JICHO LA MWALIMU: Tunavyoweza kuwajengea watoto umahiri wa lugha-2

Muktasari:

Njia hii imekuwa ikifanya vizuri kwa watoto wadogo wa madarasa ya awali mpaka darasa la pili, ambao hufundishwa katika shule zinazotumia mtalaa wa Kiingereza.

Katika makala ya wiki iliyopita niliishia kwa kuonyesha kuwa mtoto anaweza kujua lugha ya kigeni ikiwa wazazi wake wataamua kuitumia katika mazungumzo nyumbani. Endelea.

Watoto wataweza kumudu lugha ya kigeni kama lugha mama kwa sababu wanaitumia katika mazungumzo. Ikumbukwe uwezo wa kutambua lugha ni kwa kuizungumza zaidi kuliko kuiandika.

Katika mbinu hii, mzazi au mwalimu hutumia lugha lengwa tu na kuichukulia ndiyo lugha mama. Mbinu hii ya lugha hujikita katika kufanya mazungumzo kuliko kuandika.

Njia hii imekuwa ikifanya vizuri kwa watoto wadogo wa madarasa ya awali mpaka darasa la pili, ambao hufundishwa katika shule zinazotumia mtalaa wa Kiingereza.

Watoto hao huwa mahiri katika kuzungumza kiingereza kuliko kukiandika. Hii ni kutokana na kwamba kwa kipindi hicho, kuandika hakutiliwi umuhimu kuliko kuongea.

Athari za lugha mama

Ni jambo la kawaida kwa watu wengi waliojifunza lugha ya pili ukubwani kusumbuliwa na lafudhi au matamshi ya lugha mama wanapoongea lugha ya pili au ile ngeni.

Kwa mfano, watu kutoka jamii ya Wasukuma au Wachaga, wanaweza kujikuta wakitumia lugha ya kigeni kwa kutumia matamshi ya lugha zao za kikabila.

Pia, changamoto nyingine ni uwezo wa kusikia na kutofautisha matamshi ya baadhi ya maneno ya lugha ngeni na kuyatamka kwa ufasaha, hupungua mtu alipojifunza lugha ya kwanza.

Watu wanaojifunza lugha ya kwanza, ya pili na ya tatu wanapokuwa na umri mdogo huwa na uwezo mkubwa wa kuweza kutamka kwa ufasaha maneno ya lugha hizo zote. Hivyo, kujifunza lugha mbalimbali wakati wa utotoni, kuna faida kubwa ya kujenga umahiri wa lugha kuliko ukubwani.

Ni vizuri wasimamizi wa elimu wakaona umuhimu wa kufundisha lugha mbalimbali katika ngazi ya elimu ya msingi. Kama ambavyo imekuwa ikifanyika katika baadhi ya sekondari na ngazi za juu.

Wataalamu wa lugha kama Lamendella na Paradis, wanaeleza kuwa watoto wadogo wana uwezo mkubwa wa kujifunza lugha mpya kuliko watu wazima.

Lugha ya pili ya mtoto

Kama ambavyo imeelezwa hapo awali, watoto wengi huweza kujifunza lugha zaidi ya moja. Wengine huweza kujifunza zaidi ya lugha mbili.

Kwa mfano katika nchi ya Tanzania ambako kwa maeneo mengi lugha ya Kiswahili imetumika kama lugha ya kwanza. Pia, kuna baadhi ya sehemu lugha ya Kiswahili ni lugha ya pili baada ya lugha mama ya kikabila. 

Tafiti huonyesha kwamba watoto ambao wamejengewa misingi mizuri ya lugha; katika lugha yeyote ile huweza kujengeka vema kiakili na kuwa na uhusiano imara na wazazi au walezi wake.

Huwa na uwezo wa kufanya mawasiliano kwa kiwango kikubwa na huwa na maandalizi kwa ajili ya shule. Huweza kujifunza vizuri lugha ya pili au ngeni kama wataipata kutoka katika kaya au jamii wanayotoka kuliko darasani.

