Tutafakari kama Mkurabita bado unahitajika Tanzania

Muktasari:

  • Rasilimali za wanyonge zinazotajwa katika mpango huu ni pamoja na ardhi, nyumba na majengo ya aina nyingine. Aidha, vitu kama baiskeli, redio na gari zinatajwa kama rasilimali wanazoweza kutumia wanyonge kuweka dhamana na kupatiwa mikopo katika taasisi za fedha endapo zitakuwa zimeongezewa thamani na utambuzi zaidi.

Mkurabita ni mpango wa kurasimisha rasilimali za wanyonge kwa lengo la kuhakikisha wanazitumia kuukimbia umasikini. Mpango huu unaelekea kutimiza miaka 14 ya uwepo wake huku lengo kuu la uanzishwaji wake likionekana kusuasua kutimia.

Rasilimali za wanyonge zinazotajwa katika mpango huu ni pamoja na ardhi, nyumba na majengo ya aina nyingine. Aidha, vitu kama baiskeli, redio na gari zinatajwa kama rasilimali wanazoweza kutumia wanyonge kuweka dhamana na kupatiwa mikopo katika taasisi za fedha endapo zitakuwa zimeongezewa thamani na utambuzi zaidi.

Toleo la mwaka 2007 la Mkurabita lililoitwa utajiri wa watu masikini (Poor People’s wealth) linaeleza wazi kuwa mpango huu ni mgumu (complex) hauleweki (unclear) utatekelezwa vipi kutoka na majukumu yake kuingilia kwa kiasi kikubwa na baadhi ya majukumu yanayotekelezwa katika Wizara, Idara, taasisi na Wakala wa Serikali.

Mkurabita ina umuhimu mkubwa sana katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania kwa kuwa kasi ya ukuaji wa sekta isiyo rasmi ni kubwa zaidi ukilinganisha na ukuaji wa sekta rasmi.

Takwimu zinaonyesha kuwa hadi kufikia mwaka 2009 sekta isiyo rasmi ilikuwa imeajiri zaidi ya watu 1.8 bilioni duniani kote sawa na asilimia 32.14 ya nguvu kazi iliyopo. Hii ni kwa wale ambao hawajihusishi na shughuli za kilimo. Idadi ya watu waliojiajiri kwenye sekta isiyo rasmi inatofautiana kati ya nchi na nchi kutokana na sababu mbalimbali.

Kwa Tanzania zaidi ya asilimia 90 ya nguvu kazi imejiajiri au kuajiriwa katika sekta isiyo rasmi ambapo hujipatia kipato cha kuendesha maisha yao ya kila siku. Kwa takwimu za mwaka 2010 zinaoenesha kuwa Tanzania inapoteza kati ya asilimia 35 mpaka 55 ya mapato yake ya ndani kwenye sekta isiyo rasmi.

Kwa tafsiri ya kawaida ni kuwa wakati serikali inatangaza makusanyo ya ndani kwa wastani wa Shilingi trilioni moja kwa mwezi, wakati huo huo inakuwa imepoteza kati ya Sh350 bilioni mpaka Sh550 bilioni kwa mwezi kutokana na kushindwa kukusanya kodi katika sekta isiyo rasmi.

Takwimu za mwaka 2013 zinaonesha Tanzania ina wastani wa biashara ndogo ndogo milioni tatu ila zilizosajiliwa na zinazotambulika kisheria ni 48,998 kwa mujibu wa sensa ya viwanda mwaka 2014. Hii ni sawa na asilimia 1.63 tu ya biashara hizo zilizopo. Hivyo zaidi ya asilimia 98 ya biashara ndogo hazitambuliki kisheria nchini.

Serikali ya awamu ya tatu chini ya Rais Benjamin Mkapa kwa kuona umuhimu wa sekta isiyo rasmi inakuwa kwa kasi na kuajiri nguvu kazi kubwa, wakati huo umasikini wa kipato kwa kaya unaonekana kuongezeka ikaona ni vyema ianzishe programu maalumu ya kutambua na kurasimisha rasilimali za wananchi wanyonge na masikini.

Kupitia urasimishaji huo, Serikali iliamini biashara za wanyonge zitakua, kwa maana wataweza kukopesheka hivyo kuongeza wigo wa ukuaji. Pili utaongeza kipato katika kaya na tatu utapunguza umasikini katika kaya za walengwa.

Kupitia rasilimali za mnyonge zilizoongezwa thamani ni rahisi kukopesheka na kujikwamua na umasikini wa kipato hivyo kuimarisha uchumi na Pato la Taifa (GDP) pia.

Wakulima pekee ni zaidi ya asilimia 66 ya Watanzania wote kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2012. Wengi wao wanamiliki mashamba ambayo hayajaendelezwa kwa maana ya kurasimishwa na kupewa hatimiliki.

Moja ya kazi kubwa iliyofanywa na Mkurabita miaka kadhaa nyuma ni pamoja na kurasimisha mashamba ya wananchi na kuwapatia hatimiliki za kimila katika wilaya za Bariadi, Babati, Mbozi, Bunda, Njombe, Iringa, Kilosa na Mvomero.

Ni kazi nzuri sana, ila ingeweza kufanywa na idara ya ardhi katika halmashauri husika kwa kuongezewa ‘nguvu’ na wizara yenye dhamana.

Kuna sababu za Mkurabita uondolewe. Mosi, mpango wenyewe kupitia maandiko yake inakiri kuwapo ugumu usio eleweka wa majukumu yake. Pili, uwepo wa majukumu yanayofanana kwa kiasi kikubwa kati ya Mkurabita na taasisi nyingine za Serikali.

Hili lipo maeneo mengi. Taasisi za usimamizi na udhibiti wa masuala ya biashara na uwekezaji yanakabiliwa na changamoto hii pia. Wafanyabiashara wamekuwa wakilalamika juu ya suala hili na kupendekeza kuhuishwa kwa majukumu yao ili kuokoa muda na gharama kw amuda mrefu.

Hivyo, kwa maoni yangu, naishauri Serikali kuivunja Mkurabita na majukumu yake kutekelezwa kwa mifumo ya kawaida ya Serikali.

Kwakuwa lengo la Serikali ni kuhakikisha wananchi wake wanaishi maisha mazuri na yenye gharama nafuu, si busara kuwa na wiraza, idara au taasisi nyingi za umma ambazo kimsingi zina majukumu yanayofanana kutimiza shabaha ya aina moja.

Zipo program nyingine ambazo utekelezaji wake unafanana na Mkurabita. Mpango wa Kukuza Uchumi na Kupunguza Umaskini (Mkukuta) au Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf) ni mfano mdogo.

Mwandishi ni mtakwimu na ofisa mipango wa halmashauri.