Sunday, November 19, 2017

Ubachela utakupendeza kama ukinywa pombe zinakimbilia mikononi

 

Kuna hii hadithi inasambaa wa kiasi fulani katika mitandao ya kijamii, sina uhakika kama ni ya ukweli au porojo tu lakini kuna nyakati chimbuko la vitu fulani huwa si umuhimu kuzidi faida zinazopatikana ndani yake.

Hadithi inamuhusu mwenzetu mmoja, ila yeye ana sifa ya ziada ya ulevi, tena ule wa kiwango cha juu kabisa. Yaani kama utaamua kulinganisha ulevi na mnada, basi yeye itambidi umfanye ‘Bilionea Dk Shika’ kwa sababu kila mnada ataibuka kidedea tu (huu ni mzaha).

Kuna siku jioni alikuwa anarejea nyumbani, yuko maji kama alivyokuwa jana na juzi yake. Alipoingia ndani akakuta mke na watoto wao wawili wamelala. Kama kawaida, akaanza fujo kwa kuwaamsha watoto, kisha alipofuatwa mama, ‘bila kosa lolote’ akaanza kushushiwa makonde mazito, na alipo ridhika akapanda kitandani kulala.

Inapotokea namna hiyo watoto hubaki na kibarua cha kumbembeleza mama na kama bahati siku hiyo, kabla mwenzetu usingizi wa pombe haujamchukua, alisikia maneno aliyokuwa akiyasema mtoto wake wa mwisho mwenye miaka mitano wakati anamtuliza mama yake.

Anamwambia; “Mama nyamaza. Nikiwa mkubwa, nikiwa Afande, nitampiga baba na mbunduki wangu nimuue.”

Ni sentensi yenye maneno kumi na mawili tu, lakini yenye uwezo wa kuyeyusha nguvu za kreti zima la bia, na hivyo ndivyo ilivyokuwa kwa mwenzetu. Alikuwa amelewa, lakini aliposikia damu yake mwenyewe ikiweka ahadi ya kumuua siku moja bia ziliondoka kichwani na kwa kutumia akili yake safi akagundua kuwa njia anayopitia haitamuacha salama — anahitaji kujitathimini.

Ukweli usiopingika ni kwamba wanaume wengi ni walevi na tunapenda pombe, lakini wengi wetu hazitupendi. Na ili kujua kama una kichwa cha pombe au la we tazama matendo yako ukishalewa.

Ukiona baada ya kunywa tu unayajua matusi yote hata ambayo bado hayajanza kutumika— basi elewa pombe hazikupendi. Na cha kufanya ni kuanza kufanya utafiti wa soda gani zitakufaa kati ya za machungwa au zabibu.

Au wewe ukiona ukishautwika tu unajihisi kama ‘Matumla’ fulani hivi, wala usipate kujiuliza maswali mara nane nane, wewe pombe hazikutaki, na una mawili ya kuchagua, kati ya kuachana na habari za ulevi au uanze mazoezi ya masumbwi ili labda siku moja ukapeperushe bendera ya Taifa kwenye nchi za watu huko kupitia ndondi za kulipwa.

Muhimu kukumbuka ni kwamba pombe zinatengenezwa sio kwa sababu wewe unywe, kisha uwageuze watu ‘mabegi ya kufanyia mazoezi’, hapana. Pombe zipo ili tunywe, tufurahi na tupate mawazo ya kuibadilisha dunia. Sijui ni kwa namna gani pombe inatoa mawazo ya kubadilisha dunia lakini ndiyo hivyo.

-->