Ujue ufugaji mseto wa samaki na wanyama

Mfano mzuri wa ufugaji mseto wa samaki pamoja na aina nyingine ya ndege na wanyama. Lakini mfugaji huyu pia anaendesha bustani jirani na bwawa

Muktasari:

FAIDA ZA MBOGA MBOGA 

Mboga mboga hutumika moja kwa moja kama chakula cha samaki kwa kuwa jamii ya samaki wengi wanaofugwa ni wale wanao kula majani kama jamii ya sato na perege na hata jamii ya kambale. Hivyo mabaki ya mboga mboga kutoka bustani hukatwa katwa vipande vidogo vidogo kwa ajili ya kulisha samaki.

Ufugaji mseto wa samaki ni ufugaji ambao bwawa la samaki linakuwa ndani ya shamba pamoja na shughuli nyingine za shamba

Shughuli hizi ni pamoja na kilimo cha mazao mbalimbali kama vile mbogamboga, mpunga na mengineyo. Ufugaji huo pia unaweza kujumuisha ule wa wanyama na ndege wanaoliwa.

Ufugaji samaki pamoja na shughuli nyingine za shamba, una faida mbalimbali ikiwamo  kuongeza ufanisi wa  mavuno,  matumizi mazuri ya  eneo  pembejeo pamoja na nguvu kazi.

Mambo ya kuzingatia

Kabla ya kuanza ufugaji mseto mkulima inabidi ajiulize maswali kama ni kiasi gani anataka kuwekeza katika mradi. Ni kiasi gani cha fedha pamoja na nguvu kazi atakavyotumia kutoa huduma kwenye mabwawa ukilinganisha na shughuli zingine za shamba?

Pia ajiulize kwanini anafuga samaki? Je, ni kwa ajili ya kuongeza upatikanaji wa samaki kama kitoweo nyumbani au kipato au anafuga kwa sababu jirani au rafiki yake anafuga?

Katika ufugaji mseto wa wanyama na samaki, aina ya wanyama inabidi izingatie imani ya kidini katika eneo husika la ufugaji na walaji. Pia inabidi mfugaji azingatie suala la upatikanaji wa vyakula vya mifugo.

Aina za ufugaji mseto wa samaki

1.Ufugaji mseto wa kilimo cha mazao na samaki. Mimea inayolimwa mashambani au isiyolimwa yaweza kutumika kama chakula cha samaki au kutengenezea chakula cha samaki. Mimea hii pia yaweza kutumika kama mbolea ya kurutubisha shamba hasa pale ambapo mbolea za wanyama ni nadra kupatikana.

Mimea ambayo imekuwa ikitumika katika maeneo mengi kama chakula cha samaki ni pamoja na majani ya tembo, mahindi, viazi vitamu, mtama, maharage ya soya, mboga mboga kama mchicha, sukuma wiki, spinachi, Chinese

Mabaki ya mazao yatokanayo na mimea kama vile mihogo, maganda ya ndizi, majani ya mapapai na maganda yake, pumba za mahindi, mtama, ufuta na mpunga hutumika kama chakula cha samaki. Kama eneo linafaa kwa kilimo cha mpunga basi mkulima anaweza kutengeneza mseto wa mpunga na samaki.

 Kambale na perege wanaweza kufugwa katika mashamba ya mpunga hasa msimu wa kulima mpunga. Kwenye shamba la mpunga mbolea inaweza kuongezwa ili kuongeza uzalishaji wa vyakula vya asili kwa ajili ya samaki.

Mseto wa kuku au bata na samaki

Wakulima wengi huwa wanafuga kuku au bata katika maeneo yao ya kuishi. Faida au mazao yatokanayo na kuku ni pamoja na mayai, nyama na samadi ya kuku. Samadi ya kuku ina virutubisho vingi kwa matumizi ya shamba pamoja na mabwawa ya samaki.

Katika mseto huu banda la kuku au bata linaweza kujengwa kando ya bwawa au juu ya bwawa la samaki. Katika mseto wa bata na samaki, huwa bata anatumia bwawa kama sehemu ya kuishi na malisho wakati huo akiwa anarutubisha bwawa.

Bata huwa wakati wa mchana anatafuta chakula ndani ya bwawa na usiku anakuwa kwenye banda. Bata huwa wanakula viluwiluwi wa chura, vimelea vya mbu, wadudu na majani ambayo yapo ndani ya bwawa.

