UCHAMBUZI: Tusipokuwa makini utandawazi utaharibu vizazi vyetu

Muktasari:

Miaka ya karibuni tumeshuhudia ongezeko la matumizi ya simu za mkononi, mitandao ya kijamiii na hata teknolojia ya habari na mawasiliano.

Maendeleo ya teknolojia yanapigiwa kelele kila mara. Kwenye habari tumeshuhudia wadau wanavyohamasisha uharakishwaji wa maendeleo hayo.

Miaka ya karibuni tumeshuhudia ongezeko la matumizi ya simu za mkononi, mitandao ya kijamiii na hata teknolojia ya habari na mawasiliano.

Ni jambo jema kwani sasa hakuna haja ya kusafiri umbali mrefu kupeleka habari ya msiba. Au hakuna haja ya kuwa na shaka tena katika kutuma pesa kutoka kwa mtu mmoja kwenda kwa mwingine. Badala yake unaweza kutumia simu yako ya mkononi, ukafanya malipo ya aina yoyote unayohitaji.

Siyo hivyo tu, hali hii imeenda mbele zaidi kwani hivi sasa unapohitaji kusafiri kwa kutumia ndege unaweza kununua tiketi ukiwa nyumbani kwako, hili pia ni jambo la kupongeza.

Kwa kifupi naweza kusema ile dhamira ya kuifanya dunia kuwa kijiji imetimia.

Tafsiri ya yote haya kwangu ni maendeleo. Siwezi kubisha kuwa hatujasogea.Tumepiga hatua kutoka pale tulipokuwa kwenye matumizi ya analogi na sasa tupo katika digitali. Tumeingia kwenye digitali sina hakika sana kama ilikuwa ni hiyari yetu ama utandawazi umetusukuma.

Kwa sababu kinachoonekana kwa sasa ni kwamba wenzetu wameingia huko wakiwa wamejiandaa, kuliko sisi tulio ulimwengu wa tatu.

Kwa upande wa watoto wetu, wao ni kizazi cha digitali. Hali hii imeathiri hata mtindo wa maisha yao.

Hakuna tena watoto wenye muda wa kushiriki michezo ya asili kama vile rede, tayari bado, kidali au kombolela. Watoto wamekuwa na tabia za kimagharibi hawana tena uafrika, ama kwa kutojua au kuona ni ushamba tu.

Shuleni hali imezidi kuwa mbaya ile kawaida ya kukimbia mchakamchaka kila asubuhi kupasha moto viungo sasa haipo. Katika sherehe zao wanaimba Bongo Fleva. Hii maana yake ni kuwa kifo cha ngonjera na kwaya ndiyo kimewadia.

Watoto wanataka kuishi kizungu. Utamaduni wetu wameuzika, wanaporudi nyumbani wanakutana na mzazi wao mpya ambaye ni televisheni.

Muda mwingi wanajihusisha na utamaduni wa magharibi, kuanzia mitindo ya mavazi, nywele na hata namna ya kuzungumza.

Wazazi siku hizi wameacha majukumu yao ya msingi ya kulea watoto na badala yake jukumu hilo limeachwa kwa wasichana wa kazi na walimu shuleni.

Kutokana na malezi duni ya watoto, mara nyingi wanapotoka shule na kurudi nyumbani kazi yao kubwa ni kuangalia televisheni.

Wale wa shule ya msingi mara nyingi hupendelea kuangalia vipindi vya katuni, lakini walio shule za sekondari wao hupendelea kuangalia vipindi vya muziki au filamu za tamthilia.

Sina tatizo na wao kuangalia vipindi vya televisheni. Tatizo langu ni moja tu hapa, kwamba ni nani anawasimamia wakati wakiangalia vipindi hivyo.

Ikumbukwe kuna tofauti kubwa kati ya utamaduni wa magharibi na ule wa nchi za Afrika. Utamaduni wa magharibi haukatazi baba kuoga kwenye bwawa na mtoto wake wa kike, kwa utamaduni wa Afrika kitendo hicho ni uchuro.

Yapo mengi yanafanyika ambayo ni kinyume na maadili yetu, lakini watoto wetu huyaangalia tena kwa uhuru.

Watoto wanajifunza vitu vya ovyo kupitia televisheni. Haya yote yamekuwa yakitokea wakati sisi wazazi wao tukiwa kwenye ‘mwendo kasi’ wa kutafuta maisha.

Hivi karibuni ilisambazwa taarifa ya kusikitisha sana ikitoa tahadhari kuwa kuna katuni imetengenezwa makusudi kuhamasisha ushoga. Ikiwa taarifa hii ina ukweli, basi tumekwisha.

Wito kwa wazazi ni kuwa makini kwa watoto hasa wanapoangalia vipindi vya televisheni.

Hoja yangu naiomba mamlaka husika kufuatilia kila kinachoonyeshwa kwenye televisheni, ili kuwakinga watoto na vishawishi vibaya.