MBALAMWEZI YA KISWAHILI : Tunahitaji kuwa wazalendo katika Kiswahili

Tuesday November 14 2017

 

By Erasto Duwe

Uzalendo ni dhana inayofafanuliwa katika ‘Kamusi ya Kiswahili Sanifu’ kuwa ni hali ya mtu kuwa tayari kuifia nchi yake.

Katika makala haya uzalendo unachukuliwa kuwa ni hali ya mtu kuwa na mapenzi katika lugha ya Kiswahili na kuwa tayari kuitumia katika mazingira mbalimbali, hata yale ambayo isingekuwa rahisi kufanya hivyo.

Kutokana na ukweli kwamba Wakoloni walifanikiwa kutusadikisha kuwa kila kitu chetu ni cha kishenzi, jambo hilo limeendelea kutuathiri hadi leo hii. Athari hiyo imeiathiri jamii yetu kwa miongo kadhaa hadi sasa.

Tunu zetu bora za utamaduni kama vile mila, desturi, lugha kwa kuzitaja kwa uchache, zimekuwa zikionekana kuwa za kishenzi.

Kinyume chake jambo lolote linalohusiana na Wakoloni hao hata kama halina maana yoyote kwetu, limekuwa likitukuzwa na kupewa thamani ya pekee. Hiyo ni kasoro kubwa ambayo lazima tuikiri wazi.

Kwa upande wa lugha adhimu ya Kiswahili, kumekuwa na mitazamo kadhaa miongoni mwa wanajamii. Lipo kundi la wasomi linaloshadidia Kiswahili kuenziwa na kutumiwa katika nyanja mbalimbali muhimu katika jamii yetu.

Aidha, kuna kundi jingine la wasomi ambalo linaweka ukinzani mkubwa dhidi ya matumizi ya Kiswahili katika maeneo hayo mbalimbali muhimu. Mvutano wa makundi ya wasomi umekuwa na athari pia katika kuwaathiri Watanzania wengine ambao hawaingii katika makundi hayo tajwa ya wasomi.

Wapo wanaoamini kwamba Kiswahili hakina thamani kama zilivyo lugha za kigeni hususan Kiingereza.

Watu hao nao wamekuwa wakishadidia thamani na umuhimu wa lugha za kigeni kwa kukibeza Kiswahili hata kama lugha hizo za kigeni hawazijui huku wakitumia Kiswahili katika mawasiliano yao yote.

Aidha, lipo kundi linalokithamini Kiswahili kwa kuunga mkono kauli za wasomi wanaokishadidia Kiswahili. Hao wanatamani pia kuwa Kiswahili kipewe majukumu makubwa zaidi ikiwamo kutumika kufundishia katika nyanja zote za elimu.

Ikumbukwe kwamba ‘Kiswahili ni chetu, lugha za kigeni ni zao.’ Hata siku moja lugha hizo za kigeni hazitarejelewa kwamba asili yake ni Tanzania au Afrika Mashariki.

Dunia nzima inatambua kwamba, kitovu cha Kiswahili ni Tanzania ama Afrika Mashariki. Kwa hivyo, hilo ni jambo la kujivunia, na kwa sababu hiyo tunapaswa kukienzi Kiswahili, kukitoa kilipo na kukipeleka mbele zaidi ili kwamba ile dhana ‘sisi ni kitovu cha Kiswahili duniani’ idhihirike.

Hakuna lugha iliyo bora zaidi kushinda nyingine. Kila lugha ni bora kwa watumiaji wake kwa kuwa inawawezesha kukidhi mahitaji yao.

Wenye mtazamo kwamba Kiswahili kipo nyuma bado, wamekosa taarifa za sasa mintarafu nafasi na hadhi ya Kiswahili duniani.

Hata hivyo, kukiongelea vibaya kilicho chako badala ya kutafuta nafasi ya kukikwamua ni kukosa uzalendo na ni utumwa wa kimawazo.

Wakati baadhi yetu wakiwa na mawazo dufu dhidi ya Kiswahili, wageni kutoka mabara mbalimbali wanakisaka kwa udi na uvumba kutokana na umuhimu wake.

Viongozi wetu wa nchi wamekuwa mfano wa kuigwa katika hili. Rais wetu, John Magufuli ameonyesha uzalendo wa hali ya juu.

Tofauti na ilivyokuwa imezoeleka awali, sasa tunashuhudia Rais wetu akitumia Kiswahili mbele ya wageni wa kimataifa wasiokijua Kiswahili. Kufanya hivyo kuna mchango mkubwa katika maendeleo ya lugha yenyewe. Kiswahili kinazidi kupanda hadhi na kinazidi kutangazwa kote duniani. Uzalendo huu ndio unaohitajika.

Kila mmoja akiwa na mapenzi ya namna hii, Kiswahili kitazidi kutukuka. Tuige mfano wa uzalendo katika Kiswahili kutoka kwa Rais wetu, shime!

Advertisement