Uchaguzi mdogo na mlolongo wa malalamiko

Muktasari:

  • Uchaguzi huo ulifanyika baada ya wabunge wa majimbo hayo, Maulid Mtulia - CUF Kinondoni na Dk Godwin Mollel aliyekuwa Chadema, kujitoa na kujiunga na CCM mwishoni mwa mwaka jana.

Uchaguzi mdogo katika majimbo ya Kinondoni jijini Dar es Salaam na Hai mkoani Kilimanjaro umemalizika na CCM imeibuka na ushindi kwa kuyachukua majimbo yote mawili. Pia, ilinyakua kata zote tisa zilifanya uchaguzi huo Jumamosi.

Uchaguzi huo ulifanyika baada ya wabunge wa majimbo hayo, Maulid Mtulia - CUF Kinondoni na Dk Godwin Mollel aliyekuwa Chadema, kujitoa na kujiunga na CCM mwishoni mwa mwaka jana.

Katika uchaguzi mdogo uliotangulia Januari 13 katika majimbo ya Singida Kaskazini, Songea Mjini na Longido baadhi ya vyama vya siasa viliususia vikilalamikia unyanyaswajikubadili matokeo na mawakala kutimuliwa vituoni katika uchaguzi uliokuwa umetangulia Novemba katika kata 43.

Hata hivyo, safari hii vyama hivyo vilijitosa katika uchaguzi wa Kinondoni na Hai na hivyo kuufanya kuwa mgumu kutabirika kiushindani. Hata hivyo matarajio yao hayakufiwa badala yake wameishia kwenye mlolongo mpya wa malalamiko na sintofahamu zaidi.

Wakati wa kampeni

Kampeni za uchaguzi huo zilifunguliwa Januari 21, zikiambatana na matukio kadha wa kadha yaliyolalamikiwa na baadhi ya vyama vya siasa. Katika jimbo la Siha, CCM ililaumiwa kwa kumtumia Mkuu wa wilaya hiyo, Onesmo Buswelu kupanda jukwaani kumnadi Dk Mollel, jambo lililoelezwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuwa si sahihi.

Kama hiyo haitoshi, CCM iliendelea kuwatumia mawaziri ambao walitoa ahadi mbalimbali zikiwamo za kutekeleza majukumu yao ya kiserikali endapo wagombea wa chama hicho watachaguliwa.

Miongoni mwao ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), Seleman Jaffo, Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Waziri wa Mambo ya Ndani na wengineo. Pia Naibu Spika wa Bunge, Dk Tulia Ackson naye aliahidi Mtulia kumpa nafasi zaidi bungeni.

Viapo vya mawakala

Wakati kampeni zinaelekea ukingoni Februari 11 ambayo ilikuwa siku ya kuwatambulisha na kuwaapisha mawakala wa vyama vya siasa vilivyoshiriki uchaguzi huo, Chadema ililalamika kwamba mawakala wake katika jimbo la Kinondoni wamekataliwa kuapishwa.

INAENDELEA UK 20

INATOKA UK 17

Ilieleza kuwa katika Kata ya Hananasif, ofisa mtendaji aligoma kuwaapisha mawakala hao akiwataka waache majina yao hadi atakapowaita siku tatu kabla ya siku ya kupiga kura.

Baadaye ilidaiwa karibu watendaji wa kata zote walifanya hivyo katika jimbo hilo na chama hicho kupitia idara ya habari kilisema hakukuna sababu yoyote ya msingi iliyotolewa na wahusika.

Kama hiyo haitoshi, baadaye viongozi wa chama hicho wakiongozwa na Mwenyekiti Freeman Mbowe walifika makao makuu ya NEC kudai viapo vya mawakala wa chama hicho kwa jimbo la Kinondoni, ikiwa ni siku mbili kabla ya uchaguzi huo.

Ujumbe huo ulieleza sababu sita kwa NEC, zote ziliwa ni malalamiko; Mosi, mkurugenzi wa manispaa ya Kinondoni kukataa kuwaapisha mawakala wa ziada.

