UCHAMBUZI: Nyonyesheni watoto acheni visingizio

Wakati Tanzania inajiandaa kuadhimisha wiki ya unyonyeshaji duniani ambayo huadhimishwa Agosti kila mwaka, imebainika kwamba hapa nchini kuna wanawake wanaotumia sindano za kukausha maziwa kukwepa kuwanyonyesha watoto wao.

Wapo ambao wanatoa sababu ambazo binafsi naziona hazina msingi wala tija, eti wanahofia kuharibu maumbile yao kutokana na unene unaosababishwa na kunyonyesha na wengine wanadai eti wakinyonyesha maziwa yatalala.

Lakini kaulimbiu ya maadhimisho hayo ambayo tayari imeshatolewa inayosema; ‘Unyonyeshaji ni ufunguo wa maendeleo endelevu’, inakinzana na madai ya baadhi ya wanawake hao ambao wanajitazama wao zaidi badala ya afya ya mtoto yule aliyezaliwa.

Utafiti mpya wa Shirika la Afya Duniani (WHO) uliotolewa wiki iliyopita unaonyesha kuwa takribani watoto 7.6 milioni duniani hawanyonyeshwi kila mwaka, wakiwamo wa Tanzania. Hii ni changamoto inayopaswa kufanyiwa kazi kwa sababu wataalamu wa afya wanatuambia maziwa ya mama ni kinga tosha dhidi ya maradhi na ili mtoto akue vizuri, anatakiwa kunyonya maziwa ya mama pekee bila kuchanganya na chakula kingine ndani ya miezi sita mfululizo, jambo linaloonekana kutozingatiwa na kina mama takribani 700,000 nchini. Kihalisia, mtoto mchanga ana tabia ya kulala usingizi ndani ya saa moja baada ya kuzaliwa tunaambiwa na madaktari bingwa wa watoto. Wanasema ndani ya muda huo anapaswa kunyonyeshwa, kwa hiyo mama asione uvivu wala maumivu kumnyonyesha. Wanasema mtoto hatakuwa na hamu ya kunyonya ndani ya muda huo hivyo ni jukumu la mama kumshawishi anyonye. Lakini pamoja na maelezo hayo ya madaktari na wataalamu wa afya wanayoyatoa kwenye kliniki za wajawazito, wapo ambao wanathubutu hata kujidunga sindano baada ya kujifungua ili kuzuia maziwa yasitoke kusudi wasinyonyeshewatoto wao, huu ni ukatili. Inashangaza kuona wanawake wakijifunza mbinu zisizofaa za kukausha maziwa kusudi tu wakwepe wajibu wao wa kuwanyonyesha watoto wao.

Lakini wakumbuke kuwa kitendo cha kuyazuia maziwa ambayo ndicho chakula pekee anachopaswa kupewa mtoto katika miezi sita ya ukuaji wake baada ya kuzaliwa, ni cha hatari pia kwa afya ya mama.

Inaelezwa kutokana na vitendo hivyo, mama anaweza kupata saratani ya matiti. Chapisho moja lililotolewa na Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, linasomeka, “Maziwa yanapozuiwa kutoka nje huchochea kwa asilimia kubwa mwili wa mama anayepaswa kunyonyesha, kutengeneza chembechembe ambazo baadaye husababisha saratani ya matiti.” Hivyo, kama mama atazingatia umuhimu wa kumnyonyesha mwanawe ndani ya muda unaoainishwa na wataalamu, atakuwa pia anajiepusha na maradhi ya saratani.

Najiuliza, hivi kipi bora, kuugua saratani au kulinda umbo la mwili wako! Mama uchekwe barabarani kwa kuwa na mtoto aliyedumaa ama utapiamlo kwa kukosa maziwa yako au umnyonyeshe kusudi ujidai mbele za watu kuwa na mtoto mwenye afya bora? Hakuna anayebisha kuwa mama anayenyonyesha anapaswa kula chakula cha kutosha kusaidia kutengeneza maziwa ya kumlisha mtoto wake, lakini wakati wa kunyonyesha kuna maelekezo hutolewa na wataalamu wa afya ambayo yanapaswa kuzingatiwa kusudi mama asinenepe kupita kiasi. Na wapo wengine wanaozingatia ushauri wa wataalamu unaowasaidia kupanga uzazi bila kutumia njia za uzazi wa mpango hata kama anashiriki tendo la ndoa anaponyonyesha kwa kuzingatia hatua kadhaa wanazoelezwa.

Mwakilishi Mkazi wa Unicef Tanzania, Maniza Zaman aliwahi kusema, “Unyonyeshaji unaweza kuokoa maisha ya mtoto na kuboresha afya yake na unamuwezesha kuwa na upeo mkubwa kiakili jambo ambalo pia ni sifa kwa mama.”

Hivyo, wanawake wanyonyesheni wanenu acheni kuwakatili.

0713 235309