Tutafakari deni tuliloachiwa na wanajeshi wetu waliouawa DRC

Muktasari:

  • Katika kongamano hilo, Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama, alitoa hotuba ya kujengea mkazo maudhui (keynote adress), ya kwa nini Kerry ateuliwe kuwa mgombea urais wa Democrats kisha awe Rais wa Marekani.

Kongamano la Kitaifa la chama cha Democrats (DNC) mwaka 2004, liliketi kuanzia Julai 26 mpaka 29. Madhumuni yake yalikuwa kupitisha jina la John Kerry kuwa mgombea urais kwenye Uchaguzi Mkuu Marekani mwaka 2004.

Katika kongamano hilo, Rais wa 44 wa Marekani, Barack Obama, alitoa hotuba ya kujengea mkazo maudhui (keynote adress), ya kwa nini Kerry ateuliwe kuwa mgombea urais wa Democrats kisha awe Rais wa Marekani.

Ni hotuba hiyo ambayo ilimpa thamani kubwa Obama kuelekea kuchaguliwa kuwa Rais wa Marekani katika Uchaguzi Mkuu 2008. Hotuba hiyo imepewa jina la Hotuba iliyomtengeneza Obama kuwa Rais (The Speech that Made Obama President).

Pamoja na mambo mengi ambayo Obama aliyazungumza kwa ustadi mkubwa mpaka kuvutia watu kumuona anafaa kuwa Rais wa Marekani, sehemu ambayo nimechagua ili kuileta hapa tuitafakari kwa pamoja ni ile ambayo alizungumzia askari wa Marekani waliokuwa wakifia vitani Afghanistan na Iraq.

Obama alisema: “Tunapotuma vijana wetu wa kike na kiume kwenye njia inayodhuru, tunao wajibu mkunjufu siyo wa kudanganya namba au kuficha ukweli kwa nini vijana wetu wanakwenda vitani, bali kuzijali familia zao wanapokufa.

“Tuwatendee inavyostahili askari wetu mpaka wanaporejea, na kamwe tusiende vitani kama hatuna vikosi vya kutosheleza kushinda vita, kuokoa na kutunza amani kisha kutwaa heshima ya ulimwengu.”

Bila shaka Obama anatambua deni ambalo Taifa linakuwa linadaiwa na askari wanaoingia vitani au kwenda kutunza amani kwenye mataifa ambayo yanakuwa hayana utulivu. Ndiyo sababu ya kueleza ulazima wa familia za askari kutunzwa.

Rejea sehemu ambayo Obama alizungumzia “kutwaa heshima ya ulimwengu”, hivyo ndivyo ilivyo. Majeshi yanapoingia vitani na kushinda au yanapokwenda nchi mbalimbali kutuliza machafuko na kulinda amani, mafanikio ni kwa nchi. Hiyo ndiyo tafsiri ya Obama.

Tanzania imekuwa ikisifiwa sana na Umoja wa Afrika (AU), vilevile Umoja wa Mataifa (UN), kwamba hutoa askari mahiri kwenda kutunza amani kwenye nchi mbalimbali kadiri wanapohitajika na kutimiza malengo kwa mafanikio. Pongezi hizo zina thamani na heshima kubwa kwa nchi mbele ya uso wa kimataifa.

Inapaswa ifahamike kuwa nyuma ya sifa na pongezi hizo kwa nchi, kuna gharama kubwa ambayo askari wa Kitanzania wanakuwa wameibeba. Gharama hiyo ni kubwa kuliko nyingine yeyote ambayo binadamu anaweza kuingia kwa ajili ya kuipigania nchi yake. Gharama inayohusu uhai binafsi.

Ni hapo pa kujiuliza, kipindi ambacho askari wa Kitanzania wanaingia gharama ya uhai wao kwa ajili ya kuitetea nchi yao, je, nchi inatenda nini kulipa deni hilo kubwa ambalo halipimiki kwa mizani ya kawaida? Kipi cha zaidi ambacho kinafanyika kwa ajili yao?

Tathmini kuhusu namna mwanajeshi anavyostahili zaidi kama mtumishi wa umma, inapaswa kuanzia pale kwenye dhamira yake ya kutumika kama askari na moyo wa kujitoa kwa ajili ya Taifa lake. Anapopokea mafunzo yenye maumivu makali kisha kula kiapo cha kuifia nchi yake.

