Tukio la kipigo cha mwanafunzi Mbeya linaashiria mgogoro mpana

Wazazi wakiwa kwenye mkutano katika shule ya Sekondari Vikindu mkoani Pwani. Ushirikiano kati ya walimu na wazazi ni chachu kubwa katika kudhibiti nidhamu shuleni. Picha na blog ya innobanzi

Muktasari:

  • Walimu wanalalamika kuwa bodi za shule zikipelekewa wanafunzi wakorofi wanawatetea na kuwaacha waendelee na masomo, kitendo ambacho huwapa kiburi zaidi wanafunzi hao na kuamua kuendelea kuwafanyia vitendo viovu walimu wao.

Upashanaji habari kwa sasa umerahishiswa  tofauti na zamani. Hii yote ni matunda ya utandawazi. Tunazungumza zaidi kwenye mitandao ya kijamii kuliko kuonana ana kwa ana.

Hata lilipotokea sakata la walimu kumuadhibu mwanafunzi wao kinyume na maadili ya ualimu mkoani Mbeya, taarifa na picha zilisambaa kwenye mitandao.

Mbali ya kushabikia au kusikitikia kilichotokea,  tujadili jambo ambako tunaweza kujifunza kutokana na tukio hili kwa kuangalia haki za wanafunzi na wajibu wao kwa walimu.

Vilevile, tuangalie haki za walimu na wajibu wao katika malezi ya wanafunzi.

Jambo kubwa tunalojifunza ni kwamba hata kama watu wengi watakubaliana na hukumu ya jamii kuhusiana na kitendo kile cha kikatili,  bado kuna mgogoro mkubwa wa uhusiano kati ya wanafunzi, walimu na wazazi.

Sheria na kununi zinasemaje?

Sheria ya haki za mtoto ya mwaka 2009 inatafsiri mtoto ni mtu yeyote mwenye umri chini ya miaka 18. Kwa hiyo, mwanafunzi aliyesulubiwa, Sebastian Chinguku kwa mujibu wa sheria anatambuliwa kama mtoto.

Sehemu ya 12 ya sura ya pili ya sheria hii inasema:  “Mtu yeyote hataruhusiwa kumfanya mtoto apate mateso, adhabu ya kikatili, ya kinyama au matendo yenye kumshushia hadhi.”

Sheria hiyo pia inasema: “Hakuna adhabu kwa mtoto inayokubalika ambayo imekithiri kwa matendo au kwa kiwango kulingana na umri, hali ya mwili na akili yake. Hakuna adhabu inayokubalika kwa ajili ya umri mdogo wa mtoto au vinginevyo kwa sababu mtoto hawezi kuelewa nia ya adhabu hiyo”.

Kifungu kinamaanisha kuwa mtoto hapaswi kufanyiwa vitendo vya kikatili vitakavyoshusha utu wake na kumdhalilisha.

Pia adhabu lazima itolewe kwa lengo la kumrekebisha mtoto na kumsadia aweze kuwa mtu mwema kwa familia yake, jamii yake na taifa.

Kimsingi, wanaopiga kelele kuwa adhabu ya viboko iondolewe shuleni wanasema huumiza mwili wa mtoto na wakati mwingine kumfanya achukie masomo au kushindwa kuendelea na masomo kutokana na majeraha.

Vilio vya makundi ya kutetea haki za watoto pamoja na sheria ya haki za watoto ya mwaka 2009, viliifanya wizara  kutoa mwongozo kuhusu adhabu shuleni kupitia waraka wa elimu namba 24 wa mwaka 2002.

Miongoni mwa maelekezo katika waraka ule ni kuwa viboko vitatolewa kwa ajili ya makosa makubwa. Walimu wengi wanasema makosa hayo ni kama vile wizi, uvutaji wa bangi, kupigana na wenzake na uharibifu wa mali za shule na za wenzake.

Waraka pia unaagiza, mwalimu mkuu ndiye mwenye mamlaka ya kuruhusu kimaandishi au mwenye kutoa adhabu hiyo. Na viboko visizidi vinne na viandikwe kwenye kitabu cha kumbukumbu.

Kwa ushahidi huu, bado kwa namna yoyote ile Chinguku  hakustahili kipigo kile. Hata hivyo, tukio zima linatufundisha nini?

