuweze kufanya vizuri. Wakati mwingine anakuja mtu hapa anahitaji mashine ya zaidi ya Sh 50 milioni, lakini tunakosa mtaji wa kuitengeneza mashine hiyo,” anasema na kuongeza:

“Ukiondoa changamoto za vifaa na mtaji, hata wateja hawapatikani kwa wingi kama tulivyotarajia. Hii inaonyesha bado jamii haijawa na mwamko juu ya teknolojia hii”.

Malengo yao

Vijana wa kundi la Tim wanalenga kutengeneza mashine nyingi ambazo wanaamini kuwa zitatatua changamoto ya maji katika maeneo mbalimbali, baada ya kubaini kuwa maji ndiyo changamoto kubwa nchini.

Kifungu anasema mradi wao utaambatana na mafunzo kwa vijana wengine.

“Kama kundi tumepanga kufundisha vijana wengi juu ya utengenezaji wa mashine hizi, kwani tukiwa wengi ndivyo tutakavyowafikia wananchi wengi zaidi.

Tuna malengo pia ya kuwa wabunifu wakubwa Tanzania katika utengenezaji wa mashine hizi na ikiwezekana tuuze nje ya nchi,”anaeleza.

Wito kwa Serikali

Kifungu anatoa rai kwa Serikali kutoa kipaumbele kwa vijana ambao wanafanya ubunifu wa vitu mbalimbali vyenye manufaa katika jamii na taifa kwa jumla.

Anasema kama ubunifu wa kuvuta maji kutoka kisimani kwa kutumia upepo kupitia mashine ya upepo itapewa kipaumbele, Tanzania inaweza kufika mbali katika utatuzi wa changamoto ya maji.

“Serikali itumie fursa hii ya mashine za upepo na kuzitumia katika maeneo mbalimbali yenye shida ya maji. Sisi tupo tayari kwenda popote kwa ajili ya kutatua changamoto ya maji kwa jamii, watendaji husika wa Serikali watutembelee waone kazi zetu,’’ anaeleza.