MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Tujivunie thamani ya Kiswahili chetu

Muktasari:

  • Mchungaji huyo maarufu kwa jina la Mzee wa Upako, alisema kuwa laiti angekuwa na mamlaka, angekifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia, kwa kuwa ni lugha ambayo Watanzania wanaijua vizuri.
  • Mzee wa Upako alidokeza kuwa, Tanzania ni nchi yenye dhima kubwa katika ukombozi wa nchi nyingine za Kiafrika.

Hivi karibuni Mchungaji Anthony Lusekelo wa Kanisa la Maombezi (GRC) lililopo Ubungo Kibangu, jijini Dar es Salaam, amekitaja Kiswahili kuwa ni lugha bora kuliko lugha nyingine.

Mchungaji huyo maarufu kwa jina la Mzee wa Upako, alisema kuwa laiti angekuwa na mamlaka, angekifanya Kiswahili kuwa lugha ya kufundishia, kwa kuwa ni lugha ambayo Watanzania wanaijua vizuri.

Mzee wa Upako alidokeza kuwa, Tanzania ni nchi yenye dhima kubwa katika ukombozi wa nchi nyingine za Kiafrika.

Alieleza kazi kubwa iliyofanywa na Mwalimu Julius Nyerere, katika kuzisaidia baadhi ya nchi za Kiafrika kujinasua kutoka utawala wa kikoloni. Akifafanua hayo, alieleza upekee wa Tanzania unaojipambanua katika lugha ya Kiswahili.

Akifananisha baadhi ya maneno ya Kiswahili na visawe vyake katika lugha za kigeni, anasema kuwa Kiswahili ni lugha yenye ladha tamu na laini kutamkwa kinywani.

Aliongeza kuwa, Tanzania ni nchi pekee yenye lugha yake yenyewe ukilinganisha na nchi nyingine za Afrika.

Alisema: “Kiswahili ni lugha yenye heshima na hadhi kubwa duniani. Katika Afrika, Kiswahili ni lugha ya pili kimatumizi na hadhi; na kati ya lugha za dunia Kiswahili ni lugha ya saba duniani.”

Alieleza kuwa kwa sababu ya hadhi hiyo kimataifa, Kiswahili hakina budi kupewa nafasi ya pekee katika elimu.

Alisisitiza akisema, “Ningekuwa mimi kiongozi ningesema Kiingereza kifundishwe kama somo na Kiswahili kitumike kama lugha ya kufundishia masomo yote katika viwango mbalimbali vya elimu.”

Akitoa msisitizo huo, alionyesha kuwahurumia Watanzania akisema, “Nawahurumia Watanzania! Kati ya Watanzania 100, wanaojua Kiingereza ni wawili.” Kutokana na takwimu hizi alieleza kuwa kuendelea kufundisha kwa Kiingereza ambacho wengi hawakijui badala ya Kiswahili ni kuwachanganya watoto.

Aidha, alisisitiza kuwa, nchi nyingi zenye maendeleo makubwa duniani, zimekuwa zikitumia lugha zake katika elimu, sayansi na teknolojia; lakini siyo kwa kutumia lugha za mkopo. Alieleza pia kwamba, Nigeria inatabiriwa kuwa nchi kubwa baada ya miaka 20 ijayo. Hata hivyo, akaeleza kuwa litakuwa taifa lisilokuwa na lugha yake.

Fauka ya hayo, ameeleza kuwa Kiswahili sasa kimepewa nafasi kubwa katika Bunge la Afrika Mashariki na ni lugha rasmi katika Bunge la Afrika. Amesema kwamba, aliwahi kupata nafasi ya kuzungumzia umuhimu wa Kiswahili katika Bunge la Afrika Mashariki akiwa na marehemu Abdallah Kigoda na Celina Kombani na mchango wao ukazaa matunda.

Nikimwacha Mzee wa Upako, huko Zanzibar, Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif Ali Idi ameeleza umuhimu na nafasi ya Kiswahili nchini Tanzania. Anasema kuwa, Kiswahili ni moja ya nguzo muhimu za uchumi hapa nchini. Makamu huyo wa Rais, aliyasema hayo katika hafla ya usiku wa Kiswahili uliojumuisha wanachama wa Chalukita iliyofanyika huko Zanzibar hivi karibuni. Vilevile, alilitaka Baraza la Kiswahili la Taifa (Bakita) kupambana kwa nguvu zote dhidi ya wale wanaokibananga Kiswahili ili kuhakikisha kinatumika ipasavyo.

Alisisitiza pia kuwa, ufundishaji wa lugha ngeni uendane na utamaduni wa Waswahili.

Wapenzi wafuatiliaji wa safu hii, Kiswahili ni lugha ya thamani kwetu. Wakati fulani baadhi yetu wanashindwa kulitambua hilo kwa sababu ya kutukuza vya wageni na kuvibeza vyetu.

Maneno ya Mzee wa Upako na Balozi Seif Ali Idi yatuzindue akili kukienzi Kiswahili chetu na kukitumia kujiimarisha kiuchumi.