Ufanisi wa benki ni muhimu kufadhili miradi ya maendeleo

Muktasari:

  • Faida ya benki na biashara nyingine yoyote hupatikana baada ya gharama za uendeshaji kuwa ndogo zikilinganishwa na mapato. Kwa sekta hii, uwiano wa asilimia 60 unapendekezwa zaidi.
  • Benki yenye gharama zisizo za riba (non-interest expenses) ndogo zaidi zikilinganishwa na mapato yaliyopo, ndiyo yenye ufanisi mkubwa. Kadri gharama hizi zinavyokuwa ndogo, humaanisha ufanisi wake.

Wakati harakati za kuimarisha uchumi zikiendelea ni muhimu kuingalia sekta ya benki na fedha. Kwa kuangalia taarifa za robo ya nne ya mwaka 2016, yapo mengi yanayotoa picha ya sekta hii muhimu kufanikisha miradi binafsi na ya umma.

Faida ya benki na biashara nyingine yoyote hupatikana baada ya gharama za uendeshaji kuwa ndogo zikilinganishwa na mapato. Kwa sekta hii, uwiano wa asilimia 60 unapendekezwa zaidi.

Benki yenye gharama zisizo za riba (non-interest expenses) ndogo zaidi zikilinganishwa na mapato yaliyopo, ndiyo yenye ufanisi mkubwa. Kadri gharama hizi zinavyokuwa ndogo, humaanisha ufanisi wake.

Takwimu zilizopo zinaonyesha kuna benki 66 nchini ingawa si zote zimesajiliwa kwenye Soko la Hisa Dar es Salaam (DSE) au jingine lolote duniani. Kupata picha, tuangalie maeneo manne ambayo ni faida ya mtaji au return on equity (ROE), faida ya mikopo au net interest margin (NIM), kiasi cha mikopo isiyolipika au no-performing loans (NPL), na uwiano wa mikopo na amana za wateja.

Faida ya Mtaji (ROE)

Faida ya mtaji ni miongoni mwa vipimo muhimu vya ufanisi wa benki. Kwa sekta hii, wawekezaji huhitaji walau asilimia 10.

Kwa kipindi hicho; Stanbic ilipata asilimia 20.8 ikifuatiwa na Standard Chartered iliyokuwa na asilimia 17.7 na NMB asilimia 17.6. TIB Group ikipata hasara ya asilimia 18 wakati Barclays ilipata asilimia 2.6 huku CRDB ikipata asilimia sita. Kati ya benki sita zilizofanya vizuri, mbili pekee ndizo za nyumbani.

Licha ya benki hizo kubwa kwa mtaji, rasilimali na matawi; zipo ndogo zilifanya vizuri. Hizi zinajumuisha Akiba Commercial Bank iliyopata asilimia 31.7 ikifuatiwa na PBZ yenye asilimia 29.7 na Mkombozi asilimia 19.4.

Ecobank ilipata hasara ya asilimia 86 ikifuatiwa na Azania asilimia 32 na UBL asilimia hasi 20.

Faida ya Mikopo (NIM)

Benki na taasisi zote za fedha hujiendesha kwa kukopa kutoka kwenye vyanzo tofauti kwa gharama ndogo na kukopesha wateja wake kwa bei kubwa. Vyanzo hivi vinaweza kuwa BoT, taasisi za bima, mifuko ya hifadhi ya jamii, benki za nje au miongoni mwa benki zenyewe.

NIM ni tofauti kati ya riba inayolipwa na benki kutoka ilikokopa dhidi ya inayopokea kutoka kwa wateja iliowakopesha. Itakumbukwa, kuanzia Machi 6, BoT ilitangaza kushusha riba ya kuzikopesha benki za biashara nchini kutoka asilimia 16 hadi asilimia 12.

Katika kipimo hiki, Benki ya NMB iliongoza ikiwa asilimia 12.5 ikifuatiwa na Citibank asilimia 10.8 kisha CRDB na NBC zilizofungana kwa asilimia 10 kila moja. Stanbic ilipata faida ya asilimia 6.6, Benki M asilimia tano na Standard Chartered asilimia 4.4.

