UCHAMBUZI: Tusione fahari kuchangia msiba kuliko matibabu

Muktasari:

Hatukupata msaada unaotosha kununua dawa kwa wakati. Tulizungumza na uongozi wa hospitali ili angalau tupate dawa kwa ahadi ya kulipa baadaye lakini tuligonga mwamba.

Hivi karibuni nilifiwa na mdogo wangu kutokana na saratani. Alikuwa ni kijana wa miaka 22 tu. Alizaliwa 1994. Kwenye kipindi chote cha kuugua kwake tulikuwa tukipiga simu kwa ndugu na jamaa ili kupata michango yao kwa ajili ya matibabu yake lakini mwitikio haukuwa wa kutosha.

Hatukupata msaada unaotosha kununua dawa kwa wakati. Tulizungumza na uongozi wa hospitali ili angalau tupate dawa kwa ahadi ya kulipa baadaye lakini tuligonga mwamba.

Alipoanza tiba ya saratani aina ya ‘chemo’ madaktari walitwambia atatakiwa kutumia kwa awamu sita. Dawa zinazochanganywa kwa tiba hii hugharimu zaidi ya Sh500,000 kwa awamu moja.

Tulifanikiwa kupata ‘chemo’ ya kwanza, lakini kutokana na ukata, ilituchukua muda mrefu kupata fedha za dawa na hatimaye alifariki dunia. Cha ajabu, siku ya msiba ndugu na jamaa walichanga fedha nyingi. Nakumbuka hazikuwa chini ya shilingi milioni tatu ndani ya siku mbili tu.

Nilijiuliza maswali kadha wa kadha nikiwaangalia wanavyotoa michango yao kwa kushindana. Nilizungumza na moyo wangu, walikuwa wapi watu hawa wakati mdogo wetu anaugua? Mbona tuliomba sana fedha, lakini hawakujitokeza? Pengine wangefanya hivi kipindi hicho angeishi.

Ni tabia ya Watanzania wengi kuchanga fedha kwenye msiba lakini hawajitokezi mtu anapougua. Wanaonyesha ufahari kwa magari, ofa ya viti, maturubai, fedha hata bia kwenye msiba lakini si wakati wa kuuguza.

Nilishangaa kuona sare zilivaliwa kwa wingi. Muuza fulana alikuja na aliziuza kati ya Sh10,000 na 15, 000 na akamaliza mzigo wote. Mwenye madela naye alipofika pale msibani, akinamama waliyagombea kwa Sh15,000 kila moja.

Kila mtu akawa anataka kuonyesha upendo kwa marehemu ambaye kwa wakati huo haoni, hasikii, wala hataweza kushukuru. Nikajiuliza tena haya yote ni fahari ya msiba au ya marehemu?

Hata wale ambao hawakuwahi kutoa walau Sh200 ya machungwa ya mgonjwa, siku hiyo walinunua madela na tisheti. N.

Zamani waombolezaji walijikunyata kwa uchungu, wakavaa kanga zao na baadhi ya mila hazikuruhusu kuoga na kuvaa viatu mpaka matanga yanapovunjwa. Leo hii hayo hayapo.

Pengine madela, tisheti na maua ni maendeleo, lakini tabia ya kuacha kujitoa wakati wa ugonjwa na kuonyesha ufahari msibani sidhani kama inajenga zaidi ya kubomoa.

Naunga mkono kuchanga fedha msibani kwa ajili ya chakula kwa waombolezaji, viti na inapendeza kumhifadhi mpendwa wetu kwa staha ili kuonyesha kumthamini.

Hata hivyo jamii haina budi kubadilika. Tujenge utamaduni wa kujitoa na kuhamasishana kuchangia pindi yanapotokea mahitaji ya kielimu, magonjwa au maafa kama tetemeko na mafuriko.

Kwa mfano katika suala la magonjwa, familia iwe na mfumo wa kuitisha vikao na wanafamilia wachangie kiasi ambacho kitatumika kwa matibabu.

Kwa mtindo huu, zitapatikana fedha za kumsaidia mgonjwa kwa chakula, nauli za kwenda hospitali na dawa. Kila mtu aguswe kumhudumia mgonjwa ili kuokoa maisha yake na asisubiri kifo aje aonyeshe mbwembwe zake kwa marehemu asiyeona chochote afanyacho.

Mtandao wa GiveForwad.com, unatoa mbinu za kupata fedha pindi familia inapokuwa na mgonjwa.

Kama ambavyo watu huanzisha vikundi vya Whattsup kwa ajili ya kuchangisha fedha za harusi au shughuli nyingine yoyote kadhalika makundi hayo yatumike kuongeza kipato kwa ajili ya matibabu.

Upendo wetu utapimwa iwapo tutamtendea mema aliye hai na kushuhudia tunachomfanyia. Wala si kuonyesha huzuni siku ya msiba kifahari ya kusukuma jeneza.

Tuwasiliane: 0764 438 084