Tunaweza kuwawahi akina Poulsen

Muktasari:

Dove alikuwa ameguswa na kiwango cha mataifa mengi ya Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia kule Brazil. Inawezekana kabisa akawa na macho yenye mboni kali na ambayo yanatizama kesho katika soka letu.

Moja ya waandishi wachache ambao hawajawahi kukaa mbali na habari mchanganyiko kutoka Afrika hasa habari za michezo anayefahamika kama Ed Dove aliwahi kutoa ushauri kwa namna gani ambayo soka la Afrika linaweza kukua.

Dove alikuwa ameguswa na kiwango cha mataifa mengi ya Afrika kwenye fainali za Kombe la Dunia kule Brazil. Inawezekana kabisa akawa na macho yenye mboni kali na ambayo yanatizama kesho katika soka letu.

Kwenye makala yake mojawapo kati ya makala zake nyingi kuhusu soka letu alitoa sababu saba ambazo yeye alizipatia jina la mabadiliko ambayo aliamini kama yangefanyika basi soka la Afrika lingekuwa katika nafasi nzuri zaidi ya kufanya vyema kuliko ilivyoeleka ambako tunakuwa kichwa cha mwendawazimu alichotaja mzee wetu Ali Hassan Mwinyi siku moja.

Katika wino aliamua kumwaga juu ya mataifa yetu yote, alitaja sababu zake kuwa kuimarisha ubora wa ligi za ndani, kuachana na kukariri majina na badala yake kutazama uwezo wa wakati husika, kuongeza umoja wa wachezaji na kuepuka majina makubwa kutawala madogo kiuamuzi.

Suala la uwazi na kuaminiana kwenye ngazi ya uongozi, kutibu ugonjwa wa kifedha unaoibuka kabla ya mashindano, kutumia maarifa wakati wa kuchagua makocha na kubwa zaidi kushawishi wachezaji wa Afrika wenye uraia wa mataifa mengine kurudi na kucheza nyumbani kwenye asili yao.

Ni miaka mitatu sasa tangu Dove atoe ushauri huu na wakati mengine yakiwa yanaendelea kuibuka na kuja taratibu hili la kupata wachezaji wenye asili ya Afrika wanaoweza kutumikia mataifa yetu linaonekana kuwa rahisi zaidi.

Timu ya Taifa ya Zimbabwe ilipitisha sera ya kuhakikisha kuwa inamtambua kila raia wa Zimbabwe duniani kote mwenye kipaji ili arejee kuchezea taifa hilo.

Katika mpango huo haraka haraka shirikisho la soka nchini Zimbabwe liliwaita wachezaji Macauley Bonne anayechezea klabu ya Leyton Orient, Admiral Muskwe aliyepo katika kikosi cha Leicester City, kiungo wa Celtic, Kundai Benyu, na beki wa Nottingham Forest, Tendai Darikwa huku pia wakituma wawakilishi kumshawishi mchezaji anayekuja vyema kwenye kikosi cha Arsenal, kinda anayefahamika kama Reiss Nelson.

Kwenye akili ya Wazimbabwe wanauamini ukweli ambao hausemwi kwa kiwango kikubwa kuwa mataifa mengi makubwa ya Ulaya yamenufaika kwa kiasi kikubwa na vizazi vya Afrika kabisa na wamekuwa wakipiga hatua kila uchwao.

Hii ni kuanzia miguu ya Zinedine Zidane ambayo iliipa Ufaransa ubingwa wa dunia kisha Ulaya mpaka ikafika kwa Vieira mpaka leo Kante na Pogba wakiwa viungo bora zaidi wakitokea huku nyumbani.

Lakini hili lililowahi kutajwa na Ed Dove wala halikomi na kugota katika timu ya Taifa ya Ufaransa pekee ambayo pengine wengi wanaitizama zaidi bali mpaka kwa Ubelgiji. Kikosi cha leo cha Ubelgji ambacho kinaaminika kuwa na kizazi cha dhahabu zaidi kuwahi kutokea, kinaweza kuanzisha takaribani nusu ya wachezaji muhimu wa kikosi cha kwanza wanaozungumza Kilingala.