Benki ndogo zilikuwa TWB asilimia 91.5, Access asilimia 28.9 na Akiba iliyopata asilimia 19.8 wakati Equity ilipata asilimia 1.8 ikifuatiwa na Benki ya UBA iliyopata asilimia 1.1 na Benki ya Ushirika Kilimanjaro asilimia 0.09.

Mikopo Isiyolipika (NPL)

Mikopo inayotolewa na benki au taasisi yoyote ya fedha huhesabika isiyolipika iwapo mteja hatopeleka marejesho kuanzia siku 90. Ndiyo maana benki hujitahidi kutafuta wateja watakaomaliza marejesho yao kuepuka hili.

Hiki ni kipengele muhimu ambacho wawekezaji hukiangalia. Mara nyingi, hupendekezwa iwe chini ya asilimia moja ingawa BoT inaagiza mikopo isizidi asilimia tano.

Kwa kipimo hiki, DTB iliongoza ikiwa na asilimia 2.6, NMB ilifuata na asilimia tatu na Benki M asilimia 3.9. Benki ya Citibank ilikuwa na asilimia 4.3, Stanbic asilimia 4.6.

Hali ilikuwa tofauti TIB Group iliyokuwa na asilimia 31, CRDB asilimia 13, Barclays asilimia 12.3, Exim asilimia 9.5 huku NBC na Standard Chartered zikifungana kwa asilimia tisa kila moja.

Benki ndogo; UBL na Canara zilikuwa na asilimia sifuri za mikopo hii wakati Finca ilikuwa na asilimia 2.3 na Habib asilimia 2.7 wakati zaidi ya theluthi moja ya wateja TWB walishindwa kulipa mikopo yao, ilikuwa na asilimia 35 ikifuatiwa na Banc ABC asilimia 30 na Benki ya Ushirika Kilimanjaro asilimia 29. Kati ya benki zote zilizopo nchini, takwimu zinaonyesha ni 16 pekee kanuni ya asilimia tano zinazopendekezwa na BoT.

Uwiano wa mikopo na amana

Benki hupokea amana za wateja wenye ziada na kuwakopesha wenye uhitaji kwa riba. Hutoa riba ndogo kwa wanaoweka fedha na kutoza kubwa kwa wanaokopa ili zipate faida ya riba.

Uwiano huu huonyesha uwezo wa benki kulipa madeni yake na kutimiza mahitaji ya wateja inaowahudumia wakati wote. BoT inapendekeza uwiano huu usizidi asilimia 80 ili zinazobaki zitoshe kukidhi mahitaji ya wateja.

Ikizidi BoT huchukua hatua kuhakikisha marekebisho yanafanyika ili kuiepusha kuanguka. Twiga Bancorp ilishindwa kuzingatia kipengele hiki, pamoja na sababu nyingine za kufilisika kwake.

Kulingana na taarifa zilizochapishwa; Benki ya Serikali, TIB Group ilikuwa na asilimia sifuri, Citibank ilikuwa na uwiano wa asilimia 44.3 na Barclays asilimia 63.5.

Benki nyingine ni NBC asilimia 67.1 wakati Stanbic ilikuwa na asilimia 65.1. Zilizokuwa na uwiano mkubwa ni Benki M kwa asilimia 99.8, CRDB asilimia 83 na Standard Chartered asilimia 79.1.

Finca iliongoza taasisi ndogo zbaada ya kuwa na asilimia sifuri. Benki ya India ilikuwa na asilimia 45 wakati Benki ya Ushirika Kilimanjaro ilikuwa na asilimia 48 na Habib asilimia 50.4.

Benki ya Access ilikuwa na uwiano mkubwa zaidi baada ya kupata asilimia 112.8 na Equity asilimia 108 wakati Ecobank na Canara zilipata asilimia 106 kila moja.