Tirdo kuzalisha mkaa wa makaa ya mawe Machi

Muktasari:

  • Mkurugenzi Mkuu wa Tirdo, Profesa Mkumbukwa Mtambo amebainisha hayo wakati wa utiaji saini makubaliano ya pamoja ya utengenezaji wa nishati hiyo baina ya shirika lake na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kw akushirikiana na Shirika la Nyumbu (TATC).

Shirika la Utafiti na Maendeleo ya Viwanda Tanzania (Tirdo) linakamilisha mchakato wa kuanza kutengeneza mkaa unatokana na makaa ya mawe (briquette) kwa ajili ya matumizi ya nyumbani.

Mkurugenzi Mkuu wa Tirdo, Profesa Mkumbukwa Mtambo amebainisha hayo wakati wa utiaji saini makubaliano ya pamoja ya utengenezaji wa nishati hiyo baina ya shirika lake na Shirika la Maendeleo la Taifa (NDC) kw akushirikiana na Shirika la Nyumbu (TATC).

Kwa muda mrefu makaa ya mawe yamekuwa yakitumika kwa uzalishaji wa viwanda pekee lakini sasa shirika hilo linaona ni wakati muafaka wa kuongeza vyanzo vya nishati kwa ajili ya kupikia.

“Kupitia maabara yetu ya kisasa ya makaa ya mawe, tumefanya utafiti ili kubaini athari za kiafya na kimazingira zinazotokana na makaa ya mawe kwa kipindi cha miezi sita kuanzia June 2017 hadi Novemba mwaka jana, kabla ya kuanza kuzalisha nishati hii,” alisema Profesa Mtambo.

Lengo la makubaliano ya taasisi hizo tatu, Profesa Mtambo alifafanua kuwa ni kutengeneza mkaa huo kwa ajili ya matumizi ya nyumbani badala ya kutumika viwandani pekee.

“Kupitia utafiti wetu, tumejiridhisha kwamba tunaweza kutengeneza mkaa unatokana na makaa ya mawe baada ya kupunguza nguvu na moto mkali uliopo katika makaa hayo,” alifafanua.

Awali, Mkurugenzi wa Utafiti na Ubunifu wa Shirika la Nyumbu, Dk Lawrence Kerefu alisema hadi Machi uzalishaji wa mkaa huo utakuwa umeanza na kuwa tayari kwa ajili ya matumizi ya nyumbani kwani usanifu wa mashine na mitambo ya kuzalisha nishati hiyo umeshakamilika kwa zaidi ya asilimia 50.

“Hadi Februari mwishoni tutakuwa tumemaliza kufanya usanifu wa mashine na mitambo ya kuzalisha nishati hii na kitakachofuata ni kuanza rasmi kuzalisha mkaa unaotokana na makaa ya mawe,” alisema Dk Kerefu.

Dk Kerefu alisema ni vizuri wananchi wakaachana na mkaa unatokana na kuni badala yake wakatumia wa makaa ya mawe ili kutunza mazingira.

Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Taifa la Maendeleo (NDC), Ramson Mwilangali alisema makubalinao hayo ni mwendelezo wa kukuza viwanda kwa sababu nchi ina utajiri wa makaa ya mawe hivyo ni vizuri kutumika kwa matumizi ya nyumbani na kupunguza uharibifu wa mazingira unatokana na ukataji wa miti kwa ajili ya kuchoma mkaa.

Takwimu zinaonyesha zaidi ya hekta 300,000 za misitu huvunwa kila mwaka kwa ajili ya kuchoma mkaa jambo linalohatarisha mazingira na kuchochea mabadiliko ya tabianchi.

Zaidi ya nusu ya mkaa wote unaochomwa nchin unatumika Dar es Salaa, jiji lenye takriban wakai milioni sita. Vijijini, watu wengi pia wanatumia kuni ambazo huchangia uharibifu na uchafuzi wa mazingira.