Uhariri na ukiushi wa taratibu za kiuandishi katika fasihi

Muktasari:

  • Kazi kubwa ya mhariri wa matini ni kuhakikisha kuwa muswada anaoushughulikia unaeleweka kwa walengwa.
  • Kwa sababu hiyo, mara zote mhariri huyo hujishughulisha na suala la kurekebisha lugha kwa mujibu wa kanuni mbalimbali kama vile zile zihusuzo uakifishaji, miundo ya sentensi, ufasaha wa lugha na kanuni nyinginezo.

Uhariri ni taaluma inayohusiana na kusoma, kusahihisha na kusanifu miswada ya makala, vitabu na kazi nyingine za kiuandishi kwa lengo la kuiweka katika hali bora ili iweze kuwasilisha ujumbe uliokusudiwa na mwandishi.

Kazi kubwa ya mhariri wa matini ni kuhakikisha kuwa muswada anaoushughulikia unaeleweka kwa walengwa.

Kwa sababu hiyo, mara zote mhariri huyo hujishughulisha na suala la kurekebisha lugha kwa mujibu wa kanuni mbalimbali kama vile zile zihusuzo uakifishaji, miundo ya sentensi, ufasaha wa lugha na kanuni nyinginezo.

Lengo la makala haya ni kuonesha udhaifu unaojitokeza katika baadhi ya kazi zinazohaririwa. Ikumbukwe kwamba, mhariri akishapokea muswada wa mteja wake anapaswa kuusoma wote, kuelewa muktadha wake na kuufanyia uhariri ipasavyo.

Hata hivyo, zipo kazi mahususi ambazo mhariri hana budi kuzishughulikia kwa umakini mkubwa. Mathalani, mhariri anaposhughulikia muswada wa kifasihi, anapaswa kuelewa kwa kina kusudio la mwandishi wa kazi hiyo.

Kuna malalamiko mengi ya waandishi yanayohusiana na kubanangwa kwa kazi zao za kifasihi. Hii inatokana na uhariri unaofanyika katika kazi hizo kushikilia kanuni bila kuangalia muktadha wa kazi hizo. Matokeo yake baadhi ya wahariri badala kujenga, wanabomoa.

Ikumbukwe kwamba katika uandishi wa kazi za kifasihi, mwandishi kulingana na lengo lake anaruhusiwa kukiuka baadhi ya kaida za kiuandishi ili kuijenga kazi hiyo kwa namna aonavyo inafaa.

Kwa mfano, kwa makusudi, mwandishi anaweza kutumia lugha isiyo fasaha na kukiuka kanuni za kiuandishi. Machoni mwa mhariri asiyejua mbinu hiyo, ataona kuwa ni kosa.

Kifasihi, ukiushi una dhima kubwa katika kuijenga kazi husika na kufanikisha lengo la mwandishi.

Kwa mfano, tukirejelea tamthiliya ya ‘Kinjeketile’ iliyoandikwa na Ebrahim Hussein na kuchapishwa mwaka 1969, kwa sehemu kubwa mwandishi huyu ametumia mbinu ya ukiushi wa kaida za lugha katika kazi hiyo.

Mathalani, katika sehemu ya kwanza, mwandishi amewachora wahusika Bi Kitunda na Bi Kinjeketile wakizungumza:

Bi Kitunda: Habali, Bi Kinjeketile?

Bi Kinjeketile: Nzuli, nzuli. Salama? (uk.1)

Ukichunguza majibizano hayo utabaini kasoro katika baadhi ya maneno. Herufi ‘l’ imetumika katika maneno ‘habali’ na ‘nzuli’. Sehemu zenye herufi ‘l’ katika maneno hayo, zilipaswa kuwa na herufi ‘r’ kwa kuzingatia msamiati fasaha wa Kiswahili. Hivyo, kwa ufasaha tungekuwa na maneno ‘habari’ na ‘nzuri’.

Mhariri asiyejua kusudio la ukiushi huo, atamrekebisha mwandishi na kumtaka atumie maneno ‘habari’ na ‘nzuri’. Kwa kufanya hivyo, mhariri atakuwa amebananga na kuharibu kusudio la msanii la kukiuka ufasaha wa maneno hayo.

Mwandishi ametumia ukiushi kwa makusudi kwa lengo la kuonesha kwamba wazungumzaji hao ni wa jamii ya Wamatumbi ambao herufi ‘r’ huitamka kama ‘l’.

Matumizi ya ukiushi huu huivutia hadhira na kuijengea imani kubwa kuhusu yale yanayotokea (ingawaje ni kazi tu ya kiubunifu). Hii inaonyesha pia kuwa, tamthiliya hii imeandikwa ikiwahusu watu wa jamii hiyo

Kwa sababu hiyo, wahariri wa kazi za kifasihi wanapaswa kuwa makini. Pamoja na kuzingatia kanuni za uhariri wa matini vilivyo, hawana budi kukumbuka kwamba katika muktadha fulani kazi hizo huwa na ukiushi ambao lazima uheshimiwe kwa kuwa una dhima kubwa katika ujenzi wa kazi hizo kisanaa.