Tuanze mzizi wa kuporomoka kwa elimu

Muktasari:

  • Wala tusiwaone Watanzania wanaokosoa mfumo wetu wa utoaji wa elimu kama wachochezi ama wasioitakia mema nchi, bali tuwaone ni wazalendo wenye lengo la kuiboresha elimu yetu.

Katika moja ya mijadala iliyotikisa Bunge la bajeti linaloendelea mjini Dodoma ni kudidimia kwa elimu nchini, lakini nionavyo mimi, tusitoe majibu ya kisiasa tutafute mzizi wake.

Wala tusiwaone Watanzania wanaokosoa mfumo wetu wa utoaji wa elimu kama wachochezi ama wasioitakia mema nchi, bali tuwaone ni wazalendo wenye lengo la kuiboresha elimu yetu.

Nimefarijika sana na kauli ya Serikali bungeni kuwa iko kwenye mchakato wa kuandaa mjadala wa kitaifa unaolenga kuboresha elimu, hoja iliyowahi kutolewa na Rais mstaafu Benjamin Mkapa.

Kauli hii yenye kutia moyo, ilitolewa na Naibu Waziri ofisi ya Rais (Tamisemi), Joseph Kakunda, wakati akijibu swali la Mbunge wa Vunjo, James Mbatia aliyesema kuna udhaifu mkubwa sekta ya elimu.

Lakini, Waziri mwenye dhamana ya Elimu, Profesa Joyce Ndalichako, naye aliiagiza Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU) na Baraza la Vyuo vya Ufundi (Nacte), navyo kuchukua hatua.

Profesa Ndalichako aliziagiza TCU na Nacte kufanya mapitio upya ya nyenzo wanazotumia kukagua ubora wa vyuo, watakapobaini havikidhi ubora wavifunge bila kuogopa hata kama ni vya Serikali.

Pia, aliwaagiza maofisa elimu kote nchini, kusimamia kwa karibu ubora wa elimu katika shule zote za msingi na sekondari na mimi nasema mzizi wa tatizo unaanzia bora wa elimu katika ngazi hii.

Zipo changamoto nyingi kama nitakavyojaribu kuzitaja, ambazo naamini ndizo zinazochangia kudidimiza elimu yetu hasa bajeti ndogo inayotengwa kwa ajili ya elimu msingi hadi sekondari.

Japokuwa Serikali ya Awamu ya Tano imeongeza bajeti kwenye elimu, lakini bado haitoshi na wala haijaweka wazi Serikali inatumia asilimia ngapi ya pato la Taifa GDP) kwenye elimu.

Kwa mujibu wa EAC fact figures, mwaka 2016 Tanzania inatumia asilimia 1.1 hadi 1.4 ya GDP kwenye elimu msingi wakati Kenya walifika hadi 7.2, Rwanda 6.0, Uganda 3.8 na Burundi 7.2

Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) linapendekeza asilimia 6 ya GDP wakati Benki ya Dunia asilimia 5 sisi bado tuko 1.1 na hatujafikisha hata asilimia 2.

Kutokana na bajeti ndogo, mishahara ya walimu iko chini haiwavutii wenye ufaulu wa juu wa darala la 1 na 2 kujiunga na ualimu wakati nchini Finland ualimu ni kozi ya kwanza wanayopigania.

Ni upungufu huo wa bajeti unafanya mabadiliko ya mitaala haiwafikii walimu wote kwani wachache wanapewa mafunzo wakitegemewa kuwa nao watatoa mafunzo kwa wenzao wakirudi shuleni.

Wanaporudi shuleni hawapati ushirikiano wa wenzao kwani wanawaona kuwa wao walikwenda kwenye mafunzo wakalipwa, inakuwaje wanakuwa wanatoa mafunzo hayo kwao bila malipo?

Si hivyo tu, lakini kutokana na bajeti ndogo miundombinu shuleni, vitendea kazi na nyumba za walimu ni shida na ieleweke asilimia 75 ya shule ziko vijijini ambapo hakuna nyumba za walimu.

Lipo tatizo la motisha kwa walimu kwa kutolipwa kwa wakati madeni yao, kutopandishwa madaraja, kutopewa fedha za likizo na wao kutojaliwa na watu au jamii inayowazunguka kama siku za nyuma..

Lipo tatizo la Waziri wa Elimu kutokuwa na Baraza la kumshauri kama sheria inavyoelekeza, matokeo yake yeye ndiye elimu na elimu ndiye yeye vipaumbele vyake ndiyo vipaumbele vya Taifa.

Hali hii husababisha nchi kutokuwa na mwelekeo katika usimamizi na uendeshaji wa Elimu nchini kwa sababu kila waziri anakuja na sera yake na siyo ya Taifa na yeye ndio anageuka kamusi ya elimu.

Nitoe mfano mwaka 2000-2005 aliyekuwa Waziri wa Elimu, marehemu Joseph Mungai alitumia madaraka yake ya uwaziri akaamua fizikia na kemia zifundishwe kama somo moja.

Mitaala ikatungwa, vitabu vikatengenezwa, serikali ikaweka fedha lakini alipokuja waziri mwingine akafuta yale ya Mungai kwa sababu Waziri ndiye anayefanya ni kamusi ya elimu.

Ndio maana nimetangulia kusema, huu ni wakati wa kutafuta mzizi wa kuporomoka kwa elimu yetu, tukishaweka mambo sawa kwenye elimu ya msingi na Sekondari, hata vyuoni mambo yatakuwa sawa.