Wednesday, April 19, 2017

Uanzishaji wa viwanda uzingatie uhifadhi wa mazingira

 

By Anthony Mayunga,Mwananchi

Mkakati wa kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda kama unavyoelezwa na viongozi wa ngazi mbalimbali nchini, unatakiwa kutekelezwa kwa uangalifu mkubwa hasa upande wa hifadhi ya mazingira.

Mkakati huu unatakiwa usifanywe kwa lengo la kutimiza tu ahadi ya Rais John Magufuli bila kuzingatia mahitaji ya uhifadhi wa mazingira, tusipofanya hivyo tutajikuta tunakuwa taifa lililoathirika na uharibifu mkubwa.

Pamoja na nia njema ya Rais ambayo inalenga kukuza uchumi wa nchi na wananchi wake kwa ajili ya kuipeleka Tanzania kwenye uchumi wa kati, lazima tuchukue tahadhari kubwa ili nchi iendelee kubaki salama.

Kwa viwanda vichache vilivyopo sasa tunashuhudia Taifa linakabiliwa na matatizo mengi ya uharibifu wa mazingira unaofanywa na makundi mbalimbali ikiwa ni pamoja na wawekezaji wa viwanda vidogo na vikubwa.

Nani asiyeona jinsi misitu, hifadhi za wanyama na maeneo ya makazi yanavyoharibiwa kwa kivuli cha uwekezaji bila kuangalia athari za uharibifu wa mazingira kwa viumbe hai, yote hayo yakifanywa kwa misingi ya kuifanya nchi kuwa ya uwekezaji.

Ni ukweli usiofichika kuwa hivi sasa kuna makundi mawili, moja linahamasisha ujenzi wa viwanda kila wilaya, jingine chini ya waziri anayehusika na mazingira linalia na uharibifu wa mazingira hasa maeneo ya wawekezaji wenye viwanda.

Ninatambua juhudi ambazo tayari zinaendelea kufanyika, maana ni jambo la kawaida kumsikia waziri au timu yake kila wanapokwenda wakitangaza kufunga viwanda au kuvipiga faini kutokana na athari za kimazingira, lakini naamini kadri viwanda vitakavyoongezeka juhudi zaidi za kuvibana zitatakiwa kuongezwa.

Hii ni kwa sababu malalamiko ya wananchi kuhusu uharibifu, utiririshaji maji yenye kemikali, taka ngumu, moshi na uharibifu wa mifumo ya ikolojia na kusababisha adha kubwa kwa watumiaji, yanaendelea kutoka kila kona ya nchi.

Kwa kutazama malalamiko hayo, tunabaini kuwa uchafuzi wa mazingira nchini bado ni tatizo sugu, ndiyo maana ninashauri wakati mikakati ya kuifanya Tanzania kuwa nchi ya viwanda, tunapaswa kuangalia mahitaji ya sheria na namna ya kuwalinda watu dhidi ya madhara wanayoweza kupata kutokana na uharibifu wa mazingira.

Uchafuzi wa mazingira una athari nyingi, zinazoonekana na zisizoonekana kwa haraka. Unachangia ongezeko la umaskini kwa wananchi na magonjwa mbalimbali yakiwamo maradhi ya mfumo wa hewa na saratani ya mapafu.

Kutokana na tatizo hilo, Taifa kwa sasa linatumia fedha nyingi kushughulikia madhara hayo na huko tuendako linaweza kutumia fedha nyingi zaidi iwapo tahadhari haitafanyika kabla Tanzania ya viwanda haijashika kasi.

Wakati uwekezaji huo unazidi kuchagizwa, kuna haja ya kufanya tathmini kuona tulipotoka, tulipo ili tuweze kuingia Tanzania ya viwanda kwa tahadhari kubwa ya uchafuzi wa mazingira.

Hili likifanyika itasaidia kupunguza migogoro kati ya wawekezaji wa viwanda na wananchi kama ilivyo sasa katika maeneo mengi ambako wawekezaji wanaona Tanzania si mahali salama kutokana na kukiuka kwao taratibu za uhifadhi wa mazingira.

Hivi kasi yetu ya kwenda kwenye viwanda inatambua Tamko la Haki za Binadamu la mwaka 1948 na Haki za Kikatiba ambalo linabainisha kuwa maisha ya mwanadamu na makuzi yake yana uhusiano mkubwa na mazingira kwa kuwa anaishi humo na anahitaji maji safi na mazingira mazuri?

Kwa mantiki hiyo haki za kimazingira zinamhusu mwanadamu na hivyo kuanzisha viwanda kwa kasi bila kuangalia athari za mazingira ni sawa na kuwa na uchumi usioweza kutatua matatizo ya wananchi.

Hii ni kwa sababu baada ya muda, kama hali hii haitaangaliwa kwa kina, taifa litakuwa na watu wagonjwa wasioweza kuzalisha.

Tunapohimiza viwanda kila kona tunatakiwa kuweka angalizo la kuhakikisha vyanzo vya maji, bahari, mito na maziwa vinalindwa ili kuepusha madhara kwa wananchi.

Uwekezaji unaohimizwa sasa kwa kasi lazima uzingatie mahitaji ya sheria mbalimbali zilizopo kama Sheria ya Mazingira ya Mwaka 2004, Sheria ya ardhi ya mwaka 1999, Sheria ya ardhi ya vijiji ya mwaka 1999, Sheria ya Mipango miji ya mwaka 2007.

Pia Sheria ya Hifadhi za Taifa, Mamlaka ya Hifadhi ya Ngorongoro, Sheria ya Wanyamapori ya mwaka 2009, Sheria za Misitu ya mwaka 2002, Sheria ya Hifadhi za Bahari ya mwaka 1994 na Sheria ya Uvuvi ya mwaka 2003.

Nikitambua kuwa miradi mingi ya maendeleo na kiuchumi inachangia uharibifu mkubwa wa mazingira licha ya Sheria na kanuni zilizopo kwa maslahi ya wakubwa, ninasisitiza mahitaji ya kufanyika tathmini ya athari za kimazingira kwa kila mradi kabla ya kuanza.

Mwandishi ni mwandishi wa Mwananchi mkoani mara. 0787239480.     

-->