Pili, ni Msimamizi wa uchaguzi kukataa wabunge na madiwani wa Chadema kuwa mawakala; tatu, msimamizi huyo kuweka sharti jipya la kutaka mawakala wote wawe na vitambulisho; nne, kutotolewa kwa hati za viapo kwa mawakala; tano, kutofahamika kituo cha majumuisho ya kura na wasimamizi kuwa makada wa chama tawala na kuwapo uwezekano wa wao kupiga kura mahali wanaposimamia.

Licha ya malalamiko hayo kupata majibu ya Tume siku moja kabla ya uchaguzi, Chadema haikuridhika kwa kuwa viapo na barua za kuwatambulisha mawakala havikutolewa hadi muda wa kazi unakwisha siku moja kabla ya uchaguzi.

Maandamano

Akizungumza baada ya mkutano wa kufunga kampeni katika uwanja wa Buibui kata ya Mwananyamala, Mbowe aliwaongoza wafuasi wa chama hicho kwenda kudai viapo hivyo kwenye ofisi msimamizi wa uchaguzi kwa maandamano yaliyosambaratishwa na polisi na kusababisha kifo cha kifo cha Akwilina Akwiline aliyekuwa mwanafunzi wa Chuo cha Taifa cha usafirishaji (NIT) akiwa ndani ya daladala.

Pia, wakati kampeni zikiendelea, Chadema ilitangaza kumpoteza aliyekuwa wake katibu wa kata ya Hananasif, Daniel John ambaye mwili wake ulipatikana akiwa ameuawa huku aliyekuwa naye, Reginald Malya akikutwa ufukweni mwa bahari ya Hindi akiwa na majeraha.

Ofisi ya Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam ilisema wanaendelea na uchunguzi ili kuwabaini watu waliohusika na kifo hicho, huku askari sita wakiwa wametiwa mbaroni.

Siku ya uchaguzi

Siku ya uchaguzi Februari 17, vituo vilifunguliwa saa 1:00 asubuhi. Hata hivyo, mawakala wa vyama vya upinzani walikataliwa katika baadhi ya vituo kwa kukosa barua za utambulisho.

Katika vituo vingi, hasa Kinondoni walikataliwa kuingia kwenye vituo kwa zaidi ya saa sita, huku mawakala wa CCM na vyama vingine wakiwa ndani ya vyumba vya kupigia kura.

Jambo hilo liliwakasirisha viongozi wa Chadema na Mkurugenzi wa operesheni, Benson Kigaila alidai zilikuwa njama za kupora ushindi wao kwa kuwazuia mawakala kuwapo vituoni.

“Hizi ni njama kwa sababu tumelalamika kwa muda mrefu bila mafanikio. Tulikwenda makao makuu ya NEC tukawaeleza hawakushughulikia, jana (Februari 16 tumekwenda kudai barua kwa mkurugenzi wa uchaguzi hatukupewa,” alisema Kigaila na kuongeza:

“Mimi mwenyewe nimemfuatilia mkurugenzi hadi saa 5 usiku akasema barua ziko kwa wasimamizi wa vituo Biafra. Tulipofika huko wasimamizi walisema hawajapewa barua.”

Kigaila alisema baadhi ya mawakala wao wamepewa barua saa 2 asubuhi licha ya kufika vituoni saa 11 alfajiri. Hata hivyo alisema licha ya kupewa barua, wasimamizi walizikataa wakisema zimeghushiwa saini.

Hata hivyo, madai hayo yalikanushwa na Msimamizi wa Uchaguzi, Aaron Kagulumjuli akisema viongozi wa vyama ndiyo walichelewa kuchukua viapo na barua za utambulisho.

Hata hivyo, Kagulumjuli baadaye alisema wingi wa mawakala ndiyo umemsababisha kuchelewesha barua.

“Tuliwaambia viongozi wa vyama waje wachukue, baadhi hawakuja wengine walikuja na wengine wamekuja saa 11 na saa 12, kwa hiyo kutokana na idadi kubwa ya mawakala nilionao, lazima nichelewe kuwagawia zile barua. Kwa hiyo ni tatizo la viongozi wa vyama,” alisema Kagurumjuli.

