UCHAMBUZI: Ubabe uepukwe ukusanyaji kodi

Muktasari:

Misururu mirefu ya wananchi kulipa kodi hasa ya majengo ni ushuhuda wa utayari wa jamii kutoa ushirikiano wa kuimarisha mapato ya Serikali. Ni kipindi ambacho Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inahudumia wateja wengi zaidi.

Ukusanyaji wa mapato ya Serikali ni suala lililopewa kipaumbele na Serikali ya Awamu ya Tano. Nguvu za kutosha zimeelekezwa katika maeneo yote yanayotakiwa kukusanywa kodi hasa ya mapato kwa kiasi kubwa kwa kubana mianya mingi ya ukwepaji.

Misururu mirefu ya wananchi kulipa kodi hasa ya majengo ni ushuhuda wa utayari wa jamii kutoa ushirikiano wa kuimarisha mapato ya Serikali. Ni kipindi ambacho Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) inahudumia wateja wengi zaidi.

Hii ni kutokana na ongezeko la uelewa na mwamko wa wananchi juu ya umuhimu wa kulipa kodi kwa ridhaa yao bila kushurutishwa kufanya hivyo, ingawa usimamizi na utekelezaji wa sheria za kodi umechangia watu kuwa makini kutimiza wajibu huu muhimu.

Hata hivyo, katika usimamizi wa sheria na taratibu za ukusanyaji wa mapato haya una changamoto kutoka kwa wakusanyaji na watumishi wanaohusika na eneo hili.

Wakusanyaji wa mapato haya ya Serikali ni tatizo kwenye maeneo mengi kwani utendaji wao siyo rafiki; ni wababe, wenye lugha chafu na za kejeli. Upo ukiukwaji wa sheria na taratibu katika mchakato wa ukusanyaji wa mapato haya ya Serikali.

Katika kipindi hiki ambacho uelewa na mwamko wa ulipaji kodi umeongezeka, tusingetegemea vitendo hivi kufanywa na watumishi wa TRA, halmashauri, polisi au idara nyingine za Serikali ambazo kwa namna moja au nyingine zinahusika na ukusanyaji wa mapato kisheria.

Kumekuwa na ukiukwaji mwingi wa taratibu katika kudai mapato. Watumishi hawa hudhalilisha, hubambikia viwango vikubwa vya kodi huku ubabe na lugha chafu zikitolewa bila sababu za msingi jambo ambalo ni baya.

Walipakodi wengi siyo wakaidi hasa katika kipindi hiki ambacho wanayaona manufaa yanayotokana nazo na wakati mwingine wanashindwa kufanya hivyo kutokana na changamoto za kibiashara hivyo kuhitaji staha, elimu na utaratibu muafaka unaotakiwa kufuatwa ndani ya muda uliopangwa.

Hata hatua za kisheria zinapochukuliwa kwa ambao hawajalipa kwa wakati, kuna taratibu za kufuata na siyo kuvamia na kufunga biashara kibabe na kutoa lugha za kutisha. Hii si sawa na haikubaliki kwani kupitia mazungumzo, inawezekana hali isingefika huko.

Nadhani, kuna haja ya watumishi hawa kupigwa msasa wa namna bora ya kutekeleza majukumu yao na watambue kwamba wanachokifanya si ugomvi unaohitaji ubabe, bali weledi unaoweza kumfanya mlipakodi ajisikie fahari anapotimiza wajibu wake.

Ili kufanikisha malengo ya ukusanyaji kodi, walipaji wanastahili staha na kuthaminiwa na siyo kuburuzwa kwani kwa kufanya hivyo Serikali inaweza kukosa mapato haya muhimu kwa maendeleo ya nchi.

Kuna malalamiko kuhusu namna baadhi ya watumishi wa mamlaka zinazohusika na ukusanyaji kodi zinavyotumia njia zisizo za kistaarabu.

Ni lazima wabadilike na taratibu zifuatwe kufanikisha hilo. Kwa bahati nzuri, sheria zipo ingawa wao huamua kuziweka pembeni na kutumia nguvu na ubabe jambo ambalo siyo sawa kabisa.

Elimu iendelee kutolewa juu kodi zote ambazo mfanyabiashara anatakiwa kuzilipa na kiwango chake na muda wa kufanya hivyo. Pia, kodi zilizofutwa au kurekebishwa zifahamike. Mameneja wa wilaya na mikoa wanaweza kusaidia hili.

Mgawanyo wa ukusanyaji pia uwe wazi. Kwa mfano, kuna zinazokusanywa na TRA zibainishwe au zile zinazoenda halmashauri au faini za zinazokusanywa na Polisi, Zimamoto au Idara ya Misitu, Sumatra au Ewura.

Mwandishi anapatikana kwa namba 0716069926