Mseto wa ng’ombe, mbuzi, kondoo au sungura na samaki

Tofauti na kuku au bata, mbolea itokanayo na kinyesi cha wanyama kama ng’ombe, mbuzi na kondoo huwa ina virutubisho vichache. Hata hivyo, hii mbolea inaweza kutumika baada ya kuikusanya kwa muda kabla ya kuitumia.

Rojorojo itokanayo na kinyesi cha ng’ombe baada ya kupitia kwenye mtambo wa biogesi ni nzuri zaidi kutumika katika mabwawa ya samaki. Mbuzi na kondoo wanaweza kutumika ingawa katika maeneo mengi ni vigumu kukusanya kinyesi chao kutokana na mfumo wa ulishaji.

Kinyesi cha sungura pia kinaweza kutumika katika kurutubisha bwawa kwa kujenga banda juu ya bwawa kama ilivyo kwa upande wa ufugaji kuku.

Mseto wa nguruwe na samaki

Ufugaji mseto unaweza kufanyika kwa nguruwe mdogo mwenye umri wa kuanzia mwezi mmoja na nusu hadi miezi mitatu hadi kufikia kiwango cha uuzaji yaani kilo 60 hadi 100 kwa muda wa miezi 5 hadi 6.

Pia, unaweza kufanyika kwa kufuga nguruwe mwenye uzito kuanzia kilo 10 hadi 15 kwa kipindi cha siku 180 ambapo  atauzwa  akiwa na wastani wa kilo 80 hadi 105. Kwa mseto huu, mzunguko mmoja wa samaki unaenda sambamba na mzunguko mmoja wa nguruwe.

 Kwa maana hiyo kwa muda wa miezi sita, mfugaji anavuna nguruwe na samaki kwa wakati mmoja. Idadi ya wanyama inatakiwa iendane na mahitaji ya mbolea kwenye bwawa. Kwa kawaida wanahitajika nguruwe 60 kwenye bwawa lenye ukubwa wa hekta moja. Nguruwe mmoja ana uwezo wa kutoa mbolea kwa wastani wa kiasi cha kilo 6.5 hadi 7.5 kwa siku.

Aina ya samaki wanaofaa katika kilimo mseto

Perege na kambale ni samaki wanaofugwa katika maeneo mabalimbali hapa Tanzania. Perege ndiye ambaye  anafahamika zaidi kwa wafugaji. Chakula cha asili cha perege ni vimelea vya kijani vilivyomo ndani ya maji, lakini ana uwezo wa kula aina nyingi za vyakula ikiwa ni pamoja na pumba za mahindi na mpunga, majani na mabaki ya jikoni.

Vile vile anakua vizuri kama kutakuwa na mbolea za samadi na za chumvi chumvi, na anaweza kuhimili kiasi kidogo cha hewa ya oksijeni. Madume ya perege hukua haraka zaidi kuliko majike, na uvunaji unaweza kufanyika baada ya kufikisha uzito wa gramu 250.

 Kambale hula vyakula vya asili ndani ya maji kama vile wadudu, konokono, vifaranga wa chura na samaki wengine wadogo. Vilevile anakula vyakula vya ziada kama vile mabaki ya vyakula hasa yenye asili ya nyama. Kambale hutumika kupunguza wingi wa perege ndani ya bwawa.

Hii ni kutokana na ukweli kwamba perege anazaliana kwa wingi kwenye bwawa. Kambale anakua haraka  kama chakula chenye protini kinapatikana kwa wingi. Kambale anaweza kuishi kwenye maji yenye hewa kidogo ya oksijeni. Tofauti na perege, kambale ana mifupa michache na minofu mingi na ni mtamu hasa anapokaushwa kwa moshi.

Faida za kuku katika ufugaji mseto

Chanzo cha mbolea. Lengo kuu la ufugaji wa kuku kwenye ufugaji mseto ni urutubishaji wa bwawa la samaki ili kupata chakula cha asili kwa samaki. Kinyesi cha kuku hutumika kama chanzo cha mbolea kwa sababu huwa kina kiasi kikubwa cha urea.

Hutoa chakula cha samaki. Tofauti na kuwa chanzo cha rutuba, kinyesi cha kuku huliwa moja kwa moja na samaki.

Musa Ngematwa ni mtaalamu wa ufugaji wa samaki. Anapatikana kwa namba 0718986328