Kiapo ambacho humfanya awe mbali na familia yake kipindi ambacho wengine wanakuwa wanastarehe na ndugu, wake, waume, wazazi au watoto wao. Unapokuwa nyumbani umelala huna wasiwasi wa kumaliza usiku salama, ukiketi sebuleni unatazama runinga kwa utulivu, unapaswa kutambua kuwa kuna ambao hawalali ili kukulinda.

Tathmini ya kwamba askari wanastahili zaidi, lazima ianzie kwenye uchaguzi wa kazi. Si kila mtu anaweza kwa ridhaa yake kuchagua kuwa mwanajeshi. Jeshi ni kazi ambayo inahitaji zaidi wito na utashi wa mtu. Hao ambao wanajisikia kuitwa ili kuhakikisha nchi yao inakuwa salama, bila shaka wanastahili zaidi.

Deni la Taifa

Baada ya kukubaliana kuwa askari ambao wanajitolea kuihudumia nchi wanastahili zaidi, sasa vema kukumbushana deni la Taifa katika kuwahudumia askari wanaoishi, lakini kwa mkazo zaidi ni kuzijali na kuzihudumia familia za askari ambao wanakuwa wamefikwa na mauti katika misheni za kuipigania nchi au kulinda amani.

Mathalan, Desemba 8, mwaka huu, iliripotiwa kuwa wanajeshi 14 wa Kitanzania waliokuwepo Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC) kwenye misheni ya kulinda amani, waliuawa na waasi, wengine 44 walijeruhiwa, wakati wawili wamepotea. Hili tayari ni deni la Taifa.

Kifo cha askari mmoja ni hasara kubwa kwa Taifa kwa sababu Serikali hupanga bajeti na kuwekeza fedha ili kumhudumia kila mmoja wao. Hivyo, vifo vya wanajeshi 14 ni msiba mkubwa kwa nchi. Ukienda ndani ya familia zao kuna pigo kubwa. Wanajeshi hao walitegemewa kama walezi.

Ukifika hapo ndipo unatakiwa kuyakumbuka maneno ya Obama, kwamba wajibu mkunjufu siyo kuficha ukweli kama askari wamekufa au kudanganya idadi ya vifo, bali kuzijali familia zao.

Wengine wapewe sababu

Hakuna fidia ya uhai wa mtu, wala halipo lolote jema ambalo linaweza kufanyika kuziba pengo la mtu aliyeuawa vitani. Hata hivyo, kuzijali familia za marehemu na kuwapa thamani stahiki wazalendo waliofikwa na mauti wakiipigania nchi, hutoa sababu kwa waliobaki kuendelea kuwa wazalendo kwa ajili ya nchi yao.

Msingi wa kuhudumia familia za marehemu inavyotakiwa ni kuonyesha shukurani kwa askari ambaye alichagua kuingia gharama ya uhai wake ili kuilinda nchi yake dhidi ya uvamizi au kuitenga familia yake na kwenda kuishi msituni kwa ajili ya misheni ya kutunza amani, hivyo kulipa heshima kubwa Taifa lake.

Hiyo ndiyo njia mahsusi ya kuwatia moto na kuwajaza molari askari wengine waliopo kwenye vikosi ili waendelee kuwa na mioyo mikubwa katika kulitetea Taifa lao. Wajione ni watu wenye kupewa thamani maalum kulingana na kujitoa kwao. Hivyo ndivyo kuwafanya wanajeshi wajivunie kazi yao waliyoilia kiapo.

Desemba 9, mwaka huu, Tanganyika ilisherehekea miaka 56 ya uhuru wake. Bila jeshi imara uhuru si lolote. Zipo nchi na wapo watu wanatamani siku moja kuivamia Tanzania lakini wanashindwa kujaribu kwa sababu ya uwepo wa jeshi imara. Jinsi Idd Amin alivyodhibitiwa ni kielelezo tosha cha uhitaji wa wanajeshi makini na wazalendo.

Tuwaombee pumziko jema wanajeshi wetu waliopoteza maisha DRC. Inauma kuona waliingia gharama ya uhai binafsi kwa sababu ya watu wenye kung’ang’ania madaraka, huku upande wa pili ukuamini bunduki ni ufumbuzi wa kisiasa.

Inauma kuwapoteza wapigaji waliotaka kuifanya Afrika na dunia kuwa mahali salama pa kuishi. Msisitizo ni kuwaenzi kwa kuonyesha shukurani kwao, si kwa kujenga mnara wa kumbukumbu ya mashujaa peke yake, bali kuzikumbatia familia zao kwa hali na mali siku zote.