ELIMU NA MALEZI : Uhusiano mwema ni muhimu kwa tabia ya mtoto

Muktasari:

  • ‘Hasikii. Jeuri asikwambie mtu. Usipomfanyia purukushani huwezi kumwambia kitu akasikia.’ Kwa mujibu wa maelezo yake, kuna nyakati hubidi amtishe, amwadhibu vikali na hata kumtukana ikibidi.

‘Mwanangu ni mtundu haijapata kutokea’ alilalamika msomaji mmoja wa safu hii. Sikuelewa ana maana gani aliposema mwanae ni mtundu. Nikaomba ufafanuzi.

‘Hasikii. Jeuri asikwambie mtu. Usipomfanyia purukushani huwezi kumwambia kitu akasikia.’ Kwa mujibu wa maelezo yake, kuna nyakati hubidi amtishe, amwadhibu vikali na hata kumtukana ikibidi.

‘Hao watoto unaowaongelea sio huyu wangu. Huyu ni mkorofi. Ukisema nimsikilize kama unavyoshauri ndio unaharibu. Akiona fimbo ndio kinaeleweka.’ Nilitamani kujua kama mbinu hizo anazotumia zimesaidia.

‘Kidogo. Nikimshikia fimbo ndio tunaelewana. Ukienda hivi hivi hana anachoelewa. Shida yake kubwa ni utukutu. Ni mwongo sijapata kuona.’

Mzazi huyu anawakilisha mtazamo wa wazazi wengi. Imejengeka imani kuwa watoto wanazaliwa na tabia zao. Wapo watoto kwa ‘asili’ ni wakorofi na watundu wakati wapo pia watoto wapole na wasikivu.

Ni dhahiri kuwa vinasaba vina mchango wake kwenye kuumba tabia zetu. Kama ambavyo huwezi kuamua kimo cha mwanao, huwezi pia kuamua mustakabali wa tabia fulani za mtoto kwa asilimia mia moja.

Tunafahamu, kwa mfano, kuna watu wana ukali usioelezeka. Pamoja na kulelewa kwenye familia yenye watu wapole, anaweza kutokea mtu mwenye hasira kali. Ukimgusa anawaka kwa ghadhabu. Katika mazingira kama haya, inaonekana upo uwezekano wa kurithi tabia fulani fulani.

Hata hivyo, watafiti wa tabia za mwanadamu wanakubaliana kuwa mazingira ya kimalezi anamokulia mtoto nayo yana mchango mkubwa katika kuchonga tabia zetu. Hata pale inapoonekana watoto wamerithi tabia kwa wazazi wao, kimsingi wanakuwa wanaakisi kile wanachokiona kwa wazazi wao.

Makala haya yanaangazia makundi manne ya tabia za watoto yanayotokana na mazingira ya kimalezi. Kimsingi, hoja ni kuwa hulka anazokuwanazo mzazi ndizo zinazochangia kutengeneza tabia ya mtoto. Lengo si kujenga hatia kwa wazazi bali kutusaidia kuelewa mchango wa yale anayoyafanya katika kujenga mustakabali wa mtoto kitabia.

Mtoto mtulivu mwenye uchangamfu

Huyu ni mtoto mwenye utulivu na kwa hakika anajiamini. Huwa ni mchangamfu kwa watu kwa sababu anapenda watu. Ukitaka kupima upendo wa mtoto huyu kwa watu, mpe kitu. Ni mwepesi kuwapa wenzake. Ingawa kuna umri fulani kila mtoto huwa na ubinafsi, mtoto wa kundi hili anapozidi miaka miwili, anakuwa mwepesi kuwapa watu kile alichonacho. Sababu ni kuwa anawaona wengine kuwa bora kama alivyo yeye.

Pia, hana ugomvi wala usumbufu. Tangu anapokuwa mdogo, huwezi kusikia akilia bila sababu. Hata pale anapolia ni rahisi kumtuliza. Kwa mfano, anapoachwa na mzazi wake, anaweza kulia kama watoto wa makundi mengine lakini ni mwepesi ‘kusahau’ na kuendelea kucheza. Mama anaporudi baadae, mtoto huyu humchangamkia.

