UCHAMBUZI: Tukishikamana tutaondoa ajali barabarani

Muktasari:

Ajali za barabarani zinaweza kuzuilika iwapo kila mmoja atatumia nafasi yake kuhakikisha zinapungua na kuondokana na machungu ya madhara yake.

Umefika wakati Watanzania tunahitaji kukataa ajali zinazoepukika hasa za barabarani kwani zimegharimu maisha ya wengi.

Ajali za barabarani zinaweza kuzuilika iwapo kila mmoja atatumia nafasi yake kuhakikisha zinapungua na kuondokana na machungu ya madhara yake.

Nalazimika kuandika makala hii hasa kutokana na ajali iliyotokea hivi karibuni huko wilayani Karatu, Arusha ikihusisha wanafunzi wa Shule ya Msingi Lucky Vincent. Ilisababisha vifo vya wanafunzi 32, walimu wawili na dereva hivyo kuacha vilio na majonzi kwa maelfu ya Watanzania huku nguvu kazi kubwa ya Taifa ikipotea.

Kwa mujibu wa taarifa za Shirika la Afya Duniani (WHO) ya mwaka 2015, watu milioni 1.25 hufa kila mwaka kutokana na ajali za barabarani na kati ya asilimia 20 mpaka 50 milioni hubaki na ulemavu wa kudumu.

Kwa Tanzania, takwimu hizo zinaonyesha mwaka 2015 watu 3,462 walifariki dunia katika ajali 8,337 zilizotokea huku majeruhi 9,383 wakibaki na majeraha au ulemavu. Mwaka jana waliofariki dunia kwa ajali walikuwa 3,256 kutoka kwenye ajali 5,152 zilizotokea ambazo zilishababisha majeruhi 8,958.

Takwimu hizi zinaonyesha ukubwa wa tatizo. Naamini, ajali hizi zinazuilika iwapo tutaunganisha nguvu kwa pamoja. WHO inataja mambo matatu yanayochangia kwa kiasi kikubwa ajali za barabarani ambayo ni mwendokasi, ulevi na uzembe.

Visababishi vilivyotajwa vinaweza kuzuilika iwapo dereva atasimamia nafasi yake kikamilifu na askari wa usalama barabarani na abiria watatekeleza wajibu wao kama inavyotakiwa. Uchunguzi wa chanzo cha ajali ya Arusha unaendelea. Baada ya ajali ile, nilijaribu kutafakari; kati ya ulevi, mwendokasi na uzembe ni kipi kinaweza kuwa chanzo?

Ajali imeshatokea lakini kuna hatua zinapaswa kuchukulia ili kupunguza madhara yatokanayo na ajali kama vifo na majeruhi. Ufungaji wa mikanda ni moja ya hatua muhimu za kupunguza madhara yatokanayo na ajali hizi kwa utafiti unaonyesha abiria wa kiti cha mbele akifunga mkanda anazuia madhara kwa asilimia 50 wakati wa viti vya nyuma akifanya hivyo hupunguza kwa asilimia 70.

Sitaki kuamini kuwa wanafunzi wale walisafiri bila kufunga mikanda, lakini kwa hali ilivyokuwa, inawezekana hawakufanya hivyo.

Watanzania bado tunahitaji elimu ya usalama barabarani kwani ajali ni janga. Elimu hii inahitajika kuanzia shuleni, kazini na ikibidi vijiweni ili kuhakikisha kila mtu anakuwa mlinzi wa mwenzie awapo barabarani.

Chama Cha Waandishi wa Habari Wanawake (Tamwa) ni miongoni mwa taasisi zinazotoa elimu hii. Imejikita zaidi katika kutetea masilahi ya wanawake kwani waathirika wakuu wa ajali za barabarani ni wanaume ambao hupoteza zaidi maisha kuliko wanawake, hivyo kuwaacha wajane na majukumu yote ya kutunza familia.

Umefika wakati; mashirika na taasisi nyingine kusimama imara kuhakikisha elimu ya usalama barabarani inatolewa kwa watu wote.

Haina maana kuendelea kuwaachia askari wa usalama barabarani na Sumatra kusimamia jukumu hili kwani kufanya hivyo ni kuruhusu tuendelee kuteketea kwenye ajali za barabarani.

Katika hili ni vema kila msafiri akawa msimamizi wa sheria za barabarani ikiwamo kukemea uendeshaji wa kizembe, mwendokasi na kumkataa dereva aliyelewa atakapoonekana kukabidhiwa usukani.

Abiria wakipaza sauti na madereva wakawa makini kutekeleza majukumu yao, ajali zitapungua.

Mchambuzi ni mwandishi wa Mwananchi mkoani Morogoro. Anapatikana kwa namba 0714 273 333.