Uchumi utakua wanawake wakimiliki, kuendesha biashara

Muktasari:

Wanafunzi wengi wameelezwa kukosa sifa za kupata mkopo wa Serikali kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) hivyo kutishia ndoto za maisha yao kitaaluma.

Wakati Serikali ikisisitiza kuhusu mpango wake wa kujenga uchumi wa viwanda na kukuza ajira, wapo wanaoona ni jambo lisilowezekana kutokana na yanayotokea kwenye mikopo ya wanafunzi wa elimu ya juu pamoja na sekta ya benki na fedha.

Wanafunzi wengi wameelezwa kukosa sifa za kupata mkopo wa Serikali kutoka Bodi ya Mikopo ya Elimu ya Juu (HESLB) hivyo kutishia ndoto za maisha yao kitaaluma.

Taarifa za robo ya tatu ya mwaka huu kwa sekta ya benki na fedha zilizonyesha taasisi kadhaa zikiwamo kongwe zikipata hasara kwa mara ya kwanza huku nyingine zikifilisika, ni machache kati ya mengi ambayo wasio na imani wanaona ni changamoto ya kuipata Tanzania ya viwanda.

Wakati hayo yote yakitokea, Veneranda Lupasyo, mama wa watoto watatu  na mfanyabiashara wa mboga katika Soko la Kigogo Sambusa, anakabiliana nayo na kuendesha maisha yake huku akiamini ipo siku atakuja kumiliki utajiri mkubwa.

“Biashara hii ni nzuri licha ya kwamba ina changamoto zake lakini naamini kama mtu unaifanya kwa moyo mmoja, ina kipato kizuri sana,” anasema Lupasyo.

Mama huyo mjane anasomesha watoto wake sekondari na mmoja Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut) bila msaada wa yeyote baada ya mumewe, Fredy Msyete kufariki dunia miaka mitano iliyopita.

Kabla mumewe hajafariki, anasema alimfungulia genge nyumbani kwake, Mburahati. Na alikuwa anauza vitu mchanganyiko lakini eneo hilo lina ushindani mkubwa kutokana na wingi wa magenge yaliyopo.

“Mume wangu alikuwa ananisaidia lakini baada ya kufariki mambo yalibadilika. Ilibidi nitafute mbadala wa kukabiliana na hali ngumu iliyokuwa imeanza kuninyelemea. Nilitafuta biashara itakayoniingizia kipato cha kumudu maisha, mimi na watoto wangu,” anasema.

Anasema  mwaka 2012 alipata meza sokoni hapo baada ya kuonana na uongozi wa na kuanzisha biashara ya kuuza mboga mchanganyiko akiwa na mtaji wa Sh200,000 ambao mpaka sasa ameukuza mpaka zaidi ya Sh35 milioni ndani ya miaka minne.

Wakati anaanza, anasema alikuwa akiuza zaidi mboga za majani lakini baada ya mtaji kukua, akaongeza kabeji, njegele na maharage mabichi (green beans), biashara ambayo anaendelea kuifanya hadi sasa.

Lupasyo anasema kwa sasa anaagiza mzigo mkubwa na kuuuza kwa wachuuzi. “Hivi sasa naishi maisha mazuri tofauti na mawazo niliyokuwa nayo muda mfupi baada ya kufiwa. Najimudu. Namsomesha mtoto mkubwa chuo kikuu kwa kulipa ada mwenyewe. Hapati mkopo wa Serikali, ninalipa kwa biashara hii.”

Ukatili wa kijinsia masokoni

Lupasyo anasema wanawake wengi hujikuta wakinyanyaswa wanapofanya biashara zao hasa kwenye masoko makubwa kutokana na kushindwa kutambua haki zao za msingi.

Hata hivyo, anasema yeye alipata ujasiri wa kukabiliana na hali hiyo baada ya kupata mafunzo yaliyotolewa na Shirika lisilo la Kiserikali la Kuwezesha Wanawake Kibiashara (EfG) Tanzania kwa ushirikiana na Chama cha Waandishi wa Habari Wanawake Tanzania (Tamwa), Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla) na Kituo cha Msaada wa Kisheria kwa Wanawake (Wlac) na kupendekeza mafunzo hayo yarudiwe katika masoko kwa ajili ya kutoa elimu juu ya ukatili wa kijinsia dhidi ya wanawake.

Shirika la EfG Tanzania, linawasaidia wafanyabiashara wasio katika sekta rasmi kuinua nafasi zao katika nyanja mbalimbali hasa kiuchumi. Shughuli za shirika hilo zinawalenga zaidi wanawake walioajiriwa au kujiajiri katika sekta zisizo rasmi, kwa kuwajengea uwezo wa kutambua fursa za masuala yanayohusu maisha yao, utawala na maendeleo ya kiuchumi na kijamii.

