Wednesday, October 25, 2017

Ugumu wa chama cha ACT- Wazalendo kusimama upya

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto

Kiongozi wa Chama cha ACT-Wazalendo, Zitto Kabwe akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki kuhusiana na mambo mbalimbali ya kitaifa. Kushoto kwake ni kaimu mwenyekiti wa chama hicho, Jeremiah Maganja. Picha ya Maktaba 

By Tausi Mbowe, Mwananchi tmbowe@mwananchi.co.tz

Bundi amezidi kukiandama Chama cha ACT- Wazalendo na safari hii aliyekuwa Katibu Mkuu mwanachama wa chama hicho, Samson Mwigamba pamoja na wanachama 10 wametangaza kujivua uanachama na kujiunga CCM.

Mwigamba ambaye ni mmoja wa waanzilishi wa chama hicho kilichosajiliwa rasmi mwaka 2014 mwishoni mwa wiki alitangaza na kujivua uanachama jijini Dar es Salaam.

Bundi huyo anaonekana kuzidi kukinyemelea chama hicho baada ya siku za hivi karibuni aliyekuwa mshauri wa chama, Profesa Kitila Mkumbo kutangaza kusitisha rasmi uanachama wake, ikiwa ni baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Katibu mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji.

Chama hicho kilichoanzishwa chini ya uenyekiti wa Kadawi Limbu kwa lengo la kuwa mbadala wa vyama vyote vya upinzani nchini kwa madai kwamba vilivyopo vimekosa demokrasia ya kweli, kauli ambayo inaonekana wazi kukisulubu chama hicho na sasa hali si shwari tena kwa upande wake.

Hata hivyo, tofauti na ilivyotarajiwa kwa chama hicho kutoa upinzani mkubwa kwa chama tawala na vyama vingine vya upinzani, hasa Chadema ambao wanachama wake wengi walitoka, kimejikuta kikipoteza makada wake wa kutumainiwa baada ya viongozi hao wakuu kujiuzulu nyadhifa na wengine kuachia kabisa uanachama.

Kwa sasa ni wazi chama hicho kinapita katika wakati mgumu na kiongozi wa ngazi za juu aliyeshiriki mchakato wa kuanzishwa kwake, Zitto Kabwe kujikuta anabaki mwenyewe.

Hata hivyo, kiongozi huyo anajipa moyo huku akisema kuwa kamati ya uongozi imejiridhisha na kwamba chama hicho bado kipo imara na kinasimamia misingi yake ikiwamo uzalendo na kupigania haki na demokrasia huku kikiongozwa na kaulimbiu ya utu na uadilifu.

Kwa nini wanaondoka

Akizungumzia hatua hiyo kiongozi huyo wa ACT Wazalendo anasema wanachama wanaoondoka katika chama hicho hawatoki kwa sababu ya kugombana na uongozi, bali wamepata fursa sehemu nyingine ambayo chama hakiwezi kuitoa.

Akizungumza baada ya Mwigamba na wenzake 10 kujiuzulu uanachama, anasema, “Sijawa Rais na siwezi kukuteua kuwa mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, sijawa Rais bado na siwezi kukuteua kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maji.

“Kuna mambo ambayo siwezi kuyafanya kama kiongozi wa chama au mwenyekiti na katibu mkuu hawawezi na chama hakiwezi. Fursa zilipokuja tuliwaruhusu waondoke, hatukuwakatalia na walivyoondoka hatukuwahi kuwarushia madongo kama chama.”

Zitto ambaye pia ni mbunge wa Kigoma Mjini anasema baada ya Profesa Kitila Mkumbo kuteuliwa kuwa katibu mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji, chama hicho kilimweleza kwa wadhifa wake hawezi kuwa mshauri wao na mwisho wa siku aliandika barua ya kujivua uanachama.

Kiongozi huyo anasema ACT Wazalendo ilishtushwa na kauli ya Mwigamba aliyedai kuwa chama hicho kimekiuka misingi yake na ndiyo sababu iliyomfanya ajivue uanachama.