Utafiti uliofanywa na Chuo Kikuu cha Harvard kilichopo Marekani, umeonyesha kwamba ubunifu, uwezo wa kufikiri na kutafakuri na uwezo wa kuelewa mambo mbalimbali huongezeka endapo watoto watapatiwa fursa ya kujifunza lugha ya pili au ngeni wakiwa katika umri mdogo.

Sera ya elimu na mafunzo ya mwaka 2014 ambayo waandaaji wa mitalaa kwa shule za msingi wameizingatia, inahimiza kuwa ufundishwaji wa lugha moja uanze kabla ya kuongeza lugha ya pili. Mtaalaa huo ulioboreshwa umeeleza kuwa kwa shule za msingi zinazotumia lugha ya Kiswahili ziaanze kufundisha somo la lugha ya Kiingereza kuanzia darasa la tatu.

Vivyo hivyo kwa shule zinazotumia mtalaa wa Kiingereza, zitapaswa kuanza kufundisha Kiswahili kuanzia darasa la tatu. Hii ni ili kutoa fursa kwa wanafunzi wakiwa darasa la kwanza na la pili kujifunza vizuri lugha kwa umahiri.  

Watoto hujifunza lugha kwa kusikiliza

Mbinu ya usikilizaji huwasaidia watoto na mtu yeyote kujifunza lugha. Wazazi wanapowasaidia watoto katika njia hii ni vema wasifanye haraka.

Watoto hupaswa kufahamu kwanza maneno au misamiati mipya na kuyarudia kuyatamka mara nyingi katika vitendo tofauti tofauti. Kwa mfano, vitendo vya kuimba, kwa kuruka na kusema, kwa kusema na kupiga makofi na  kwa kusimulia

Wazazi au walezi wanaweza kutumia redio, CD au hata simu zao kwa kupakua katika intaneti na kuwasikilizisha watoto wao na kuwataka warudie maneno. Msisitizo uwe katika utamkaji wa maneno hayo.

Mbinu hii humjengea umahiri wa kuzungumza ana kwa ana. Baada ya kumudu kusikiliza hufuata kukariri mazungumzo; ndipo hufuata kusoma na kuandika. Pia, ucheshi huwafanya watoto wajifunze.

Motisha ya namna yoyote ni vizuri ikatolewa kwa mtoto anapoweza kutamka vizuri maneno tarajiwa. Motisha inaweza kuwa kupongezwa kwa kupigiwa makofi au kusifiwa kuwa amefanya vizuri; na wala siyo lazima iwe zawadi ya pipi.

Kujifunza kwa mwitikio wa vitendo

Mbinu ya mwitikio-kamili wa kivitendo hulenga zaidi utumiaji wa stadi moja ili hatimaye kuweza kuimarisha stadi nyingine. Mtoto humsikiliza na kumtazama mzazi au mwalimu akitamka amri na kuzitekeleza moja kwa moja.

Baada ya hapo mzazi au mwalimu hupaswa kurudia kila amri na kumtaka mtoto atekeleze baadaye.

Lugha ya ishara ni muhimu pia kwa sababu watoto wataangalia kwa umakini na kutambua lugha. Inasisitizwa kuwa katika kujifunza lugha ya pili, kutumike vitenzi vilivyo katika kauli ya amri kama ilivyo kwa watoto wadogo wanapojifunza lugha kwa kusema kama vile  mama taka mma! mama taka uji!

Kujifunza lugha kijumuiya

Mbinu hii ya ujifunzaji lugha kijumuiya hujulikana pia kama mbinu ya ujifunzaji kwa ushauri.

Katika mbinu hii mtoto huzingatiwa katika mbinu mbili, kwa upande mmoja hisia zake kama binadamu, hupewa nafasi ya kujieleza na kupewa ujuzi wa lugha kwa kiwango kinachotakiwa.