Uamuzi wa Msajili wa Vyama umeongeza mpasuko CUF

Msajili wa vyama vya siasa nchini, Jaji Francis Mutungi akizungumza na wandishi wa habari jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Msajili Msaidizi idara ya usajili wa vyama, Sixty Nyahoza. Picha ya Maktaba

Muktasari:

  • Kumekuwa na hofu kwa wafuasi wa CUF hasa wa Zanzibar ambao wana wasiwasi kwamba kurudi kwenye uenyekiti wa chama hicho, Profesa Lipumba kunaweza kudidimiza madai yao ya kudai haki ambayo wanadai waliporwa katika Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofutwa. Jambo jingine linalotia shaka ni iwapo Profesa Lipumba ataelewana tena na kufanya kazi pamoja na Katibu mkuu wake, Maalim Seif au atatafuta mbinu na kutaka kulipa kisasi kwani kwa siku kadhaa alikuwa akimshutumu Maalim Seif hadharani. Mazingira hayo bila shaka yoyote yanaweka mtihani mgumu CUF na umakini mkubwa unahitajika ili kupita salama kipindi hiki kigumu ambacho kinakikabili chama hicho.

Chama cha Wananchi (CUF) ni moja ya vyama vyenye historia tangu mfumo wa vyama vingi vya siasa uanze nchini mwaka 1992.

Licha ya CUF kupoteza nafasi ya kuwa chama kikuu cha upinzani nchini kwa maswahiba wake, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), chama chenye hadhi kubwa miongoni mwa vyama vya upinzani.

Hata hivyo, chama hicho ndicho chenye nguvu katika visiwa vya Zanzibar na kimekuwa kinatoa ushindani mkubwa kwa chama tawala, CCM katika kila uchaguzi tangu uchaguzi wa kwanza chini ya mfumo wa vyama vingi uliofanyika mwaka 1995.

Chama cha CUF mara kadhaa kinadai kilishinda Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar na mgombea wake wa urais wa Zanzibar, Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif Sharif Hamad alishinda kiti hicho.

CUF na Maalim Seif wanadai Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar uliofanyika Oktoba 25, 2015 walishinda kiti cha urais na ndiyo sababu kuu ya Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi wa Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha kuufuta uchaguzi huo.

Jecha alifuta Uchaguzi Mkuu wa Zanzibar Oktoba 28 siku ambayo alipaswa kumtangaza mshindi wa urais wa Zanzibar. Pia, alifuta matokeo ya wajumbe la Baraza la Wawakilishi na madiwani ambao tayari walishatangazwa kuwa ni washindi na kukabidhiwa vyeti na wasimamizi wa uchaguzi huo.

Katika siku za karibuni CUF imekumbwa na mgogoro uliotokana na uamuzi wa Profesa Ibrahim Lipumba kujiuzulu na baada ya kupita karibu mwaka kuamua kurudi katika nafasi yake.

Kitendo hicho kiliwagawa wanachama wa CUF, huku wengine wakimuunga mkono Profesa Lipumba na wengine wakipinga hatua hiyo na katika mkutano mkuu maalumu wa chama hicho uliokuwa na lengo la kujaza nafasi yake wajumbe waliafiki uamuzi wake wa kujiuzulu.

Baada ya uamuzi huo vurugu zilitokea katika mkutano huo na kulazimika kuahirishwa bila uchaguzi kufanyika na baadaye Baraza Kuu la CUF likamsimamisha uanachama Profesa Lipumba na wanachama wengine kadhaa ambao walipinga hatua hiyo kwa kupeleka malalamiko yao kwa Msajili wa Vyama vya Siasa nchini, Jaji Francis Mutungi.

Uamuzi wa Msajili washtua

Katika uamuzi wa suala hilo Jaji Mutungi aliamua kumrudisha katika nafasi ya uenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba, uamuzi ambao unapaswa kujadiliwa mantiki yake kwani unashtusha.

Uamuzi wa Jaji Mutungi unaacha maswali mengi kuliko majibu pale ambapo unaweza kujiuliza ni vipi mtu ajiuzulu uongozi kwa hiari yake mwenyewe, lakini baada ya kipindi cha mwaka mmoja arudi tena kwenye nafasi hiyo.

Msajili wa vyama vya siasa katika uamuzi wake huo anajenga mazingira ya kuvifanya vyama vya siasa viwe vitu vya kuchezewa na baadhi ya viongozi kwa kuingia na kutoka siku watakayo na baadaye wakitaka kurudi wafanye hivyo, kwani yeye atakuwa anawalinda.

Uamuzi wa aina hii haukubaliki kwa kuwa unaondoa hadhi za vyama na kuwa ni chombo ambacho kinaweza kuchezewa wakati wowote na mtu yeyote akiwa anataka kufanya hivyo.

Profesa Lipumba wakati anataka kujiuzulu alishauriwa na viongozi wenzake wa CUF, wanachama wa chama hicho na viongozi wa dini, lakini hakutaka kuwasikiliza na kuchukua uamuzi huo pamoja na kukiacha chama na kwenda kwenye shughuli zake binafsi.

Inakuwaje baada ya kipindi cha mwaka mmoja msomi huyo awe na hamu tena ya kuongoza CUF ambayo aliitelekeza katika kipindi kigumu wakati inajiandaa kuingia katika Uchaguzi Mkuu mwaka jana.

Msajili hana mamlaka

Hakuna mahali popote katika sheria panapompa haki na mamlaka Msajili wa Vyama vya Siasa kubatilisha uamuzi wowote yale yaliyofikiwa na vikao halali ya vyama vya siasa.

Jambo hilo limewahi kuthibitishwa na Mahakama Kuu ya Tanzania ambayo iliamua kupitia Jaji Thomas Mihayo katika kesi ya Emmanuel Nyenyemela na Magnus Msambila dhidi ya Msajili wa Vyama vya Siasa.

Jaji Mihayo katika kesi hiyo alisema, “sioni popote katika sheria ya vyama vya siasa ambapo msajili ana madaraka ya kubariki au kupinga vikao vya vyama vya siasa au uamuzi ambao vikao hivyo vinafanya”.

Kwa uamuzi huo wa Mahakama Kuu ni wazi Msajili wa Vyama vya Siasa hana mamlaka inayompa nafasi ya kumrudishia uenyekiti wa CUF, Profesa Lipumba na kutengua uamuzi mwingine wa chama hicho.

Utaongeza mgogoro CUF

Bila shaka yoyote uamuzi wa Msajili wa Vyama vya Siasa badala ya kuleta suluhu katika mgogoro wa CUF utachochea zaidi mgogoro huo.

Uamuzi wa msajili katika mgogoro huo wa CUF ni sawa na kujaribu kuzima moto unaowaka kwa kuumwagia mafuta ya petroli kwani maafa ya moto huo yatakuwa makubwa zaidi.

Athari ya uamuzi wa Jaji Mutungi ilionekana siku moja tu baada ya tamko lake kutokana na kitendo cha Profesa Lipumba na wafuasi wake kuvamia ofisi  za chama hicho zilizopo Buguruni na kufanya uharibifu.

Mwandishi wa makala haya ni mchambuzi wa masuala ya siasa na jamii, anapatiakana kwa baruapepe: [email protected] na [email protected]