Kwa ujumla, mtoto huyu ni matokeo ya malezi yanayomwelewa, yanayomshirikisha, yanayomkubali vile alivyo na yanayomweka karibu. Kisaikolojia tunasema mtoto huyu ana nafsi iliyotulia. Anajisikia kama mtu aliyeshiba asiye na njaa ya ‘kueleweka’, ‘kushirikishwa’ ‘kukubaliwa’ na ‘kupendwa.’

Mtoto mkimya ‘asiyependa’ watu

Huyu ni mtoto anayejiamini kama yule wa kundi la kwanza lakini ana tatizo la kujiona bora kuliko wengine. Kwa kawaida hana tabia ya ugomvi, lakini hupenda kujitenga na watu. Kinachomfanya apende kuwa ‘kivyake’ ni kutokuamini watu wengine wanaweza kuwa na msaada kwake. Ndani yake anajiona yuko sahihi, anajitosheleza na hahitaji sana msaada wa wengine.

Mara nyingi ni mkimya na hana maneno mengi sana, ingawa anaweza kuwa na uwezo mzuri kiakili wazazi wakimwelekea mazingira sisimushi.

Unaweza kumgundua mtoto wa kundi hili tangu akiwa mdogo. Hajali pale anapoachwa na mama yake. Anaweza kulia kama watoto wengine, lakini mama anaporudi, huwa haoenekani kujali.

Tabia hii ni matokeo ya mchanganyiko wa malezi yasiyojali (yanayopuuza) hisia zake lakini yenye kumshirikisha kwa namna fulani. Unapokuwa ukaribu fulani na watoto lakini huna tabia ya kuonyesha kuelewa hisia zake kwa hakika unamfanya mtoto aamini watu hawaelewi hisia zake.

Mtoto ‘mpenda watu’ asiyejiamini

Huyu ni mtoto anayependa watu kama mtoto wa kundi la kwanza. Tatizo lake ana hulka ya kuwaona wengine kuwa bora kuliko yeye. Anapenda sana michezo na kuwa na marafiki zake na wakati mwingine anakosa muda wa kufanya mambo ya msingi zaidi.

Mtoto wa namna hii anaweza kuonekana mpole anapokuwa na watu wasiomwelewa vyema, lakini anapokutana na watu wanaomwelewa, ni mchangamfu na mwongeaji kuliko kawaida. Kimsingi ni mtoto anayejisikia upweke ndani yake na anajaribu kufidia hisia za upweke ndani yake kwa kujichanganya na watu.

Huyu ni mtoto aliyeathirika na tabia ya utoro wa wazazi (wasiopatikana kimwili.) Kwa kawaida mzazi wake ni mtu mwenye upendo lakini muda mwingi hapatikani. Shauri kutokupatikana mtoto huamini mzazi wake hamjali ipasavyo ingawa anajua anapendwa. Uzungumzaji na kupenda watu unamsaidia kufidia hali ya kukosa uwepo wa mzazi.

Mtoto mkorofi na mgomvi

Huyu ni mtoto asiyejielewa. Hujiona hana thamani na wengine wanaomzunguka hawana maana pia kama alivyo yeye. Ni mtoto anayejidharau na kudharau wengine. Hana hisia na haelewi hisia za wengine na ndio sababu huwa mgomvi na mtundu.

Ukimchunguza mtoto huyu ni kama anafurahia kuwaona wengine wakiumia. Huwachokoza wengine na hata kuwatukana almuradi ajisikie ‘mbabe.’ Ni mchoyo hasa kama amekulia kwenye mazingira ya umasikini na huwa ni mbinafsi.

Kimsingi huyu ni mtoto anayelelewa kwenye mazingira ya mabavu na udhalilishaji. Mfano wazazi walevi wenye tabia ya kupigana na kutukanana mbele yake.

Aidha, wazazi wanaoishi na hasira na maumivu ndani yao wana nafasi kubwa ya kukuza watoto wenye tabia za kundi hili. Hawa huwatumia watoto kama namna ya kufidia maumivu waliyonayo. Mfano, mzazi ‘anayeugulia uchungu ndani yake’ hutukana na kutumia nguvu kubwa kuwaadhibu watoto bila yeye kung’amua anachokifanya.

Blogu: http://bwaya.blogspot.com