ANETH MAKERE : Ubunifu wa vito vya thamani utamvusha mwanamke

Aneth Makere

Muktasari:

  • Hivi sasa ameanzaa kutumia maarifa anayoyapata kuwa mjasiriamali akiwa bado yupo masomoni jambo linalomfanya aanze kuona mafanikio ya kile anachokisomea.

Ni binti wa miaka 20. Huyu siyo mwingine bali Aneth Makere mwanafunzi wa Programu ya Ukataji Madini na Utengenezaji Vito vya Thamani (Lapidary and Jewelry Technology) katika Chuo cha Ufundi Arusha (ATC).

Hivi sasa ameanzaa kutumia maarifa anayoyapata kuwa mjasiriamali akiwa bado yupo masomoni jambo linalomfanya aanze kuona mafanikio ya kile anachokisomea.

Anasema amekua akipenda ubunifu tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi kutokana na kumwona dada yake, Maria Makere ambaye ana ofisi ya ushonaji wa nguo za wanawake.

“Unajua sisi wanawake tunapenda kupendeza kwa namna mbalimbali, viwalo vinavyotengenezwa kutokana na madini ya aina mbalimbali vitu vya asili ni sehemu muhimu ambayo naiona haijatumika ipasavyo katika tasnia ya urembo ukizingatia nchi yetu imejaa rasilimali,” anasema Aneth.

Mjasiriamali huyo anayechipukia anasema mafanikio yake katika siku za usoni yatatokana na uwepo wa soko la uhakika linalotokana na vitu vya asili na madini ya aina mbalimbali yaliyoongezwa thamani kupitia taaluma aliyoipata katika Chuo hicho ambayo bado inahitaji wataalamu wengi.

Akizungumzia uamuzi wake wa kuanza ujasiriamali akiwa bado masomoni anasema, umetokana na kuhudhuria semina ambayo ilikua ikizungumzia namna ya kubuni na kuanzisha biashara ambayo anaamini imebadili maisha yake kwa ujumla.

“Semina niliyoipata sikuichukulia kikawaida bali niliona ni fursa kwangu ambayo itaniwezesha kupambana na changomoto zilizoko mbele yangu hadi nifanikiwe kuwa mfanyabiashara mkubwa, nikiwa na kampuni yangu itakayotumia rasilimali zetu kuziongezea thamani na kunufaika nazo kikamilifu, badala ya kuwa tegemezi wa bidhaa za urembo kutoka nchi nyingine,” anasema.

Anasema aliona aanze mapema ujasiriamali kutokana na sababu mbalimbali zikiwemo kutumia elimu ya ujasiriamali kwa vitendo, badala kubaki nayo kama nadharia pekee na ikiwa ni njia sahihi ya kujifunza kutokana na makosa ambayo yanaweza kujitokeza ili liwe somo la kuhakikisha unadumu kwenye mafanikio siku zote na anaeleza kuwa siyo lazima uwe na umri mkubwa ndiyo uanze ujasiriamali.

Mtaji ulivyopatikana

“Nilishauriana na wenzangu tunaosoma kozi hii namna ya vitendea kazi tunayojifunzia kwa vitendo na wenzangu wanne wakaona ni jambo jema tukaanzisha kikundi tunachokiita ‘M Power 4 Company’.

Tumekiita kikundi chetu jina hilo kutokana na majina ya wazazi wetu kuanza na herufi ‘M’ ikiwa imetokea kwa bahati tu,” anasema Aneth.

Anasema baada ya kuafikiana walipeleka maombi ya fedha kwenye uongozi wa idara husika, lakini kwa kuwa haikuwa kwenye bajeti ya idara wala chuo, walipata michango ya hiari ambayo ilifikia kiasi cha Sh140,000 ambazo wamezitumia kununulia vifaa vya urembo kwa wanawake.

Hata hivyo, hakuwa tayari kusema mtaji wao umekua kwa kiwango gani na kudai hizo ni siri za kikundi.

Anasema moja ya changamoto anayokabiliana nayo ni ya muda wa kuwa darasani na kuhakikisha yeye na wenzake wanakamilisha oda za wateja wao kwa wakati.

Binti huyu anatoa wito kwa wasichana wenzake kujitokeza na kuonyesha vipawa vyao na kuvifanyia kazi ili viwasaidie katika maisha yao badala ya kukaa tu wakisubiri ajira, ambazo zimekua changamoto duniani kote.

Amewataka kuacha kasumba ya kuchagua kazi fulani tu bali waone ni namna gani wanaweza kutumia elimu na rasilimali zilizopo kujiletea maendeleo.

Ameendelea kusema kuwa kwa kuwa chuo hicho kinatoa mafunzo kwa vijana wengi, kuna umuhimu wa Serikali kwa ujumla kuona sababu ya kutenga fedha kwaajili ya wanafunzi watakaonyesha ubunifu.