Tulivyoipa kisogo elimu ya awali

Muktasari:

Ikiwa utaratibu hautafuatwa katika kujenga msingi imara, nyumba itaanguka wakati wowote na inawezekana ikaanguka wakati ujenzi ukiendelea au miaka michache baada ya ujenzi kukamilika.

Ujenzi wa nyumba imara unahitaji msingi uliokamilika. Msingi bora na imara hujengwa na fundi mwenye weledi mkubwa, huku akizingatia ubora vifaa anavyotumia.

Ikiwa utaratibu hautafuatwa katika kujenga msingi imara, nyumba itaanguka wakati wowote na inawezekana ikaanguka wakati ujenzi ukiendelea au miaka michache baada ya ujenzi kukamilika.

Elimu ya awali iliyo bora ndio msingi wa kupata wahitimu walio bora katika ngazi zote.

Elimu hii ndio huandaa na kujenga msingi mizuri kwa mwanafunzi kabla ya kujiunga na elimu ya msingi, kisha sekondari na hatimaye kuhitimu masomo ya elimu ya juu.

Wadau wa elimu nchini Tanzania wanaamini kwa kiasi kikubwa kwamba endapo elimu ya awali nchini Tanzania itatolewa katika misingi inayostahiki itakuwa ni njia moja wapo madhubuti ya kuimarisha ubora wa elimu.

Hii ndiyo maana wanaendelea kupaza sauti wakiitaka Serikali kupitia vyombo husika kuboresha kwanza elimu ya awali kabla ya kupanda ngazi nyingine za juu.

Katika kuhakikisha kuwa elimu ya awali inatolewa kwa watoto wa Kitanzania, Serikali kupitia Sera ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 1995 na tamko la iliyokuwa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi la mwaka 2010, iliagiza kuwa katika kila shule ya msingi nchini, ni lazima lianzishwe darasa la elimu ya awali ili kuweza kuwaandaa wanafunzi kuingia darasa la kwanza.

Hata katika Sera mpya ya Elimu na Mafunzo ya mwaka 2014, suala la elimu ya awali limepewa kipaumbele lakini pia umri wa mtoto kuandikishwa kujiunga na elimu hii umeshushwa kutoka miaka mitano hadi miaka minne, hii ikiwa na tafsiri kuwa watoto wengi watapata fursa ya kupata elimu ya awali kabla ya kujiunga na darasa la kwanza.

 

Changamoto za elimu hii

Licha umuhimu wa elimu ya awali kuwa wazi kwa muda mrefu, bado uwekezaji wake umekuwa ni wa shaka kwani utolewaji wa elimu hiyo umekumbwa na changamoto nyingi.

Miongoni mwa changamoto hizo ni upungufu wa walimu wenye sifa, uhaba wa zana za kufundishia na kujifunzia, madarasa yasiyokidhi viwango, madawati, vyoo, lakini pia umbali kati ya shule na mahali wanapotoka watoto hawa.

Cha kusikitisha zaidi, utolewaji wa elimu ya awali nchini umekuwa ni wa matamko zaidi kuliko vitendo, huku Serikali ikishindwa kutenga bajeti kwa ajili ya kuhudumia elimu hii na hivyo mzigo wa uendeshaji wa madarasa ya elimu ya awali kubaki kwa walimu, wazazi na kamati za shule.

Darasa kwa ajili ya elimu ya awali linapaswa kuendana na mtoto kulingana na umri na utimamu wa maumbile linalompa mtoto nafasi ya kufanya vitendo vya masomo.

Ukubwa wa madawati, urefu wa makabati na shubaka za kuhifadhia zana na vifaa vya kufundishia na kujifunzia ni lazima uzingatiwe. Cha muhimu zaidi ni kuwa mtoto wa elimu ya awali anahitaji chakula chenye virutubisho vyote muhimu ili aweze kukua na kupata uwezo wa kujifunza kikamilifu.

Suala la michezo pia ni muhimu sana katika maisha ya kila siku ya mtoto, Michezo humsaidia mtoto kujifunza stadi mbalimbali, kuvumbua, na kudadisi mazingira anayoishi kwa kushirikiana na wenzake.

 

Maswali ya kujiuliza

Inatupasa tujiulize maswali haya ya msingi juu ya utolewaji wa elimu ya awali nchini; - Je, ni kwa kiasi gani elimu ya awali nchini imekuwa ikitolewa kulingana na mtalaa wa elimu ya awali unavyoagiza? Je, mazingira yake yanamwezesha mtoto kukua kimwili, kiakili, kimaadili na kiroho?

Je, uanzishwaji wa madarasa ya elimu ya awali katika shule zetu za msingi unazingatia mahitaji muhimu ya mtalaa au tunafanya bora liende?

Rais John Magufuli alitoa wito kwa viongozi wa mikoa na wadau wa elimu kujitokeza kuchangia madawati ili kuondoa tatizo la wanafunzi kukaa chini

Binafsi naupongeza uamuzi wa Rais na Serikali yake kwa kuliona hili na kuliwekea msisitizo ili kuhakikisha upungufu wa madawati milioni 1.4 unatafutiwa mwarobaini wake.

Pia, nawapongeza zaidi wananchi na wadau wa elimu walioitikia wito wa Rais wa kuhakikisha kuwa kila mwanafunzi anakaa kwenye dawati ifikapo tarehe 30 Juni mwaka huu.

Hata hivyo, jambo la msingi la kujiuliza ni je, utengenezaji wa madawati haya ulizingatia umri na maumbile ya wanafunzi waliopo shuleni? Ni nani alipewa jukumu la kusimamia na kuhakikisha madawati yanayotengenezwa yanakuwa na vipimo na viwango vinavyostahili kwa mujibu wa mitalaa na miongozo?

Je, tulikumbuka kutengeneza madawati ya watoto takribani milioni moja wa elimu ya awali na watoto takribani milioni mbili wa darasa la kwanza? Au tulitengeneza madawati ili kuhakikisha tarehe 30 Juni madawati yanakuwepo shuleni?

Kwa shule nyingi ambazo zimepokea madawati kwa ajili ya kuwasaidia wanafunzi, hazina madawati maalumu kwa ajili ya watoto wa awali ambao wamelazimika kukalia madawati yaliyopatikana bila kujali umri wao.

Ni muhimu sasa tukazingatia mahitaji halisi ya wanafunzi na tukaijenga elimu yetu kwa kuhakikisha msingi wake unakuwa bora na imara.

Ikiwa utaratibu hautafuatwa katika kujenga msingi imara, nyumba itaanguka na inawezekana ikaanguka wakati ujenzi ukiendelea au miaka michache baada ya kukamilika.


Alinanuswe Kasyele ni Ofisa programu kutoka idara ya Habari na Utetezi HakiElimu. [email protected]