Tunasubiri kusikia uchaguzi wa viongozi ZFA

Muktasari:

  • Nilijiuliza maswali mengi kuhusiana na kilichoiondoa. Inaelezwa kuwa eti timu kuchezesha wachezaji 12 waliozidi miaka 17 katika mchezo na Sudan.

Nilipigwa ganzi kusikia Tanzania imepoteza nafasi ya timu za vijana wa U-17, michuano inayoendelea kule Bujumbura, Burundi.

Nilijiuliza maswali mengi kuhusiana na kilichoiondoa. Inaelezwa kuwa eti timu kuchezesha wachezaji 12 waliozidi miaka 17 katika mchezo na Sudan.

Hatua hiyo ilisababisha Baraza la Vyama vya Soka Afrika Mashariki na Kati, (Cecafa) kuiondoa Zanzibar katika michuano yake na kuisimamisha shughuli zote za Cecafa hadi hapo itakapolipa faini inayofikia Sh3.5mil.

Katika kikao chake kilichokuwa chini ya Mwenyekiti wake, Doris Petra ambaye ni Makamu wa Shirikisho la Soka Kenya, waliamua kwa pamoja kuiondoa Zanzibar.

Pia kurudisha gharama za tiketi na malazi zinazofikia Dola15,000 ambazo imetumia katika kipindi chote walichokuwa Burundi hadi walipotimuliwa.

Mbali na hilo, Ethiopia wametozwa faini ya Dola 5,000 kwa kuchezesha wachezaji watatu vijebakatika mechi waliyoilaza Somalia mabao 3-0.

Kanuni za mashindano hayo zinasema kuwa, wachezaji wanaoruhusiwa ni wale waliozaliwa mwaka 2002.

Naipongeza hatua iliyochukuliwa na Cecafa kuwaweka pembeni Zanzibar na wenzao wa Ethiopia kupigwa faini.

Uamuzi huo ni wa busara na ndio utakaokomesha vitendo vya kudanganya umri wa wachezaji.

Mashindano ya umri mbalimbali yanatayarishwa kwa sababu ya vijana wa umri unaohitajika.

Kuchezesha wachezaji wa umri mkubwa ni kuwanyima haki wale ambao wanastahili kushiriki katika mashindano hayo.

Siku zote njia ya mkato ina gharama zake.

Huwa ninakwazwa na huu uteuzi. Hivi makocha wanaoteua au kamati za ufundi, kweli hazifahamu inachokifanya? Ulimwengu huu wa Sayansi ni wapi utafanya fojari hata usionekane. Wachezaji wameshatolewa kategoria yao, wanatakiwa wa namna gani bado mtu anajipangia tu.

Pili, hata mchezaji mwenyewe, nashangaa anashindwa kujitambua. Hivi kama umri wako mkubwa, kidevu kimekomaa kwa kunyoa ndevu, utafananishwa na watoto wa shule za msingi.

Ukiangalia wachezaji wa Kenya wote ni sekondari na msingi sawa na Tanzania Bara.

Nimesema tunasubiri kusikia ikitangazwa tarehe ya uchaguzi wa Chama cha Soka Zanzibar (ZFA) baada ya viongozi wake kujiuzulu kwa kashfa ya umri wa Mapinduzi Stars.

Kashfa ya umri kwa wachezaiji 12 ni doa kubwa ambalo leo hii tungesikia Baraza la Michezo Zanzibar, BMTZ, linatangaza tarehe ya uchaguzi baada ya viongozi wa ZFA kuachia ngazi.

Kama wameshindwa kujiuzulu ambacho si utamaduni wetu, mbona hatuoni taarifa za waliohusika kuchukuliwa hatua?

Mbona hatuoni wala kusikia utetezi wa wachezaji hao kuwa walistahili na Cecafa imewaonea?

Mbona hatuelezwi kinagaubaga cha aibu hii iliyoikumba ZFA?

Mbona hatuambiwi muhusika au wahusika wakuu waliofanya uteuzi wa wachezaji ni nani na walikuwa wanalenga nini?

Waliohusika na suala hilo hawapaswi kuachwa vivi hivi kwani doa waliloitia Zanzibar halitafutika na vilevile wameitia hasara kwani wanatakiwa kurudisha gharama na kulipa faini.