Anasema baada ya kusikia kauli ya Mwigamba, kamati ya uongozi ilikutana juzi na kumuita mwanachama huyo wa zamani kutoa maelezo ya namna ambavyo chama hicho kinakiuka misingi yake, lakini hakutokea.

“Hii maana yake nini? Maana yake ni kwamba hana cha kutueleza. Hakuna kwenye chama chetu anayeondoka kwa ugomvi au Katiba ya chama inakiukwa, wenzetu wanaondoka kwa sababu wana fursa ya kulitumikia Taifa kwa namna nyingine ambayo ACT-Wazalendo hatuwezi kuwapa,” anasisitiza Zitto.

Katika ya mistari ya maelezo hayo, Kiongozi wa ACT- Wazalendo anasema hali hiyo haiwezi kuwa ndiyo mwisho wa chama hicho au kumomonyoka.

Badala yake anasema kitasonga mbele na kupata watu makini watakaofanya kazi za chama kwa weledi.     

       “Tunawatakia kila heri, lakini chama hakimomonyoki, mwaka jana mwezi kama huu mlikuwa mnamjua Ado Shaibu nyinyi? (katibu wa itikadi, uenezi na mawasiliano kwa umma ACT Wazalendo), niambieni kama mlikuwa mnamjua, lakini leo si mnamtafuta kwa nukuu. Tunaibua viongozi wenye uwezo na tutaendelea kuwaibua wengi zaidi, ndiyo kazi tunayoifanya.”

Hata hivyo, Zitto mbali na kutumia nafasi hiyo kuwashauri watu walioondoka kuacha kuwashawishi waliobaki ili nao waondoke, anajibu pia tuhuma zinazotolewa na baadhi ya watu kuwa chama hicho ni upande wa Serikali.

Anasema ACT-Wazalendo si jukwaa sahihi la kuisifia Serikali kama baadhi ya wanachama wao wanavyodhani bali wao wanaongozwa kwa misingi na taratibu walizojiwekea ikiwamo kuendelea kupambana na umaskini na hali ya maisha ya Watanzania.

Mwigamba agomea wito

Mwigamba anasema hakuona jambo jipya litakalojadiliwa dhidi yake katika kikao cha chama, kwani mengi aliyoyalalamikia alishatolea ufafanuzi katika barua yake ya kujiuzulu.

Mwigamba anasema jambo lingine lililomfanya kutohudhuria kikao hicho ni Kamati ya Uongozi hiyo kuwa na wajumbe 12 kutoka watano waliopo kwa mujibu wa Katiba ya ACT-Wazalendo.

Ibara ya 29 (25) kipengele cha (V1), kinaeleza kwamba Kiongozi wa ACT-Wazalendo na mamlaka ya kuwaalika wanachama wengi wenye mawazo maalumu kuhudhuria vikao vya chama kwa kushauriana na Katibu Mkuu na mwenyekiti.

“Cha kushangaza idadi ya wajumbe walioalikwa ilikuwa kubwa na wote walioitwa walikuwa upande wa Kiongozi wa Chama (Zitto Kabwe) na hawa wageni walipanga kunivua uanachama baada ya mahojiano,” anasema.

Pengine swali la kujiuliza ni je, vikao vya kamati ya uongozi na vingine vya juu vitafanikiwa kurejesha nguvu ya chama hicho iliyokuwepo awali?

Wachunguzi wa masuala ya siasa wanasema kuwa hali sasa kwa Zitto ni mbaya na kwamba asipokuwa makini chama hicho kinaweza kumfia mikononi kama ilivyotokea kwa vyama vingine vya upinzani ikiwamo TLP chini ya uenyekiti wake, Agustino Mrema.

Harakati za ACT-Wazalendo

Vuguvugu la uanzishwaji wa chama hicho linakwenda mbali hadi wakati Mwigamba, Zitto na Profesa Mkumbo walipotimuliwa uanachama Chadema kutokana na kuhusishwa na waraka uliotaka kumwandaa Zitto Kabwe kuwania uenyekiti wa chama hicho.

