UCHAMBUZI: Serikali iongeze nguvu mapambano dhidi ya homa ya ini

Muktasari:

Wengi wanaogopa zaidi ugonjwa wa Ukimwi wakidhani ndiyo hatarishi kwa sababu hauna kinga wala tiba.

Watu wengi hawajui mengi kuhusu ugonjwa wa homa ya ini lakini ni moja ya magonjwa hatari kwa sasa.

Wengi wanaogopa zaidi ugonjwa wa Ukimwi wakidhani ndiyo hatarishi kwa sababu hauna kinga wala tiba.

Homa ya ini ni ugonjwa unaoathiri ini na kusababishia kifo pengine kwa haraka zaidi kuliko hata Ukimwi.

Pamoja na kuongezeka kwa magonjwa mengine yasiyoambukiza, bado kuna haja ya kuweka mikakati madhubuti ya kukabiliana na magonjwa ya kuambukiza ukiwamo huu wa homa ya ini.

Homa ya ini (hepatitis B) ni ugonjwa unaosababishwa na virusi ambao wanashambulia ini na kuleta madhara kwa mgonjwa.

Ugonjwa huo unaenezwa kwa njia ya kuchangia damu au majimaji kutoka kwa mtu mwenye maambukizi hayo.

Kwa mujibu wa takwimu za Shirika la Afya Duniani (WHO), inakadiriwa kuwa zaidi ya watu milioni 257 ulimwenguni kote wanaishi na maambukizi ya virusi vya homa ya ini huku wengine wengi wakiwa hawajui hali zao.

WHO inabainisha pia kwamba, tangu mwaka 2015, watu 887,000 wamefariki dunia kutokana na ugonjwa huo baada ya kuchelewa kupata matibabu kwa wakati.

Takwimu hizo zinatuonyesha kuwa ulimwengu sasa unatakiwa kuimarisha vita dhidi ya ugonjwa huo. Hata hivyo, habari njema ni kwamba homa ya ini ina kinga yake.

Mtu yeyote anaweza kupata chanjo ya kuzuia maambukizi ya homa ya ini ili kujiweka salama wakati wote dhidi ya virusi vinavyosababisha maambukizi hayo.

Kwa sehemu ndogo, Serikali imeanza kutoa chanjo hiyo hapa nchini, lakini tatizo lililopo ni kwamba watu wengi hawana uelewa wa kutosha juu ya athari za ugonjwa huo, hivyo wanapuuzia kupata chanjo.

Elimu zaidi inahitajika ili kuwafanya wananchi wawe na uelewa wa kutosha kujikinga dhidi ya maambukizi hayo na kufuata matibabu kamili pindi inapotokea mtu ameambukizwa.

Hii itasaidia kupunguza kasi ya maambukizi yake.

Pia, Serikali kupitia Wizara ya Afya, iweke mipango madhubuti ya kuwafikia Watanzania wote, mijini na vijijini ili kuutokomeza kabisa ugonjwa huo hapa nchini kwani inawezekana.

Mapambano yakiwa makali, virusi vya homa ya ini havitapata nafasi.

Serikali pia itie mkazo zaidi kwenye chanjo ili kila Mtanzania apate fursa ya kuipata.

Pia, matibabu ya homa ya ini yaimarishwe kwenye zahanati, vituo vya afya na hospitali zote hapa nchini ili kuokoa maisha ya wananchi.

Ifahamike wazi kwamba mgonjwa mwenye maambukizi ya homa ya ini akichelewa kupatiwa matibabu, anapata maambukizi sugu ambayo husababisha kifo.

Uelewa wa wananchi na utashi wa Serikali kupambana dhidi ya homa ya ini ndiyo mafanikio ya vita hii.

Dalili za awali za kutambua ugonjwa huo ni ngozi na macho kuwa ya njano, mkojo mweusi, uchovu wa mwili, kichefuchefu na kutapika na maumivu chini ya tumbo. Dalili hizo hujitokeza siku ya 30 mpaka 60 tangu mtu alipopata maambukizi.

Watoto walio chini ya umri wa miaka sita wako hatarini zaidi kupata maambukizi sugu.

Takwimu za WHO zinaonyesha asilimia 80 hadi 90 ya watoto wachanga chini ya mwaka mmoja, wako hatarini kupata maambukizi sugu wakati asilimia 30 hadi 50 ya watoto chini ya miaka sita, wako hatarini pia kupata maambukizi sugu.

Kwa takwimu hizo, wazazi wana jukumu kubwa la kuwatunza na kuwasimamia watoto wao ili kuhakikisha wanaepuka mazingira yote yanayoweza kuwasababishia maambukizi ya homa ya ini.

[email protected] au 0763891422Afya ya jamii inalindwa na jamii yenyewe kwa kuzingatia usafi na kanuni zote za afya.

Serikali inasaidia kwa kuweka miundombinu na sera wezeshi ambazo zitaisaidia jamii husika kuimarisha mazingira bora ya kifya.

Homa ya ini ni ugonjwa hatarishi kama utafumbiwa macho na wananchi pamoja na Serikali.

Lakini tukishirikiana kwa pamoja tutaishinda vita hii.

Aghalabu watu huenda hospitali kuangalia afya zao, basi sasa tujenge utamaduni wa kuangalia afya zetu na kupata chanjo zinazotolewa na Serikali.

Afya ni mali, Afya ni uhai, Afya ni silaha. Kila mtu abebe jukumu la kuangalia afya yake, ya jirani yake na jamii nzima anamoishi.

Tukifanya hivyo, tutafanikiwa katika mapambano ambayo tumeshayaanza.

Peter Elias ni mwandishi wa gazeti hili – [email protected] au 0763891422