Mgogoro kati ya walimu, wazazi na bodi za shule

Inaonekana usimamizi wa maadili shuleni unakwamishwa na siasa zaidi pale  wanafunzi wanapotetewa zaidi kuliko walimu, ambao mara kadhaa tumesikia kuwa nao wamekuwa wakidhalilishwa na wanafunzi.

Walimu wanalalamika kuwa bodi za shule zikipelekewa wanafunzi wakorofi wanawatetea na kuwaacha waendelee na masomo, kitendo ambacho huwapa kiburi zaidi wanafunzi hao na kuamua kuendelea kuwafanyia vitendo viovu walimu wao.

 Wazazi wa kisasa wamekuwa hawana ushirikiano mzuri na walimu kiasi kwamba watoto wanasikilizwa zaidi hata kama wanaambiwa makosa yao na walimu.

Hali hii ndiyo huwafanya walimu kuwa na uhusiano mbaya na wanafunzi kiasi kwamba wanaamua kuacha kurekebisha maadili yao kwa kuwa hata wakifanya jitihada hizo, bado bodi za shule na wazazi hawawaungi mkono.

Huenda hali hii imekuwa zaidi katika shule za Serikali kuliko za binafsi ambazo mzazi asipokubaliana na masharti ya shule, anaambiwa mwanawe hana nafasi.

Kizazi kipya cha walimu wasiopenda ualimu

Kwa miaka ya hivi karibuni, tumekuwa na vijana wanaokwenda kusomea ualimu kama njia ya kupata ufadhili wa masomo vyuoni au kwa kuwa nafasi pekee yenye uhakika wa ajira serikalini ni ualimu. 

Mbali na hilo, siku hizi tangu kuwapo kwa mabadiliko mengi ya mfumo wa elimu, tumekuwa tukishuhudia vijana wadogo wakimaliza vyuo kati ya miaka 21 hadi 23 na kupangiwa shule.

Matokeo yake walimu hawa vijana wanajikuta kutokana na umri wao wanaanza uhusiano wa mapenzi na wanafunzi, au kuwa karibu  nao wakiwachukulia kama wadogo zao na siyo walimu wao.

Pia, wapo wale watakapoona wanalingana na wanafunzi wao kwa umbo na umri wanalazimika kutumia adhabu kali kwa wanafunzi, kwa lengo la kuwafanya wawaheshimu kama walimu.

Inasemekana pia wanafunzi wengi wa ualimu wakienda mafunzo ya vitendo huwekwa pamoja katika ofisi moja na hivyo hukosa malezi, miongozo na usimamizi wa walimu wazoefu.

Wanakuwa huru kufanya lolote wanalotaka na matokeo yake mengine yanakuwa kinyume cha maadili ya ualimu. Kwa mujibu wa kanuni za mafunzo kwa vitendo, mwanafunzi wa ualimu haruhusiwi kumuadhibu mwanafunzi.

Tufanyeje ?

Kwa wale waliosomea ualimu vyuoni wanafundishwa kuhusu saikolojia ya ujana na namna ya kuwalea wanafunzi katika kipindi cha kubalehe.

 Mwalimu anayeijua vizuri kazi yake anaelewa kuwa umri ule wa vijana huwa ni wa usumbufu na kila mmoja katika maisha yake amepitia umri huo, japo   kwa njia tofauti.

Walimu  na wazazi wanapaswa kuweka msingi bora wa malezi ya vijana wetu ili wanapofikia umri wa kubalehe wasiwe na matatizo mengi shuleni.

Kwa bahati mbaya, wazazi wengi tunashindwa kutimiza wajibu wetu wa kuwalea na kuwahudumia watoto wetu na matokeo yake wanajikuta wanafundishwa na ulimwengu.

Ipo haja ya halmashauri zetu kujenga shule nyingine ili kupunguza mzigo kwa shule chache kuelemewa na wa wanafunzi. Ukiwa na darasa moja lenye mikondo mingi kiasi cha kuwa na wanafunzi hadi 300 ni changamoto kubwa katika usimamizi. Mbeya Day ni shule iliyoelemewa  na idadi kubwa ya wanafunzi.

Serikali ihamishie jitihada zake kwa kuboresha mafunzo ya walimu, kupunguza mzigo wa kufundisha vipindi vingi kwa wiki pamoja na kuboresha masilahi yao. Hii pamoja na mengineyo itawapa nafasi walimu kusimamia vizuri nidhamu za wanafunzi.

Mwandishi ni mchambuzi wa masuala ya jamii. 0787 525 396