Twende mbali zaidi ya kukemea mateke ya Koffi Olomide kwa Pamela

Muktasari:

Huku mitaani tunashuhudia wanawake wakipewa vipigo vya mbwa mwizi. Chumba cha jirani kila siku mwanamke anapigwa lakini upo kimya. Mwingine amepigwa mbele yako muda mfupi uliopita na haujachukua hatua yoyote.

Teke moja tu alilomrushia dansa wake linamgharimu. Anaonekana mwanamume wa ovyo asiye na maana. Sasa yupo jela na jamii yote Afrika inaonekana kupendezwa na hatua hiyo ya Serikali ya Congo.

Huku mitaani tunashuhudia wanawake wakipewa vipigo vya mbwa mwizi. Chumba cha jirani kila siku mwanamke anapigwa lakini upo kimya. Mwingine amepigwa mbele yako muda mfupi uliopita na haujachukua hatua yoyote.

Ni teke moja lakini la kuogofya kwa imani kuwa kama jambo hilo limefanyika hadharani, je, yanayofanyika nyuma ya pazia ni makubwa kiasi gani?

Unyanyasaji dhidi ya wanawake upo kwa kiwango kikubwa katika maeneo unayoishi. Hili alilofanya ni kielelezo tu kuwa hali imekuwa mbaya katika jamii yetu. Kumkemea Koffi Olomide peke yake haitoshi, anza kwa aliye karibu na wewe.

Ni jambo la kushangaza kwa sababu limefanyika hadharani lakini ukweli ni kwamba karibu nusu ya wanawake wote Afrika wanapitia unyanyasaji wa aina hiyo. Kwa mujibu wa Shirika linaloshughulikia Idadi ya Watu (UNFPA) wanawake 45 kati ya 100 hunyanyaswa na wanaume.

Unyanyasaji huu haufanywi na watu wa mbali, tumeona Pamela amenyanyaswa na bosi wake vivyo hivyo kwa wengine. UNFPA inasema ni aghalabu mwanamke kunyanyaswa na mtu asiyemjua. Wengi hufanyiwa ukatili na watu wao wa karibu.

Pia, wanakosa ulinzi baada ya kufanyiwa ukatili na mfano mzuri ni Pamela. Utaona wakati Serikali ya Kenya imetangaza kumshughulikia Olomide kwa kumrudisha kwao, dansa huyo na wenzake walipakiwa katika ndege moja.

Katika mijadala hakuna anayezungumzia hatma ya dansa huyo. Je, Olomide ataendelea kumuajiri katika bendi yake na vipi safarini wenzake walikuwa wanamwambia nini au kumuonaje.

Pengine masimango yalitawala usiku mzima kabla ya safari kutoka kwa wenzake wakimwambia kama siyo ukorofi wake bosi wao asingekamatwa. Labda safari nzima walikuwa wakimzodoa kwa kuharibu jina la kiongozi wao na pia kuwakosesha mapato.

Hakuna anayejua hatima ya Pamela. Olomide anapata anachostahili lakini vipi uhusu mwathirika huyo.

Kina Pamela wapo wengi. Olomide ni tajiri anayeweza kuendelea kuishi vizuri baada ya sekeseke hili kwisha, Pamela je?