Tutawalaumu tu Msuva, Ajib hawafungi mabao T. Stars

Muktasari:

Ilikuwa ngumu kumpata kiongozi ambaye hakupita Kivukoni. Kila mmoja alikuwa na nidhamu. Tanuru la Kivukoni liliivisha viongozi wa Tanzania. Kila aliyetoka Kivukoni alisimamia misingi ya haki na uadilifu, kama waliokiuka walikuwa wachache tu.

Mwalimu Nyerere wakati anatengeneza viongozi, ilikuwa lazima wapitie Chuo cha Maendeleo ya Uongozi, IDM Mzumbe na wakati mwingine walikuwa wakipitia Chuo cha Chama Kivukoni. Huko watu walikuwa wakipikwa, walifundishwa maadili, misingi na taratibu za uongozi wa umma.

Ilikuwa ngumu kumpata kiongozi ambaye hakupita Kivukoni. Kila mmoja alikuwa na nidhamu. Tanuru la Kivukoni liliivisha viongozi wa Tanzania. Kila aliyetoka Kivukoni alisimamia misingi ya haki na uadilifu, kama waliokiuka walikuwa wachache tu.

Viongozi wengi walisimamia kwenye misingi na wengine hadi wanastaafu. Tofauti na sasa, unaambiwa kuwa ni kizazi cha dotcom, mabadiliko ya sayansi na teknolojia. Tunakwenda hivyo hivyo.

Nimeyafikiria hayo naona yanafanana na soka yetu na wachezaji wetu. Wachezaji tulionao, wengi wao hawakupitia kwenye tanuru la kupikwa wakaiva. Hatuwezi kuwa na wachezaji wazuri ambao hawakupikwa, haiwezi kutokea hata wawe wazuri.

Wakitokea wana namna hiyo, basi tutatumia nguvu nyingi kupata mafanikio. Kwa mfano, watu wana vipawa vya uongozi, lakini hawana maadili ya uongozi, hawana misingi ya uongozi kwa hiyo wanashindwa kusimamia misingi taratibu za kiutawala.

Hiyo ni sawasawa na vijana wetu, kwamba hawakwenda katika akademi za soka, sasa hawana mbinu, hawana misingi ya soka, hawana mwelekeo na watumia nguvu kupata mafanikio.

Nimejaribu kuangalia hali ilivyo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars, huwa ninajiuliza, kwanini Stars haina mafanikio? Kwanini haifanyi vizuri mashindano ya kimataifa?

Kingine, wachezaji wanakosa misingi, halafu ukiangalia, tuna kocha mmoja wa timu ya taifa, hiyo haipo duniani. Siku hizi mafanikio hayaji kwa kocha mmoja kuanzia ngazi ya klabu hadi timu ya taifa. Huwezi kuwa na kocha mmoja katika klabu au timu ya taifa.

Kwa mfano, ukiangalia Misri, na klabu zake wana makocha wa taifa karibu sita, Mayanga angekuwa kama overall kwa mfano.

Timu ya taifa inatakiwa kuwa na kocha wa makipa ambaye ninafahamu yupo, inatakiwa kocha wa mabeki huyu atashugulika na ngome yote. Beki gani akipanda nani anashuka, nani afanye nini kwa wakati gani.

Katika viungo; kiungo cha juu na cha chini. Wakati gani wapande, wakati gani washushe mipira, ikitokea wamepaki basi wafanyeje, njia ni zipi, wanaunganika vipi na washambuliaji, hilo ndilo kubwa, nao kocha wake.

Kunakuwa na kocha wa washambuliaji. Wanafungaje, wanapigaje mipira katika maeneo yapi, faulo za dead-balls zipigweje, huo ni mfano tu. Kunakuwa na yule wa mazoezi ya viungo, halafu kunakuwa na kocha wa kuungaisha timu kama Mayanga sasa.

Kwa kuangalia soka ya Tanzania kwanza hakuna muunganiko wa kusema, mchezaji ataanzia kwenye shule za soka, atacheza kila hatua ya mashindano ya umri hadi kufikia ukubwani kuchezea timu ya wakubwa. Hakuna.

Wachezaji hawana misingi ya soka, hatuwezi. Wewe angalia wenzetu, makocha wa kutosha, sisi wa makipa tu.

Ukweli ukiangalia kwa umakini, hatuwezi kufika mbali kwa staili hii. Inatakiwa kubadilika ili kuleta tija, lakini kwa kuwa tumezoea hivi, twendeni tu inawezekana Mungu akatuona siku moja.