Ufugaji ulivyomwezesha meremeta kumiliki hoteli

Muktasari:

  • Alianza kwa kufuga kuku wa nyama, akafuatia wa mayai na baadaye akaongeza kilimo cha matunda aina ya karakara (passion).
  • Sikuamini simulizi ya namna alivyofanikiwa kiuchumi hadi nilipothibitisha kwa baadhi ya wakazi wa Mafia ambao wamemtungia jina kwa kumwita ‘mbunge au tajiri mtoto’.

Ukibahatika kukutana Abdul Qadir Omary Meremeta (39), unaweza usiamini kama kijana huyo ndiye mmiliki wa hoteli za kitalii zinayofanya vizuri katika kisiwa cha Mafia mkoani Pwani.

Alianza kwa kufuga kuku wa nyama, akafuatia wa mayai na baadaye akaongeza kilimo cha matunda aina ya karakara (passion).

Sikuamini simulizi ya namna alivyofanikiwa kiuchumi hadi nilipothibitisha kwa baadhi ya wakazi wa Mafia ambao wamemtungia jina kwa kumwita ‘mbunge au tajiri mtoto’.

“Niliishi chini ya mti kwa zaidi ya mwaka mmoja, ili nibane bajeti wakati nikihangaika kutafuta maisha. Watu walidhani nimechanganyikiwa wakanicheka na kuniita kichaa, nashukuru siku hizi naitwa bosi,” anasema.

Ufugaji wa kuku ndio ambao umemuwezesha kutimiza doto zake kimaisha. Wewe unayesoma makala haya unasubiri?

Pamoja na hatua kubwa kiuchumi aliyofikia, Meremeta hajaacha ufugaji wa kuku ambao anadai kuwa umempa heshima kubwa katika kisiwa cha Mafia, na kwamba ataendelea kuuthamini kwani unalipa.

Anasema kwa sasa anamiliki kuku wa nyama 600 na wa mayai 300 ambao wanaendelea kumuongezea kipato kwa kuwa analo soko la uhakika.

“Hoteli zangu pia zinategemea zaidi kuku ninaowafuga mie mwenyewe, pia huwa nasambaza kwenye hoteli mbalimbali hapa mjini. Kuku mmoja huwa na kilo kuanzia mbili na nusu, sitarajii kuacha shughuli hii inanilipa,” anasema.

Pia anasema wageni wanaofikia katika hoteli hizo wanategemea kuku anaowafuga na bidhaa nyingine za mbogamboga kutoka shambani kwake.

Wazo la kufuga kuku

Waswahili wanasema hata mbuyu ulianza kama mchicha.

Meremeta alipata wazo la ufuagaji wa kuku baada ya kumaliza kidato cha sita na kushindwa kuendelea na masomo ya elimu ya juu.

“Nilijibana nikapata fedha kidogo ambazo nilizifanya mtaji, niliandaa banda dogo la kuku nikanunua vifaranga na kuanza kufuga” anasema.

Anasema aliwatunza kuku wake akifuata kanuni za ufugaji bora, hadi walipofikia hatua ya kuwauza.

Japo hali ya uchumi ilikuwa ngumu kwake, alimudu kutunza fedha zilizotokana na ufugaji wake.

Anasema hakutaka kuzitumia vibaya badala yake alihakikisha anazifanyia kazi zitokanazo na ufugaji.

Wakati huo akiendelea na ufugaji wa kuku alijikita pia kwenye biashara ya mafuta ya petroli na diseli.

Alipofikisha kuku 400 aliamua kutafuta wateja wa uhakika ili asipate hasara.

“Niligundua mgodini naweza kupata wateja, licha ya hali yangu mbaya nilifunga safari hadi kwa Mkuu wa Wilaya ya Mafia nikamuomba, anisaidie kuwabembeleza wawekezaji wa mafuta ili wanipe tenda ya kuwapelekea kuku,”anasema.

Ujasiri huo ulimfanya kiongozi huyo kukubali baada ya kujiridhisha kwamba kijana huyo ana uhakika na kuku alionao.

Alitakiwa kuhakikisha kuwa anapeleka kuku 100 kila baada ya wiki mbili huku kilo moja akiuza kwa Sh6, 000 wakati, kuku hao walikuwa na uzito kuanzia kilo mbili na nusu.

