KUTOKA MEZA YA MHARIRI WA JAMII: Tuzo za waandishi, walio nje wahusishwe

Muktasari:

Baraza la Habari Tanzania (MCT) linatunuku waandishi wa habari waliong’ara katika uandishi bora wa habari nchini kwa mwaka 2016.

Kesho ndiyo siku ya utoaji Tuzo za Uandishi Bora wa Habari Tanzania (EJAT) zitakazofanyika katika ukumbi wa Blue Pearl, Ubungo jijini Dar es Salaam.

Baraza la Habari Tanzania (MCT) linatunuku waandishi wa habari waliong’ara katika uandishi bora wa habari nchini kwa mwaka 2016.

Ni hivi: wanaotunukiwa ni wale ambao walishindanisha kazi zao ama zilizochapishwa magazetini, kutangazwa redioni au kwenye televisheni.

Wengine wanaotunukiwa ni washindi katika kupiga picha za mnato na za televisheni; na wachora katuni au vibonzo.

Kitu kimoja muhimu hapa ni kwamba, wanaotunukiwa ni wale ambao waliingiza kazi zao katika mashindano.

Inawezekana kuna kazi zinazolingana au hata kupita ambazo zinatunukiwa kesho; lakini hazikuingizwa katika mashindano. Hizo zinaweza kuwa “bora” tu miongoni mwa zile ambazo hazikufika MCT.

Hilo halijadiliwi hapa bali linaibua mjadala tofauti. Ni kesho au wakati kama huo baadhi ya waandishi wanajiuliza kwanini hawakuingiza kazi zao katika mashindano.

Hawasikitiki wala kujilaumu kwa kuwa hawatapata au hawakupata zawadi. Hapana. Wanasikitika kwa kutotajwa. Kutajwa tu. Kuwa miongoni mwa waliotambuliwa “kufanya vizuri.”

Wanasononeka kwa kutokuwa sehemu ya kusanyiko la jioni moja la waandishi wa habari, wanahabari, wanataaluma mbalimbali; linalosikia majina yao yakitajwa kuwa ni miongoni mwa waandishi bora wa mwaka jana! Wanasononeka kwa kutokuwa sababu ya kuwa na Siku na Usiku Maalum ili kwenye kusanyiko hilo wang’are kwa kutajwa na kushangiliwa kuwa walifanya kazi yao vizuri na ndiyo inatambuliwa.

Ni pale wale ambao walikuwa au hawakuwa wanakufahamu hadi usiku huo, wanapokuita, tena kwa majina yako yote na kukuambia, “Wewe ndiye mshindi!”

Aliyebuni tuzo hizi aliangalia mbali. Hakuangalia tu, aliona mbali. Kuendelea kuongezeka kwa idadi ya washindani na kazi zinazoshindanishwa, ni ushahidi kuwa ushindani huu unakubalika miongoni mwa waandishi wa habari, vyombo vyao na wamiliki wa vyombo hivyo.

Ni ushahidi pia kuwa wanaodhamini mashindano haya, kwa kutoa zawadi; kampuni, mashirika, taasisi, asasi na jumuiya mbalimbali, wanaendelea kutambua thamani ya kazi ya uandishi wa habari na umuhimu wa kukuza stadi na mbinu.

Na jinsi waandishi wengi wanavyoshiriki na kazi nyingi kushindanishwa, ndivyo MCT inavyojisikia na kujiona kuwa inachofanya, siyo tu kizuri, bali halali na sahihi.

Sasa hapa ndipo ninaleta ujumbe kwa kila mwandishi wa habari: Kila unapotafuta taarifa ili uandike habari, kuwa na wazo kuwa unashindana.

Haina maana kwamba waandishi wote wanatafuta taarifa zilezile na wataandika kazi moja. Hapana. Ni taarifa mbalimbali kwa stori tofauti lakini kwa kutumia stadi na mbinu zilezile za uandishi. Kwahiyo? Kila mmoja aandike akijua kuwa kazi yake yaweza kushindanishwa – kesho au keshokutwa.

Mashindano hayaandaliwi au kusimamiwa na MCT peke yake duniani kote. Yako sehemu tofauti, mataifa mbalimbali na yanaendeshwa na taasisi na asasi tofauti.

Kuna wasioitisha mashindano. Wanasoma magazeti, wanasikiliza redio na kutazama televisheni; wanakumbana na stori au makala yako na kusema “mwandishi wa hiki hapa amekitendea haki.”

Kwahiyo, wanakuita. Wanakueleza kuwa kazi yako fulani ni nzuri na bora kwa kipindi fulani. Wanakutambua. Ikiwezekana wanakuzawadia. Wanakutangaza ndani na nje ya nchi yao.

Si ajabu kwa MCT kuanza kuboresha utaratibu wake wa kupata washindani. Leo wanaita waandishi wapeleke kazi zao wanazotaka kushindanisha.

Kesho wanaweza kusema yeyote aliyesoma, kusikia au kuona kwenye televisheni, stori inayofaa kushindanisha; aandike maelezo ya habari hiyo, aambatanishe ushahidi na sababu za kuipenda; na kuipeleka MCT ikashindanishwe.

Ikifika hapa kazi za kushindanisha zitaongezeka; na hizi kupitia utaratibu mpya, zitakuwa zimetokana na utambuzi wa jamii pana inayofuatilia kazi bora za waandishi wa habari.

Hii maana yake ni kwamba ubora hauonwi na waandishi peke yao. Misingi ya uandishi haifahamiki kwa waandishi peke yao. Uzito wa maudhui na kina cha habari havieleweki kwa waandishi peke yao.

Unaweza kukuta hata yule ambaye hakupeleka kazi yake, anakuwa mshindi katika EJAT. Hilo likitokea nitakuwa wa kwanza kushangilia.

Bali hapa ninamwandikia mwandishi wa habari katika mazingira ya sasa: Tafuta taarifa, andika kama anayeshindana kwa kutumia vigezo vyote vya uandishi bora.

Usipopata nishani, utapata sifa ya kuandika habari isiyoleta usumbufu kwa mhariri msanifu; utakuwa mfano kwa ambao bado wanajifunza; utakuwa tegemeo la wanaokuajiri au nguzo yao kati katika chombo chako cha habari.

Wasiliana na Mhariri wa Jamii kwa namba: 0713 614 872/0763 670 229