UCHAMBUZI: Vyovyote iwavyo, siasa isiathiri biashara

Nimelazimika kuandika makala haya ili kutoa ufafanuzi kuhusu dhana ya ujamaa kwa kadri ya uelewa wangu baada ya kupata ukakasi kila niliposikia mjadala kuhusu itikadi ya Tanzania.

Najua tutatofautiana mawazo lakini tutaafikiana kwa faida ya kizazi cha baada ya Azimio la Arusha, mwaka 1967.

Neno ujamaa linahusu mfumo wa maisha, taratibu, mila na desturi, kanuni, misingi, miiko na taswira nzima ya utamaduni wa wa jamii.

Mwalimu Julius Nyerere alipokabiliwa na changamoto za kulijenga taifa lenye makabila yasiyopungua 120, alihitaji ‘utamaduni wa kijamaa’ kufanikisha jukumu hilo.

Pamoja na tofauti nyingi za kimila, desturi na lugha baina ya makabila hayo, kitu kimoja kilichokuwamo kwa kila kabila ni utamaduni wa kijamaa.

Baada ya tafakuri ya kina, Mwalimu alibaini kabla ya kuzungumzia maendeleo au kurahisisha namna ya kuyaleta ni lazima makabila yote yawe kitu kimoja.

Nyenzo muhimu katika kujenga taifa litakalotanguliza utaifa kabla ya mambo mengine ni lugha na utamaduni mmoja wa Kitanzania.

Lugha itarahisisha mawasaliano baina ya makabila na utamaduni utayaleta makabila kuwa kitu kimoja.

Ili kufanikisha azma hiyo, Mwalimu Nyerere aliitumia vilivyo fursa iliyokuwapo mbele yake ya kutoa nafasi kwa Kiswahili kustawi na kushamiri kila pembe au kona ya nchi bila ya vipingamizi au masharti yoyote.

Lugha hii iliyoanza kuendelezwa na Watanzania mashuhuri na wabobezi wakiwamo Shaaban Robert, ilipata mchepuo mpya wa kustawi zaidi chini ya uongozi na uangalizi wa Mwalimu Nyerere akiwa ndiye muasisi wa taifa huru.

Hakuifanya kazi hiyo peke yake, lakini chini ya uongozi wake, Kiswahili kiliweza kustawi nchini na kuvuka mipaka kwenda ulimwenguni kote.

Utamaduni wa taifa ndiyo msingi wa maisha na maendeleo ya taifa husika.

Kwa bahati mbaya nikiri kwamba, ujamaa baada ya kuibuliwa na Mwalimu haukupata vichwa vya kuutolea ufafanuzi wa kina na kuuendeleza kifikra ili uweze kuchukua nafasi stahiki kama mwongozo wa maisha ya kila siku ya Watanzania, kizazi hadi kizazi.

Kama nilivyosema awali, ujamaa siyo itikadi ya kisiasa bali ni utamaduni wa Kitanzania japo ulifananishwa kimakosa na usoshalisti. Wenyewe ni nyenzo muhimu katika kutoa dira na mwelekeo wa mila na desturi, taratibu za maisha, nidhamu ya kazi na mfumo wa maisha ya jamii.

Ndiyo nguzo muhimu katika kuhakikisha itikadi yoyote ya kisiasa itakayopata nafasi ya kuongoza na kusimamia kanuni na taratibu za uzalishaji mali katika nchi, inajiwezesha ili isikinzane na utamaduni wa taifa.

Itikadi zinazofahamika zaidi duniani ni pamoja na usoshalisti, ukomunisti, usoshalisti wa kidemokrasia, uliberali, ubepari, na ubepari uliokithiri.

Kutokana na maendeleo ya kiuchumi na kisiasa yaliyopatikana ulimwenguni, njia bora ya kuyaendeleza na kuyasimamia kwa tija maendeleo hayo ni mfumo wa utawala wa demokrasia ya vyama vyingi vya siasa na utawala bora utakaozingatia Katiba ya nchi.

Kila chama cha siasa huchagua aina ya itikadi itakayoona inafaa na yenye manufaa kwa taifa lakini hakuna chama chenye fursa ya kuwachagulia wananchi aina ya utamaduni utakaowafaa.

Kazi hiyo ilishafanywa na muasisi wa taifa hili. Itikadi ya kisiasa itakashindwa kuleta matunda yaliyotarajiwa ni rahisi kujaribu aina nyingine lakini utamaduni wa taifa ukigeuzwa kuwa itikadi, utakapofeli kuleta manufaa yaliyotarajiwa, hakutakuwa na mbadala. Taifa litaparaganyika.