“Ilikuwa tenda ngumu kwangu lakini kwa sababu niliamua kutafuta maisha sikuonyesha kushindwa. Nilipambana, nikaweza kuvuna kuku 100,’’ anasema.

Baada ya mtaji kukua, akaamua kuanza biashara nyingine ya mafuta huku akilima matunda aina ya karakara

“Mafia tunauza mafuta ya kupima kwenye lita, nilipata eneo chini ya mti kwa ajili ya bishara ya mafuta hivyo niliuza mwenyewe. Nilianza kuishi chini ya mti, ili nisihangaike kupanga kwa gharama kubwa wakati bado nilihitaji fedha za kutosha,” anasema.

Maisha chini ya mti

Maiaka saba iliyopita aliamua kuishi chini ya mti akiamini kwamba ni njia pekee ya kupunguza matumizi.

Anasema faida ya kuishi chini ya mti ilikuwa ni kulinda mafuta aliyokuwa akiuzia chini ya mti, ambayo hakuwa na uwezo wa kuyahamisha kila siku.

“Sikuwahi kuogopa kuishi chini ya mti kwa sababu nilijua malengo yangu, sikuwa na nafasi ya kupumzika nililala saa mbili hadi tatu kwa siku,” anasema.

Kila alfajiri alihudumia kuku wake waliojengewa banda mbali na kwenye eneo alikokuwa anaishi, bustani na kurejea kwenye mti wake ambako alikuwa akiishi.

“Watu walinishangaa aina ya maisha yangu, sikujali kwa sababu tayari nilianza kuona faida,” anasema.

Wazo la kujenga hoteli

Miaka mitano iliyopita, alipata wazo la kujenga hoteli ya kitalii, hivyo akaamua kununua kiwanja kwa sababu wakati huo alikuwa na mtaji wa kutosha na tayari alishapata nyumba ya kuishi.

Meremeta anasema alianza ujenzi wa hoteli yake kwa kujenga vyumba viwili.

“Huwezi kuamini kama nilianza kupata wageni kwenye vyumba viwili nilivyojenga, kilichowavutia ni mazingira mazuri ya nje. Nilipanda maua na nikaanza kuitangaza,”anasema.

Pamoja na biashara hii mpya, katu hakuipa mgongo biashara kuu ya ufugaji wa kuku, kwani ndiyo iliyokuwa ikimwingizia kiasi kikubwa cha fedha.

Alipozidiwa na majukumu akalazimika kuajiri wafanyakazi kwa ajili ya kumsaidia ufugaji wa kuku na hoteli yake ambayo iliendelea kuongezeka.

“Hoteli za kitalii hazihitaji nyumba moja, hapa kwangu ni nimejenga chumba kimoja kimoja kilichojikamilisha,”anasema.

Mafanikio hayo yalimfanya aanze kuheshimika kwani alipofikisha vyumba vitano, wageni wengi walianza kumuamini na kufikia kwenye hoteli yake.

Anasema alikuwa akiwatoza fedha kidogo tofauti na hoteli nyingine za kitalii ambazo hutoza hadi dola 250 kwa siku.

Utafiti wa hoteli za kitalii uliofanywa kwenye kisiwa hivyo unaonyesha kuwa, hoteli yake ni kati ya zile zinazotoa huduma nzuri kwa watalii.

Tayari ameshanunua eneo la ufukwe ambalo anatarajia kujenga hoteli ya kisasa zaidi itakayokamilika Oktoba mwaka 2017.

Siri ya mafanikio

Anasema siri kubwa ya mafanikio yake ni kuwa na melengo na bidii katika kuyafikia.

“Usiangalie kuchekwa, tazama malengo yako na fanya kazi kwa bidii utafanikiwa tu,”anasema Meremeta mwenye hulka ya ucheshi.

Katika umri wake wa miaka 39, Meremeta sasa ni miongoni mwa watu wanaoheshimika kwa kuwa vinara wa fedha kisiwani hapo. Kilichomfikisha hapo si kingine bali ufugaji wa kuku.

Unasubiri hadi upate mkopo kutoka benki ili uanze kufuga? Kama Meremeta alianza na banda moja akauza mafuta chini ya mti, unashindwa nini?