UCHAMBUZI: Ubatizo wa moto ni hatari!

Anna Mghwira, Picha na Mtandao

Muktasari:

Kati ya misamiati tata iliyotumika ni pamoja na usemi wa Katibu Mkuu wake wa zamani, Yusufu Makamba kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho atawabatiza wanachama wake kwa moto.

Misemo, methali, vijembe na mbwembwe vimesikika katika Mkutano Mkuu wa Chama cha Mapinduzi hivi karibuni.

Kati ya misamiati tata iliyotumika ni pamoja na usemi wa Katibu Mkuu wake wa zamani, Yusufu Makamba kuwa mwenyekiti mpya wa chama hicho atawabatiza wanachama wake kwa moto.

Kinyume na utaratibu tuliouzoea wa kuachiana kijiti cha uenyekiti kila awamu, mwaka huu haikuwa yakini kama kijiti kitapita salama bila kukwama. Kulikuwa na minon’gono ya kijiti kukwepeshwa ama kukataliwa kuachiwa. Kulikuwepo shaka ambayo inaonekana ilidhibitiwa.

Pili ni kuwa licha ya kuwa huu ulikuwa mkutano wa ndani, kiuhalisia ulibeba sura kubwa ya nje zaidi. Ilikuwa kama mkutano wa hadhara wa kunanga mahasimu.

Maneno huumba. Kauli ya mzee Makamba inaweza kukiangamiza chama hiki kikongwe kilichobakia Afrika. Mzee Makamba alitumia mifano ya Kibiblia kuelezea nafikiri alichomaanisha kuusifu uongozi mpya katika chama hicho, kwa kutumia mifano migumu na yenye unabii ama matarajio hasi.

Kwanza si kweli kuwa Rais mstaafu aliibatiza CCM kwa maji kwa maana ya kuandaa mazingira ya Rais ajaye kufuata. Hatujafikia ukomavu huo wa kisiasa katika kuandaa viongozi. Tangu uongozi wa awamu ya kwanza, Tanzania chini ya mfumo wa chama kimoja na chini ya mfumo wa vyama vingi, hatujawa na utaratibu wa kuandaa viongozi.

Wagombea wa nafasi mbalimbali hutokea tu kwa ridhaa yao wenyewe na kujitangaza, kisha kuchambuliwa na kupitishwa ama kukataliwa. Ndani ya CCM viongozi waandamizi takribani wote wanajinasibu kama marais ama marais watarajiwa!

Hakuna maandalizi isipokuwa kupitia utaratibu wa kura, yaani wagombea wengi kujitokeza na kujiandaa kuongoza wakati wa kampeni. Dhana ya utakatifu wa Ikulu na nani miongoni mwetu aende huko iko mbali sana. Siasa zetu bado ni za kuviziana, kutegeana na kunyemeleana ili ukimbahatisha mwenzako ummalize kabla yeye hajakuwahi.

Ni kama mchezo wa polisi na majambazi: kuwahiana, kuviziana, kunyemeleana. Hii ipo hata ndani ya vyama na katika nafsi za juu serikalini. CCM licha ya kushika uongozi tangu uhuru hakijaonyesha ukomavu wa kiutashi licha ya kufuata utaratibu wa kitaifa wa kupeana kijiti kwa kila anayetangazwa mshindi kushika nafasi ya urais hasa kwa kipindi kinachofuata.

Kigezo cha kutimiza wajibu peke yake hakitoshi kutupa taswira ya aina ya vyama vinavyoweza kuiletea nchi maendeleo. Kwa upande mwingine, kama chama kisingempitisha mwenyekiti mpya, maana yake kingeingia ukurasa mpya wa kutenganisha serikali na chama.

Hapo inawezekana tungeanza kuona tofauti za kiutendaji kama Mwenyekiti na Rais wangefanikiwa kuwajibishana ndani ya taasisi ya chama na ndani ya taasisi ya serikali.

ACT – Wazalendo inafuata mfumo huu na ijapokuwa wengi wanatilia shaka, uhalisia wake tumeona kipindi cha mpito tangu tumalize uchaguzi mkuu ambao Rais hakuwa mwenyekiti wa chama.

Tofauti ya CCM na ACT hata hivyo ni kuwa mwenyekiti wa CCM hakuonekana kutimiza majukumu yake kichama kwa uwazi sana licha ya hotuba ndefu aliyotoa akikabihi ofisi rasmi.

Kitendo cha mgombea kutokuwa na mpinzani ni dalili kuwa chama hiki kinajinasibu kuwa chama dola, si chama cha kufanya siasa, kueleza na kushawishi kupata wanachama. Vyama vilivyoleta uhuru barani Afrika vingi viliendeshwa kwa mfumo wa kidola, si kichama.

Ukuu wa chama unategemea dola: polisi na jeshi kupitisha mambo yake. Mfumo na utendaji wa chama unashawishi mazingira ya kufanyiwa ubatizo wa moto aliousema mzee Makamba.

Kama bado duniani kuna laana basi mzee Makamba ameilaani CCM kuwa ni chama kisichobadilika, kisichoumbika na kinachostahili kutupwa katika ziwa la moto kiangamie milele ili kitu kipya kizaliwe kuendeleza harakati za kisiasa. Ndiyo maana halisi ya ubatizo wa moto.!

Kuna aina tatu kuu za ubatizo katika Ukristo: Kuna ubatizo wa maji, wa Roho Mtakatifu na wa moto. Aina zingine za ubatizo ambazo hazitumiki sana ni pamoja na ubatizo wa damu na ubatizo wa matamanio. Kila ubatizo hutumika mahali husika.

Maaana halisi ya kubatizwa ni kuingizwa katika kundi kwa kuzamishwa. Unaweza kuzamishwa kwa maji halisi ama kwa roho na ama kwa moto.

Ubatizo wa maji ulifanywa na Yohana mbatizaji aliyemtangulia Yesu kwa kutumwa kuwaandaa watu kumpokea masihi. Kama tunakubaliana kuwa sisi hatufanyi maandalizi ya viongozi, basi hatuna haja ya kuzungumza wala kuongeza.

Ubatizo wa roho ni hatua inayofuata baada ya ubatizo wa maji na hasa kwa kuwa mara nyingi ubatizo huu hufanyika kwa watoto wachanga. Kadiri wanavyokuwa na kufundishwa kupata karama za Roho ndivyo wanavyozama pole pole katika ubatizo wa Roho. Na ndipo ubatizo huu hujidhihirisha kupitia matendo na maneno ama mfumo wa maisha na utumishi wa mtu. Roho mtakatifu huonekana kwa mtu aliyetubu, na kuishi kiimani na kudumu katika toba.

Mfalme Daudi aliyefahamika kama rafiki wa Mungu alisemekana kuwa mnyenyekevu aliyetambua makosa yake haraka sana na kujirekebisha kila alipokosea. Kama tunakuwa kama Daudi maana yake tunaepuka ubatizo wa moto. Tunaepuka hasira ya Mungu. Roho huongoza.

Kinyume na ubatizo wa roho, ubatizo wa moto ni kwa ajili ya wale walioshindikana, masugu wa dhambi na makosa! Hawa hutupwa katika ziwa la moto. Kwa maneno haya mzee Makamba alikuwa anaiambia CCM wasiofuata taratibu za chama watachomwa na moto wa Magufuli!

Maana yake wataangamizwa, hawatabaki. Hawatabakizwa. Magufuli mwenyewe pia amekiri kuwa yeye si mstahimilivu kama mtangulizi wake.