Wednesday, January 11, 2017

UCHAMBUZI: Tuache siasa katika kukabiliana na upungufu wa chakula

 

By Mussa Juma,Mwananchi

Maeneo mengi nchi kwa sasa yanakabiliwa na upungufu wa chakula kutokana na mavuno kidogo ya msimu uliopita.

Hali ya upungufu wa chakula inatarajiwa kuongezeka zaidi hasa kutokana na maeneo mengi kukosa mvua za vuli.

Kwa sasa bei ya nafaka imepanda, karibu maeneo mengi nchini na hifadhi ya chakula katika maghala ya Taifa imepungua.

Bei ya nafaka kama mahindi, imepanda katika maeneo mengi nchini kutoka Sh50,000 miezi minne iliyopita hadi sasa kufikia kati ya Sh80,000 hadi Sh100,000 kwa gunia.

Ununuzi wa chakula katika maghala kwa msimu wa kilimo uliopita umepungua tofauti na miaka ya nyuma.

Kwa mfano, kwa ghala la Taifa kanda ya kaskazini, lengo la kununua mazao lilikuwa ni tani takriban 15,000, lakini zilizonunuliwa ni tani takriban 5,000 tu.

Upungufu huu wa chakula umesababishwa na sababu mbalimbali, kwanza ni mbadiliko ya tabia nchi, ambayo yanaathiri maeneo mengi duniani.

Pili ni upungufu wa mvua na zana bora za kilimo katika maeneo mengi na tatu kutodhibitiwa ipasavyo kuuzwa chakula nje ya nchi.

Hivyo maeneo mengi kukabiliwa na upungufu wa chakula siyo dhambi na haitokani na uzembe wa viongozi ama wakulima.

Hata hivyo kama ambavyo, iliwahi kutokea miaka ya nyuma, kwa sasa taarifa za wilaya mbalimbali kukumbwa na upungufu wa chakula zimekuwa za kisiasa.

Ni viongozi wachache, wameweza kutoa matamko hadharani kuwa maeneo yao yana upungufu wa chakula.

Miaka ya nyuma kuliwahi kutolewa tamko kuwa kiongozi ambaye atatoa taarifa za njaa katika wilaya yake atahesabika kama ni mzembe kwa kashindwa kutekeleza wajibu wake.

Tamko hilo lililalamikiwa na asasi mbalimbali yakiwapo mashirika yasiyo ya kiserikali na hata wananchi kwani viongozi waliogopa kusema ukweli.

Kutokana na hofu za viongozi, ilitokea baadhi ya maeneo walikabiliwa na njaa kali hadi kula mizizi, lakini viongozi walikanusha na kutishia kuwachukulia hatua bila ridhaa yao.

Hali hii imeanza kujionyesha hivi sasa kwani baadhi ya viongozi wetu sasa wanapata hofukueleza ukweli juu ya upungufu wa chakula katika maeneo yao.

Naomba nirejee kusema, wilaya kukabiliana na upugufu wa chakula siyo dhambi na uzembe wa wananchi ama viongozi suala hili kwa kiasi kikubwa lipo juu ya uwezo wao.

Hivyo katika kukabiliana na tatizo la upungufu wa chakula ni vyema siasa ikawekwa kando ili kubuniwa mikakati ya kuhakikisha hakuna mtu ambaye atakufa kwa njaa.

Mikakati hii ya kukabiliana na upungufu wa chakula itafanikiwa tu iwapo viongozi katika maeneo husika watakuwa wakweli kwa kukiri upungufu wa chakula katika maeneo yao.

Hivyo sasa ni wakati mwafaka kwa viongozi kuhakikisha wanafanya uhakiki wa hali ya chakula katika maeneo yao na baadaye kutoa taarifa sahihi juu ya mahitaji halisi ya chakula.

Hata hivyo, kama tukitaka suala la upungufu wa chakula kulifanya la kisiasa tutawaumiza bila sababu wananchi ambao wengi hivi sasa wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha.

Nimalize kwa kutoa wito kwa Serikali, wanasiasa, viongozi wa dini, mashirika yasiyo ya kiserikali (NGOs) na wadau wengine kulichukulia kwa uzito unaostahili suala la upungufu wa chakula katika maeneo mengi nchini.

Mussa Juma ni mchambuzi na mwandishi wa gazeti hili Mkoa wa Arusha. Anapatikana kwa simu 0754296503 na baruapepe:mjuma@mwananchi.co.tz.

-->