Hata hivyo, Lupasyo anasema Soko la Kigogo Sambusa kama yalivyo masoko mengine, lilikuwa linakabiliwa na kero hiyo lakini hivi sasa imepungua baada ya kupatiwa mafunzo hayo.

Lakini, anasema bado kuna viashiria vya ukatili kutokana na baadhi ya wanawake kutofikiwa na elimu inayotolewa.

“Binafsi napenda kuwashauri wanawake wenzangu hasa wafanyabiashara, wajitambue. Wafanye kazi kwa bidii, wasimamie haki zao na wajue namna bora ya kutunza fedha wanazozalisha ili wafikie malengo yao,” anasema Lupasyo.

Anasema kwa kuwa amefanya biashara hiyo kwa muda mrefu, ameamua kujiingiza kwenye kilimo cha mazao hayo ili aweze kupanua wigo wa biashara yake ndani na nje ya nchi.

“Nitapenda kujiendeleza zaidi kwa kusoma mambo yahusuyo biashara na masoko. Nakusudia pia kuwelimisha wanawake wenzangu ambao ni wafanyabiashara hapa sokoni kutambua haki zao na mbinu bora za ufanyaji biashara,” anasema Lupasyo.

Anasema wanawake wanaofanya biashara masokoni wanahitaji kujengewa uwezo wa kusimamia biashara na elimu ya kukabiliana na unyanyasi wa kijinsia ili waweze kujikomboa kiuchumi na kuendesha familia zao.

Wadau

Utafiti uliofanywa na Shirika la EfG kwa kushirikiana na Tamwa, unaonyesha asilimia 31.6 ya wanawake wanaofanya biashara sokoni walishawahi kudhalilishwa na asilimia 92.7 wamewahi kukumbwa na kebehi, kejeli na matusi. Imebainika kwamba udhalilishaji huo unachukuliwa kama jambo la kawaida.

Kutokana na imani hiyo, asilimia 97.9 hawakuripoti polisi, asilimia 78 hawakuripoti kwa mtu yeyote kama vile kiongozi wa soko. Hii, kwa mtazamo mwingine, inamaanisha wanawake wenyewe wanachangia kuendelea kwa matumizi ya lugha chafu sokoni.

Utafiti huo ulifanyika katika masoko 10 ya Halmashauri ya Manispaa ya Ilala; ambayo ni Buguruni, Kisutu, Ferry, Mchikichini, Ilala, Kibasila, Kigogo Sambusa, Kiwalani, Vingunguti na Tabata Muslim.

Hali hii inatoa changamoto kwa wanahabari na wadau wengine kutumia nafasi zao kuwezesha wanawake kufaidika na fursa zilizopo na kuleta maendeleo yanayozingatia usawa wa kijinsia.

Baadhi ya wanawake wanakata tamaa kutokana na kunyimwa haki za kupata elimu ya biashara na kumiliki rasilimali zenye thamani kubwa.

“Ufumbuzi utawezekana ikiwa kutakuwa na taarifa tenganifu za kijinsia zinazoainisha mwingiliano wa jinsia na kulingana na dhana na taratibu zinazozingatia wajibu, kanuni, uhalali na hali halisi ya mazingira yanayoizunguka jamii kama vile ardhi, miundombinu, elimu na ajira,’’ anasema Mwanasheria wa Tamwa, Suzan Charles.

Anasema Wizara ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), ina jukumu la kuwaendeleza wanawake waliopo katika sekta zisizo rasmi.

Wakili na Mkuu wa Idara ya Mafunzo ya WLAC, Magdalena Mlolele anazitaja sababu za vitendo vya ukatili katika jamii kuwa vinatokana na mila na desturi zilizopo, sheria kandamizi, ufanisi mdogo wa vyombo vya kusimamia na kuhudumia waathirika wa ukatili na kutokuwapo usawa baina ya wanawake na wanaume.

Anasema kuna umuhimu kwa wadau kuendelea kujengewa uelewa kuhusu madhara ya ukatili wa kijinsia kwa wanawake na kuhusu utekelezaji wa sheria za kusimamia haki zao kuepuka tatizo hilo. Katibu Mkuu wa Wizara ya Viwanda, Biashara na Uwekezaji, Dk Adelhelm Meru anasema wakati Serikali ikijenga uchumi wa viwanda na ikitekeleza mikakati ya kuifanya Tanzania inakuwa ya uchumi wa kati, wawekezaji na wafanyabiashara wanapaswa kuheshimu haki za binadamu na kuzingatia usawa wa kijinsia.

“Wanawake ni muhimu katika kukuza biashara na uchumi hivyo wanastahili kupewa nafasi sawa kwenye umiliki wa biashara au usimamizi wa kampuni. Tunahitaji kuwa na uchumi shirikishi ili kufikia malengo tuliyojiwekea,” anasema Dk Meru.