Friday, July 21, 2017

Ujauzito hushika kwa urahisi mwanaume akiwa na umri mdogo

Wanawake wa umri wa kati ya miaka 35 na 40

Wanawake wa umri wa kati ya miaka 35 na 40 wenye wenza wa chini ya miaka 30 ,walifanikiwa kushika ujauzito haraka.Picha ya mtandao 

By Mwandishi Wetu, Mwananchi

Inaaminika kuwa uwezo wa mwanamke kushika ujauzito hupungua kadri umri unavyosonga, lakini imegundulika njia inayoweza kutatua hili. Imeonekana kuwa mwanamke anaweza kuongeza uwezo wa kupata ujauzito kama mwenza wake atakuwa na umri mdogo.

Huko mitaani wanaitwa Serengeti Boys, Ben10 na majina mengine mengi kuonyesha umri wa wanaume hawa ni mdogo, lakini katika utafiti huu wanatajwa kuwa dawa kwa wanawake waliochelewa kupata watoto.

Utafiti huo uliofanywa na Chuo Kikuu cha Havard cha nchini Marekani uliwashirikisha wanawake 2,000 kati ya mwaka 2000 na 2014.

Ilionekana wanawake wenye wenza waliowazidi umri au kuwa sawa nao hawakufanikiwa kushika ujauzito kwa haraka tofauti na wale wenye wenza ‘Viserengeti Boy’.

Wanawake wa umri wa kati ya miaka 35 na 40 wenye wenza wa umri wa chini ya miaka 30, walifanikiwa kushika ujauzito haraka.

Katika utafiti huo pia ilionekana wanawake wa umri wa chini ya umri wa miaka 30 wenye wenza wa kuanzia miaka 40 kwenda juu hawakushika ujauzito kwa urahisi ukilinganisha na wale wenye wenza wa umri wa kati ya miaka 30 na 35.

Mbaya zaidi utafiti huo ulionyesha hakuna kinachoweza kufanyika kuzuia kuzeeka kwa mbegu za uzazi.

Watafiti hao walisema wanawake wana bahati kwani mbegu za uzazi za wanaume waliowazidi umri huyapa nguvu mpya mayai yao.

“Umri wa mwanamke unaweza kuwa tatizo, lakini dawa ni kuwa na mwanamume aliyemzidi umri kwani anakwenda kuyaamsha,” anasema Dk Gillian Lockwood mmoja kati ya watafiti.

Hata hivyo, utafiti huo unaonya kuwa matokeo hayo siyo ya kudumu kwa sababu kadri mwanamke anavyokuwa uwezo wake wa kushika ujauzito hupungua hivyo ni vyema akapata watoto katika umri usiozidi miaka 40.

Utafiti mwingine uliofanywa na Taasisi ya American Society for Reproductive Medicine (ASRM) ya nchini Marekani, umesema wanawake wanaopandikizwa ujauzito huwa na nafasi kubwa ya kufanikiwa ikiwa wenzi wao ni wadogo kiumri.

Utafiti huo ulifanywa kwa wanawake 613 wa umri kati ya miaka 40 na 46 umeonyesha wale waliokuwa na wenzi waliowazidi umri walilazimika kujaribu mara mbili au zaidi ili kushika ujauzito tofauti na wale wenye umri mdogo.

Wataalamu waliofanya utafiti huo wanasema mbegu za wanaume wenye umri mkubwa hazikuweza kuungana na mayai ya wanawake wenye umri wa kati ya miaka 40 na kuendelea.

Mwandishi wa kitabu cha The Male Biological Clock, Harry Fisch anasema sababu ya wanaume wenye umri mdogo ni kuwa huwa na mbegu nyingi na zinazokwenda kwa kasi ukilinganisha na yule mwenye umri mkubwa.

Anasema kadri umri unavyoongezeka wingi wa mbegu na kasi yake hupungua, lakini haimaanishi hawawezi kumpa ujauzito mwanamke.

“Kwa mwanamume mwenye umri mdogo ni rahisi kumdunga ujauzito mwanamke ukilinganisha na mwenye umri mkubwa, lakini naye anaweza iwe kwa kupandikiza au kwa njia ya kawaida,” anasema Dk FIsch.

Anasema mwanamume akishafikisha umri wa miaka 30, uzalishwaji wa homoni za testosterone hupungua kila mwaka na ndiyo kichocheo kinachosukuma mbegu kwenda kwa kasi.

“Kama testosterone zinapungua mwilini maana yake kasi na wingi wa mbegu hupungua pia, hali huwa hivyo kila mwanamume anapoongeza mwaka mwingine katika umri wake,” anafafanua.

Hata hivyo, utafiti wa taasisi ya ASRM unasema mwanamume mwenye umri mkubwa anaweza kuwa na nguvu sawa na kijana wa chini ya miaka 30 iwapo ataishi kwa kuzingatia misingi bora ya afya njema kama vile kutovuta sigara, kutokunywa pombe na kufanya mazoezi.

Umri sahihi wa kuzaa

Pamoja na utafiti huo kufanyika, wataalamu wa afya ya uzazi wanashauri mwanamke kuzaa kabla ya umri huo ili kuepuka madhara anayoweza kuyapata iwapo atachelewa.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake na Uzazi katika Hosipitali ya Taifa Muhimbili, Dk Cyril Massawe anasema hajauona utafiti huo na kwamba ataufanyia kazi ili kuona uwezekano.

Anasema kibaiolojia mwanamke anapaswa kuzaa mapema ili kujikinga yeye na mtoto kwa sababu madhara ya kuzaa katika umri mkubwa yanajulikana, hivyo pamoja na ushauri huu ukweli ubaki kuwa kama inawezekana mwanamke apate watoto katika umri sahihi.

Uwezo wa mwanamke kubeba ujauzito hupungua anapokuwa na umri wa kuanzia miaka 30 kuendelea juu na asilimia 11.5 ya wanaobeba ujauzito huharibika.

Pia, mwanamke anapochelewa kubeba ujauzito huweza kupata matatizo ikiwamo kuzaa mtoto aliye na kasoro za kimaumbile ikiwamo Down Syndrome ( watoto mfanano).

Wanawake wa umri wa miaka 40 na zaidi wanapobeba ujauzito kwa asilimia kubwa hujifungua watoto njiti. Pia, uzazi katika umri mkubwa huchangia kuzaa kwa operesheni kwa kuwa via vya uzazi huwa vimekomaa kiasi cha kushindwa kufunguka tena.

-->