Akizungumzia suala la baadhi ya mawakala kutolewa kwenye vituo vya kupigia kura, Kagurumjuli alikiri akiwataka mawakala hao kuwafuata viongozi wao.

“Inawezekana kweli wamezuiwa kama hawana barua za utambulisho, ni wajibu wa mawakala kuwafuata viongozi wao wawape barua za utambulisho kwa sababu wao ndiyo waliopewa ili wawapatie. Msimamizi wa kituo hawajui mawakala. Kama kiongozi hajampa basi ni mpango wa kiongozi huyo ambayo haituhusu sisi kabisa.”

Sanduku kuibwa

Madai mengine ambayo yamebaki mjadala bila uthibitisho ni la kituo cha kupigia kura kwenye eneo la Magomeni, mtaa wa Idrisa, ambako wananchi walisema sanduku la kura lilichukuliwa katika kituo hicho na mtu asiyejulikana wakati upigaji kura ukiendelea.

Wakala wa chama cha SAU, Edmund Mato aliyekuwa katika kituo hicho alisema lilikuja gari na kuegeshwa karibu na kituo hicho na ndipo mtu mmoja alikuja na kuondoka na sanduku mbele ya wasimamizi na askari polisi.

“Sisi tumekaa hapa na tulikuwa hatujasinzia, wametoka watu, gari lilikuwa pale, jamaa amechukua kachukua lile box kaondoka nalo.

“Ameenda nalo hivi, wakati Polisi wanahangaika kwanini limechukuliwa, baada ya muda kadhaa box ndiyo limerudishwa, wanadai tuendelee na uchaguzi na box limefungwa vilevile, hatujui huko wamelifanyia nini,” alisema Mato.

Hali hiyo imelalamikiwa na Mkurugenzi wa mawasiliano wa CUF (Lipumba), Abdul Kambaya akisema uchaguzi huo umepoteza sifa.

Aliyekuwa mgombea wa jimbo hilo kupitia Chadema, Salum Mwalimu alifika katika kituo hicho na kuwahoji wasimamizi kwa kuruhusu uchaguzi kuendelea katika hali hiyo, akakamatwa yeye na kupelekwa kituo cha Polisi Magomeni, kisha kuachia baada ya kitambo.

Polisi baadaye walikanusha kumkamata wakisema alijipeleka mwenyewe.

Msimamizi wa uchaguzi, Kagurumjuli alisema hana taarifa ya tukio hilo.

Makada wa CCM

Licha ya Mkurugenzi wa uchaguzi wa NEC, Kailima Ramadhani kufafanua hivi karibuni utaratibu wa kuwapata wasimamizi wa vituo vya kupigia kura, taarifa zilizotolewa kwenye mitandao ya jamii zimewaonyesha baadhi ya wasimamizi wa vituo kuwa makada wa CCM.

Picha zilizotumwa kwenye mitandao ya jamii zimewaonyesha wasimamizi hao wakiwa wamevalia sare za CCM na wengine wakitajwa kusimamia kampeni za chama hicho.

Akifafanua utaratibu wa kuwapata wasimamizi, Kailima alisema taratibu zote za kuwapata wasimamizi hao zilifuatwa ikiwa pamoja na kutangaza nafasi za kazi na waliohitaji kuchujwa kwa kuangalia sifa zao na majina ya walioteuliwa kubandikwa kwenye mbao za matangazo katika kata 10 za jimbo la Kinondoni.

Wengi hawakupiga kura

Kulingana na matokeo yaliyotangazwa watu waliojiandikisha walikuwa 264,055, lakini waliopiga kura ni 45,454 na kura zilizoharibika ni 587, hivyo kura halali ni 44,867. Kwa hiyo waliopiga kura ni asilimia 17.21 ya waliojiandikisha. Hivyo asilimia 82.79 hawakupiga kura.