UONGOZI : Zamu ya mwanamke kushika hatamu imefika

Ellen Johnson Sirleaf alikuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini Liberia.

Muktasari:

  • May amekamata wadhifa huo wa juu kabisa nchini humo baada ya David Cameron kujiuzulu. Pamoja na kuwa May anatarajiwa kuongoza mchakato wa mazungumzo ya kuondoka kwa Uingereza katika nchi za Umoja wa Ulaya (EU).

Dar es Salaam. Margaret Thatcher ndiye mwanamke wa kwanza kuwa Waziri Mkuu wa Uingereza, ni kama alikuwa anafungua njia kwa sababu baada ya kupita mawaziri wakuu wengi wanaume ameingia tena mwanamke ambaye ni Theresa May.

May amekamata wadhifa huo wa juu kabisa nchini humo baada ya David Cameron kujiuzulu. Pamoja na kuwa May anatarajiwa kuongoza mchakato wa mazungumzo ya kuondoka kwa Uingereza katika nchi za Umoja wa Ulaya (EU).

Inawezekana huu ukawa ni wakati wa wanawake kwani mbali na Uingereza, nchi nyingi zina viongozi wanawake zikiwamo, Ujerumani.

Angela Merkel ni mwanamke wa kwanza kuwa kansela wa Ujerumani aliyechaguliwa mwaka 2005. Imeelezwa kuwa Merkel amesababisha kupanda kwa uchumi Ujerumani.

Upo uwezekano pia wa Taifa la Marekani kutawaliwa na mwanamke iwapo mgombea wa Chama cha Democratic, Hillary Clinton atamrithi Rais Barrack Obama katika uchaguzi utakaofanyika baadaye mwaka huu.

Bangladesh

Sheikh Hasina alichaguliwa kuwa Waziri Mkuu tangu mwaka 2009.

Norway

Erna Solberg aliteuliwa kuwa Waziri Mkuu wa pili mwanamke mwaka 2013.

Namibia

Machi 2015 Rais Hage Geingob alimchagua Saara Kuugongelwa-Amadhila kuwa Waziri Mkuu nchini humo.

Myanmar

Mshindi wa tuzo ya Nobel, Aung San Suu Kyi

alikuwa Waziri Mkuu alichaguliwa katika Uchaguzi Mkuu uliofanyika nchini humo 2015.

Liberia

Ellen Johnson Sirleaf alikuwa Rais wa kwanza mwanamke nchini humo mwaka 2005, mwanamke huyo aliibuka mshindi tena na kuongoza kwa awamu ya pili katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2012.

Korea Kusini

Park Geun-Hye Rais wa kwanza mwanamke kuongoza taifa lenye maendeleo makubwa zaidi ya kiuchumi barani Asia.

Hao ni baadhi ya wanawake viongozi walioshika nyadhifa za juu, kana kwamba hiyo haitoshi na Tanzania inaingia katika orodha hiyo baada ya kuwa na Makamu wa Rais mwanamke, Samia Suluhu Hassan kwa mara ya kwanza tangu ipate Uhuru mwaka 1961.

Katika kile kinachoonekana wanawake wanatakiwa kuinuka kwa kung’amua kuwa wakati wao wa kufanya hivyo umefika, ni kile kilichojitokeza katika kinyang’anyiro cha uchaguzi wa awamu ya tano, katika wagombea 42 wa CCM waliojitosa kuwania nafasi ya urais baada ya mchujo wanawake wawili, Asha-Rose Migiro, Balozi Amina Salum waliibuka kidedea na kubaki katika tatu bora. Hii ni mara ya kwanza pia kwa Tanzania kulishuhudia hilo.

Vikwazo

Hata hivyo, wanawake wanakabiliwa na changamoto nyingi. Kuna baadhi ya viti vimekuwa vikwazo duniani kote kwa maendeleo ya mwanamke kwa ujumla.

Nafasi ya kupata elimu

Taarifa ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu, Sayansi na Utamaduni (Unesco) ya mwaka 2013 ilibaini kuwa watoto wa kike milioni 31 duniani wenye umri wa kwenda shule hawapati nafasi hiyo, huku mmoja kati ya wasichana wanne katika nchi zinazoendelea ikiwamo Tanzania hawajamaliza elimu ya msingi.

Hali hii inachangia kwa kiasi kikubwa kwa wanawake kutokuwa na nguvu au nafasi ya kufanya maamuzi.

Nafasi za kazi

Takwimu zinaonyesha katika nchi zilizoendelea kama Marekani na kwingine wanawake bado wana nafasi ndogo ya kupata kazi.

Kwa mfano Marekani, mwanamke anapata dola 0.77 kwa kila dola moja anayopata mwanaume.

Kibaya zaidi pamoja na kupata kiasi kidogo cha fedha tafiti zinaonyesha kuwa nyingi zinatumika katika masuala ya familia tofauti na wanaume ambao hutumia kujikimu.

Afya na haki za uzazi

Katika nchi zinazoendelea kama Tanzania imeelezwa kuwa wanawake milioni 225 hawapati elimu ya uzazi wa mpango inayojitosheleza.

Kwa mujibu wa Jumuiya ya Wanawake nchini Marekani ya Woman Deliver wanawake wanakosa ushauri wa kisheria na kusababisha kupatikana mimba zisizotarajiwa milioni 74 na zinazotolewa milioni 36 kila mwaka.