Wachezaji Vincent Kompany, Youri Tielemans, Michy Batshuayi, Romelu Lukaku, Christian Benteke mpaka kwa Jordan Lukaku wote wangeweza kuwa katika kikosi cha leo cha Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo na kufanya maajabu ambayo hakuna ambaye angeweza kutegemea.

Lakini ni taifa hili pia ambalo wachezaji kama Steven N’Zonzi, Steve Mandanda, Presnel Kimpembe na Eliaquim Mangala wangeweza kulichezea kwa furaha kuliko kusubiri kuitwa na Didier Deschamps katika kikosi cha Ufaransa ikiwa haijulikani kama itakuwa leo au kesho.

Wote hawa ni vijana na ambao wangeifanya Congo iwe timu tishio zaidi duniani kwa sasa, lakini nani anajali?

Ed Dove aliona mbali, alitizama ambako wengi walipapuuza na ndio maana ni heri kuona vijana wanaokosa nafasi England kama Alexander Iwobi, Wilfred Zaha wakikumbuka na kurejea nyumbani kuchezea mataifa ya asili yao.

Tatizo linaweza kuwa moja tu mpaka sasa ambalo pengine mwandishi Marieme Jamme akiwanukuu na waandishi wakongwe kama Chinua Achebe, Amadou Hampâté Ba na Ousmane Sembene alilisema kuwa Afrika haipati maendeleo kwa sababu hata walioko nje wanaamini kuwa wakija huku wanajifunza utamaduni pekee na hakuna Maendeleo yoyote bali kufahamu tunaishi vipi katika mazingira haya.

Ndio sababu kubwa ambayo hata hawa wachezaji vijana wanaogopa kurejea huku kwa sababu kuna maisha wanayoyasoma kwenye majarida na vitabu kuwa Afrika haijaendelea na bahati mbaya zaidi wakitizama vyema wanakuta andiko ambalo linaonyesha namna gani timu ya Taifa ya Cameroon ilivyogoma kusafiri kwa sababu ya posho.

Huwezi kumshawishi Lukaku kurejea kuchezea Jamhuri Ya Kidemokrasia Ya Congo kirahisi wakati anafahamu kuwa timu ya Taifa ya Togo waliwahi kutekwa kwenye moja ya misitu maeneo hayo.

Mchezaji wa klabu ya RasenBallsport Leipzig inayofahamika kwa jina maarufu kama RB Leizpig bwana Mtanga huyu Yussuf Poulsen, alizaliwa kwa baba Mtanzania na mama raia wa Denmark, moja ya wachezaji vijana wanaokuja vyema kwenye ligi ya Ujerumani ya Bundesliga.

Alikuwepo Tanzania miezi kadhaa nyuma kabla ya msimu wa 2017/2018 kuanza, lakini hata angepatikana akiwa kijana ungemshawishi vipi aukane uraia wa Denmark ili achukue wa Tanzania kwa sababu haturuhusu uraia pacha.

Miaka inasogea na vijana wanaendelea kuingia kwenye miji ya watu, akina Yussuf wapo wengi duniani huko, lakini hawafahamu wanarejea vipi Tanzania na sera haziwaruhusu “kula bata” Dar Es Salaam na Paris kwa wakati mmoja yaani kuwa na uraia wa zaidi ya nchi moja.

Inawezekana shirikisho la soka Tanzania linafahamu kuhusu sera hii, inawezekana linajaribu kufuatilia lakini hawa wachezaji wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo wamenitia tamaa.

Jirani zangu hawa wamesababisha mate yamenitoka mdomoni kwa sababu wachezaji wote niliowataja wana wastani wa umri usiozidi miaka 26 na wananufaisha mataifa mengine huku wao wakiondolewa na Tunisia.

Sitegemei na Tanzania siku moja tujikute huku, Ed Dove alisema miaka mitatu nyuma, wapo walioanza kujifunza kama Zimbabwe nasi tuwatafute akina Yussuf. Naamini wapo na tunaweza kuwawahi huko kwenye “academy”.