Ubaya sio kulazimisha muziki mbaya, bali kuua vipaji hali si kwa sababu za kibiashara

Muktasari:

  • Au kuna nyimbo ambazo umeshawahi kuzisikia mara chache na kukubali kuwa ni nzuri lakini zikapotelea kusikokujulikana.

Hebu jiulize ni mara ngapi umeusikia wimbo kwa mara ya kwanza na kujisemea moyoni ‘aaah wa kawaida sana au mbaya ‘ lakini baada ya kuusikia mara nyingi unajikuta unaanza ‘kuukubali’.

Au kuna nyimbo ambazo umeshawahi kuzisikia mara chache na kukubali kuwa ni nzuri lakini zikapotelea kusikokujulikana.

Yaani kuna wimbo ulipousikia mara ya kwanza au kuuona kwenye runinga ukajisemea ‘huu lazima utabamba’, ‘huu utachukua tuzo mwaka huu’, lakini hujawahi kusikia hata umeingia kwenye 50 bora zozote.

Ushauri wa bure ni kwamba unapousikia wimbo mzuri ununue ‘usidownload’ kwa kuwa utakuwa umemuibia huyo msanii. Ukishafanya hivyo utunze na ikibidi tengeneza chati na zako mwenyewe kwa kuwa sikio lako au jicho haliamui kazi bora.

Soko la muziki ndilo linaloamua wimbo upi utakuwa bora ndiyo maana kwenye kumi bora za nyimbo utawakuta wasanii walewale kila siku. Utajiuliza hivi kigezo cha wimbo kufanya vizuri ni kipi lakini wakati huohuo ukizipenda nyimbo unazosikiliza.Suala la kuzipenda nyimbo unazozisikia lipo Kisayansi. Yaani sehemu fulani ya ubongo ambayo iliamini wimbo unaousikiliza ni mbaya, huanza kulainika taratibu na kuanza kuupenda mara baada ya kuusikia mara nyingi.

Hata mtekaji anaweza kumpenda mateka wake anapokaa naye muda mrefu kwa kuwa sehemu hii ya ubongo huanza kuona mazuri ya mtu huyo.

Walioshikilia soko la muziki wanatumia udhaifu huu wa kibinadamu kuwafanya watu wapende wanachoamua kutaka kuwasikilizisha au kukiuza. Muziki ni biashara hivyo siwashangai wanaofanya hivi hata kidogo.

Kwenye masoko ipo dhana imejengeka kwa jamii kuwa tasnia hiyo huwalazimisha watu kununua vitu wasivyovitaka kwa kufanya matangazo mara nyingi zaidi, vivyo hivyo kwenye burudani.

Siyo mbaya kuupenda muziki mbaya au kuwanufaisha wasanii wasio na vipaji, ubaya ni kuua vipaji kwa sababu za kibiashara.

Kwa sababu majukwaa ni mengi, basi hawa wenye vipaji waungwe mkono kwa kununua kazi zao au kuzitazama katika mitandao ambayo mwisho wa siku itawalipa.

Kuzinyonya nyimbo, kuziweka katika blogs ni namna nyingine ya kuwaibia. Hakuna tofauti kati ya anayewabania na anayewaibia kwa sababu wote wanawanyonya.