Mwigamba na Profesa Mkumbo walitimuliwa uanachama wakati Zitto alivuliwa nyadhifa zake zote zikiwamo za Naibu Katibu Mkuu na Naibu Kiongozi wa Upinzani Bungeni, ukisubiri kesi aliyokuwa amefungua mahakamani. Baada ya kesi kuamuliwa na Zitto kupoteza, naye alitimuiwa.

Mara baada ya viongozi hao kutimuliwa walianza harakati za kuanzisha chama kipya huku Mwigamba akitangulizwa katika kukisajili kisha akafuata Profesa Mkumbo. Muda mfupi baadaye Zitto Kabwe ambaye kwa muda mrefu alihuishwa na uasisi wa chama hicho alijiunga rasmi na chama hicho na kupewa kadi yenye namba 007194.

Mara baada ya kujiunga na chama hicho wanachama walimchangua Zitto kuwa kiongozi wa chama huku Anna Mghwira akichaguliwa kuwa mwenyekiti hadi alipoteuliwa na Rais kuwa mkuu wa mkoa.

Hatua hiyo ilikuja siku moja bada ya Zitto kutangaza kuachia ubunge na kuandika barua rasmi huku akiahidi kuendeleza mapambano ndani ya chama hicho.

Mara baada ya kupata usajili wa kudumu chama hicho kilishiriki katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 na kumsimamisha mwenyekiti wake Anna Mghwira aliyeibuka na kura 98,763 sawa na asilimia 0.65, nyuma ya Rais John Magufuli wa CCM aliyepata asilimia 8,882,935 (asilimia 58.46) na Edward Lowassa wa Chadema aliyeibuka 6,072,848 (asilimia 39.97).

Profesa Kitila

Mapema mwezi huu Profesa Mkumbo alitangaza kung’atuka rasmi uanachama wa ACT Wazalendo na kubaki raia wa kawaida.

Hatua ya Profesa Mkumbo aliyekuwa mshauri wa chama ilikuja miezi sita baada ya kuteuliwa na Rais John Magufuli kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji. Hata hivyo, Profesa Kitila alisema uzoefu wa miezi sita wa kutumikia nafasi yake serikalini umeonyesha ni vigumu kwake kuendelea na uanachama na kutekeleza majukumu yote mawili.

Mchange

Mwaka jana pia chama hicho kilishuhudia mwanachama mwingine Habibu Mchange akijiuzulu kwa kile alichodai ili kupata muda mwingi wa kusimamia shughuli zake za kijasiriamali.

Kabla ya kujiuzulu Machange alikuwa kiongozi mwandamizi wa chama hicho, kwa kuwa katibu wa Mipango na Mikakati na baadaye Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa katika sekretarieti ya chama hicho na mjumbe wa kamati kuu na mjumbe wa Halimashauri kuu ya chama hicho.

Hata hivyo, Machange alisema kuondoa kwake kushiriki katika siasa kusihesabiwe kama sehemu ya kukwamisha au kurudisha nyuma matarajio na au malengo ya chama hicho.

Anna Mghwira

Kiongozi mwingine ni Anna Mghwira ambaye alilazimika kukaa pembeni baada ya kuteuliwa kuwa Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro.

Mapema mwaka huu Rais John Magufuli alimteua Mghwira kushika wadhifa huo akitokea chama cha upinzani na uongozi wa chama hicho kumweka kando.

Akizungumzia hali hiyo, aliyewahi kuwa naibu waziri katika Serikali ya Awamu ya Pili, Njelu Kasaka anasema anaamini chama hicho kikijipanga kitaweza kusimama tena na kuendeleza harakati zake kama iliyokuwa awali.

“Unapoanzisha chama lazima uwe na malengo, makusudio na uwezo wa kuendesha hata kama wakijitoa wanachama wengi ili mradi chama kina katiba na taratibu zake zikifuatwa hakiwezi kufa.”

Anasema chama siyo cha mtu ni lazima kuwe na utaratibu na endapo wataondoka wengine wapande kwenye uongozi.

“Naamini wanayo nafasi ya kujipanga upya na kusimama, changamoto katika jambo lolote ni kawaida kinachotakiwa ni namna ya kutatua changamoto hizo,” anasisitiza.     

-->