Wednesday, April 19, 2017

UCHAMBUZI: Tuna haja gani na vyama 20 vya siasa

 

By Fredrick Nwaka, Mwananchi

Julai 1992 Tanzania ilirejea katika mfumo wa vyama vingi vya siasa. Kilikuwa kipindi muhimu na cha mafanikio kwa wanaharakati wa mageuzi kama Mabere Marando, James Mapalala, Bob Makani na Edwin Mtei na wengine ambao waliongoza harakati hizo za kupigania mfumo huo.

Harakati za kudai kurejeshwa mfumo wa vyama vingi zilikolea nchi nzima na mwaka 1991, Rais Ally Hassan Mwinyi aliteua Tume iliyoongozwa na Jaji Mkuu, Francis Nyalali kukusanya maoni ya wananchi na kutoa mapendekezo kujua kama taifa lilihitaji mfumo wa vyama vingi au kuendelea na mfumo wa chama kimoja.

Harakati hizo zilisababisha kubadilishwa kwa Katiba ili kurejesha mfumo huo ambao ulikuwa umefutwa Januari 14, 1963 kwa Azimio la Halmashauri Kuu ya Tanu.

Kurejeshwa kwa mfumo wa vyama vingi kulisababisha kuanzishwa kwa Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambayo kwa mujibu wa Sheria namba 5 ya mwaka 1992, mbali na kusajili vyama anapaswa kuhakikisha sheria hiyo inafuatwa na vyama vya siasa. Kwa mujibu wa tovuti ya Msajili wa Vyama vya Siasa, kufikia sasa Tanzania ina vyama vya siasa 19 vilivyosajiliwa na ambayo kwa mujibu wa sheria iliyovianzisha inavitaka kufanya mikutano ya hadhara na ndani, kuwa na wanachama Tanzania Bara na Zanzibar.

Chama cha siasa kinatakiwa kuonekana kikifanya siasa wakati wote bila kujali vikwazo na changamoto zilizopo. Katika hili lazima niseme bado kuna changamoto. Nchi ina vyama 19 lakini vinavyofanya siasa, havizidi vitano ambavyo ni Chadema, ACT, CUF, NCCR na CCM.

Hii maana yake ni kwamba kuna vyama ambavyo vipovipo tu na vinaibuka nyakati za uchaguzi vikidai vinaomba vichaguliwe kuongoza nchi.

Mathalani, ADC wako wapi? UMD wanafanya nini? NRRA, UPDP, Chaumma na TLP nao wanafanya siasa zipi? Mbona siwasikii. Sipepesi, mimi ni muumini wa mfumo wa vyama vingi kwa sababu moja tu. Kuwa na mawazo tofauti kwa lengo lilelile la kuleta maendeleo katika nchi yetu lakini sikubaliani na uwepo wa idadi kubwa ya vyama visivyokuwa na tija. Ni bora kuwa na vyama viwili au vitatu imara kuliko kuwa na vyama zaidi ya 20 vinavyojificha kabatini na kuibuka wakati wa uchaguzi.

Kama kuwa na idadi kubwa ya vyama vya siasa kungekuwa ndiyo kichocheo cha maendeleo, Malawi ingekuwa miongoni mwa mataifa ya Afrika yaliyopiga hatua kimaendeleo.

Malawi ambayo imetawaliwa na vyama vitatu vya MCP, UDF na sasa DPP tangu ilipopata uhuru kutoka kwa Uingereza mwaka 1964, bado ni taifa lililotopea katika umaskini, licha ya kuwas na vyama vya siasa 40 vilivyosajiliwa.

Kenya inayojiandaa na uchaguzi mkuu baadaye mwaka huu ina vyama vya siasa 22 vilivyosajiliwa na vingine 22 viko katika mchakato wa usajili, lakini havijafanikiwa kumaliza migawanyiko ya kikabila na kikanda iliyogubika siasa za nchi hiyo.

Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambayo tangu imepata uhuru 1960 kutoka Ubelgiji haijafanikiwa kumaliza matatizo ya kiusalama na kisiasa, ina zaidi ya vyama 25.

Zambia ina zaidi ya vyama 20 vilivyosajiliwa lakini ni vichache vinavyomudu kufanya siasa za ushindani vikiwamo PF, MMD, UPND, Ada na FDD vyenye uwakilishi bungeni.

Uganda ina vyama vya siasa 12 lakini ni viwili vya NRM kinachoongoza na Rais Yoweri Museveni na FDC kinachoongozwa na Mugisha Muntu na Kizza Besigye vinavyofanya siasa. Vingine kama vinafanya basi ni kwa bahati mbaya.

Jambo lililo dhahiri ni kwamba wanasiasa wengi barani Afrika wanaanzisha vyama kwa tamaa ya kupata madaraka na si kujenga mifumo imara itakayosaidia nchi zao kupiga hatua za maendeleo.     

-->