Afya ya uzazi, unyanyasaji

Shirika la Afya Duniani (WHO) limekadiria wanawake 800 hufa kila siku kutokana na kuzuia ujauzito bila kupata ushauri wa kitaalamu.

Kwa mujibu wa WHO, kila wanawake watatu mmoja amepata unyanyasaji wa kijinsia iwe kipigo au kingono na kusababisha wanawake wengi kuishi bila furaha na afya bora.

Ndoa za utotoni

WHO wanakafidia kuwa kuanzia mwaka 2011 hadi kufikia 2020 wasichana milioni 140 watakuwa wamefunga ndoa wakiwa katika umri mdogo.

Wasichana wanaoozeshwa katika umri huo hukosa nafasi ya kupata elimu na kukubali manyanyaso ya kila aina kutokana na kukosa maamuzi.

Jamii inasemaje?

Mkazi wa Mbagala Majimatitu jijini Dar es Salaam, Zakhia Rakif anasema mwanamke wa kawaida ambaye ametoka katika familia yenye kipato cha chini bado ana safari ndefu.

Anasema hii inatokana na kutopata nafasi katika jamii inayomzunguka kutokana na uduni wa maisha.

“ Hawezi kusikilizwa hata kama ana mawazo mazuri, ukilinganisha na mwanamume ambaye hupewa nafasi bila kujali ana kipato, amesoma au laa,” anasema Zakhia.

Zakhia anasema hata katika kazi wanawake bado wapo chini ikinganishwa na wanamume ambao hupandishwa vyeo kwa kazi inayolingana au inayofanywa sawa na wanawake.

Sharifu Twinde, mkazi wa Sinza Madukani Dar es Salaam anasema familia zinachangia kuwagawa wanawake na wanaume kuanzia ngazi za chini.

Anasema ni rahisi kwa familia kukubaliana kumpeleka shule mtoto wa kiume na wa kike abaki nyumbani kulinda nyumba, kupika, kufua na kufanya kazi za nyumbani.

“Hata katika mgawanyo wa kazi, nyingi anafanya mtoto wa kike na mtoto wa kiume hutumia muda mwingi kujisomea,” anasema.

“Hakuna tabia inayonikera kama mwanamke akiolewa kuzuiwa kufanya kazi, hili limekuwa linachangia kudumaza fikra na mitizamo yao ya kimaisha,” anasema Ally Uledi, mkazi wa Keko Bora jijini Dar es Salaam.

Uledi anasema kama mwanamke akiachwa atimize ndoto zake na kupewa nafasi anaweza kuliko mwanamume.

Anafafanua kuwa tangu zamani mwanamume anabebwa na tamaduni zilizokuwapo ambazo zimekuwa zikimbana mwanamke, lakini bado wanaonyesha uwezo.

“Hicho ni kipimo tosha kuwa wanaweza, cha kufanya waongeze bidii na wasikuba kurudishwa nyuma na kukatishwa tamaa,” anasema Uledi.

UTEUZI

Licha ya dunia kutambua umuhimu wa mwanamke na kushiriki katika ngazi za juu, Tanzania bado juhudi zinahitajika kumpandisha afike katika kiwango cha juu zaidi, ikiwamo katika kutoa maamuzi.

Utafiti uliofanywa mwaka jana na Chama cha Waajiri Tanzania (Ate) kupitia mradi wa Mwanamke wa Wakati Ujao umebaini asilimia 35 ya wanawake wapo kwenye ngazi za maamuzi sehemu za kazi.

Mratibu wa Programu ya Mwanamke wa Wakati Ujao ya Ate, Lilian Machera anasema utafiti huo ulikuwa na lengo la kufichua mambo yanayowazuia wanawake kufika ngazi za juu katika maeneo ya kazi hasa sekta binafsi na za umma.

“Utafiti huu ulifanywa katika kampuni 300 za sekta binafsi Mkoa wa Dar es Salaam kwa lengo la kupata ufumbuzi wa kudumu kuwasaidia wanawake kupata nafasi za juu katika maeneo ya kazi,” anasema.

Anasema matokeo hayo pia yamebaini hisia, mambo ya kifamilia na kujiamini ni kikwazo kwa wanawake kufikia malengo yao sehemu za kazi. Alisema malengo makuu ya mpango huo ni kupata wanawake wengi zaidi katika nafasi za uongozi na kufikia ngazi za bodi za kampuni.

Miongoni mwa wanawake waliofanikiwa kufika katika nafasi ya juu ni Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, anatumia nafasi ya uwapo wa mradi huo kuwaasa wanawake kujiamini na kufikia lengo la kuwa na asilimia 50 kwa 50.

Ate kwa kushirikiana na vyama vya waajiri nchini Norway walianzisha mradi huo ili kuboresha na kukuza ufanisi wa mwanamke katika nyanja za uongozi kwa kutoa mafunzo.

Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu anasema ili mwanamke afanye kazi vizuri lazima awe na afya njema.

Anasema jukumu lao kama Serikali ni kuhakikisha kila Mtanzania anapata huduma za matibabu sawa kwa wanaume na wanawake pale walipo.

Anafafanua zaidi kuwa kutokana na tabia za kimaumbile na kiasili za mwanamke, juhudi za kuhakikisha anapata elimu ya kujitambua na kutambua maumbile yake zinaendelea.

“Jukumu letu ni kuhakikisha mwanamke anapata elimu ya uzazi ili kupiga vita mimba za utotoni na kutoa adhabu kali kwa wanaowakatishia masomo,” anasema Waziri Mwalimu.