Ukaguzi katika bandari za Dar, Z’bar umezidi kero na unawatesa abiria

Abiria wakishuka kwenye meli ya Azam Sealink2 iliyotia nanga kwa mara ya kwanza katika bandari ya Tanga juzi ikitokea kisiwani Pemba, Zanzibar. Picha na Salim Mohammed

Muktasari:

  • Lakini, kwa kiwango kikubwa hali sivyo ilivyo hata kidogo siku hizi kwa mtu anayesafiri kwa boti za mwendo kasi kati ya Zanzibar na Dar es Salaam.

Mtanzania anayesafiri kutoka eneo moja la nchi kwenda sehemu nyengine hutarajia kupata usumbufu mdogo ukilinganisha na ule anaokutana nao anapokwenda nje ya nchi yake.

Lakini, kwa kiwango kikubwa hali sivyo ilivyo hata kidogo siku hizi kwa mtu anayesafiri kwa boti za mwendo kasi kati ya Zanzibar na Dar es Salaam.

Hapana ubishi kuwa ulinzi katika usafiri unao umuhimu mkubwa siku hizi. Hii inatokana na hali ya usalama ilivyokuwa tete duniani kote wakati huu na zaidi kutoka na matukio mbalimbali ya usafirishaji silaha na bidhaa haramu na hatari kama dawa za kulevya. Hii ni mbali ya kuzuia vibaka wasiwaibie abiria mizigo yao.

Lakini, mwendo unaoneana hivi sasa katika bandari zetu na hasa Dar es Salaam hauwezi hata kidogo kukubalika kuwa sababu ya kuwasumbua sana watu wanaposafiri ndani ya nchi yao kwa maelezo ya usalama wao.

Kwa kweli hali iliyopo hivi sasa inafanya abiria kujiona wanyonge katika nchi yao.

Hivi sasa wapo watu ambao huulizana mbona shida kama hizo wanazokumbana nazo nyumbani hawazipati wanaposafiri kwenda nje ya nchi yao.

Tumekuwa tukiambiwa mtu kwao, yaani mtu kuionea fahari nchi yake na kufurahia anapokuwepo nyumbani, hata pale anapoamua kuondoka sehemu moja ya nchi kwenda nyengine, iwe kwa matembezi au kazi.

Kwa muhtasari yanayotokea mara nyingi katika bandari zetu za Zanzibar na Dar es Salaam ni mashaka matupu na kwa kiasi fulani yanapelekea hata mtu mara nyengine ajute kwa nini aliamua kuifanya hio safari.

Tukumbuke kwamba baadhi ya wasafiri ni wazee, wagonjwa au watu wenye ulemavu.

Matatizo kwa wasafiri huanza tokea kwenye upatikanaji wa tiketi za usafiri. Duniani kote ni jambo la kawaida siku hizi kwa mtu kutumiwa tiketi kutoka eneo moja la nchi au hata nje.

Lakini, hili halipo siku hizi hapa kwetu kama vile ni jambo ambalo halikubaliki na linahatarisha usalama.

Mwenendo huu ulioanza kutumika hivi karibuni umepelekea kuwepo usumbufu mkubwa kwa baadhi ya watu wanaotaka kufanya safari.

Hii inatokana na baadhi ya watu kutarajia sehemu zao za kazi, wazee, ndugu jamaa au marafiki kuwasaidia kuwanunulia tiketi.

Wakati mwingine mtu huwa mbali sana na eneo la bandari ambapo ndipo panapouzwa tiketi na humuomba mtu ambaye yupo karibu na hapo afanye hivyo ili akifika bandarini apate tiketi yake.

Baadaye mtu huyo anapokwenda bandarini kuchukua tiketi hutakiwa kutaja namba ya tiketi na kuonyesha kitambulisho ili akabidhiwe tiketi baada ya kuhakikishwa jina la usajili liliopo katika tiketi ni sawa na lile liliopo kwenye kitambulisho chake.

Mwenendo huu hivi sasa tunaambiwa kuwa haukubaliki na haupendezi kwa wale wanaotaka kusafiri kwa njia ya bahari kati ya Zanzibar na Dar es Salaam.

Hata hivyo, mwenendo huu unaendelea kuwa ni jambo la kawaida katika usafiri wa ndege na hata mabasi au treni hapa kwetu na katika nchi nyingi duniani.

Haya tunayoyaona hapa kwetu ni makubwa na yanazusha maswali mengi yasiokuwa na majibu ya kuridhisha.

Matatizo hayaishii hapo. Abiria huwa anaangaliwa tiketi yake na kitambulisho mara nne au tano kabla na wakati wa safari kwa kuanzia katika mlango wa kuingia eneo la bandari.

Baadaye hutakia kuonyesha tiketi na kitambulisho anapoingia sehemu ya kupandia boti na wakati anapoingia ndani ya boti.

Anapoingia ndani ya hio boti mtu anaweza kujikuta amesinzia na kuamshwa kutakiwa aonyeshe tiketi yake na wakati mwingine zoezi hilo hufanyika mara mbili wakati wa safari.

Jingine lenye usumbufu mkubwa ni ukaguzi wa mizigo ambao huanza dakika chache kabla ya safari. Kuchelewa kwa ukaguzi wa mizigo kumekuwa kunapelekea kuwepo msongamano wa abiria na huwaa balaa isioelezeka pale inaponyesha mvua, hasa Dar es Salaam.

Ukiwaona akina mama wenye watoto wachanga mgongoni wanavyohangaika huku wakinyeshewa mvua utasikitika na kuwaonea imani na kukupelekea kujiuliza: Hivyo kweli hatuna huruma kwa hawa wazazi na watoto wao wadogo?

Mara nyengine abiria hutakiwa kwa muda wa hadi nusu saa kungojea huku wakinyeshewa mvua. Hii hutokana na maelezo kwamba umeme umekatika au mashine ya kukagua mizigo imeharibika na inatengenezwa.

Usumbufu huu wa mashine kutofanya kazi umekuwa ni jambo la kawaida katika bandari ya Dar es Salaam. Hapo zipo mashine mbili za kukagua mizigo, lakini moja tu ndio inafanya kazi na hiyo iliobakia leo ikifanya kazi kesho utaambiwa kuwa imeharibika na abiria wasubiri itengenezwe.

Hapo tena abiria huganda kwa muda mpaka ufanyike uamuzi wa wakaguzi kuifanya kazi ya kupekua mizigo na abiria kwa mikono.

Wakaguzi hutumia dakika 10 hadi 15 kujitayarisha kuvaa glovu kwa ajili ya kufanya kazi ya upekuzi.

Kwa muhtasari wakati umefika wa kutafuta njia za kupunguza bughudha hizi ziliopo katika bandari zetu ili wasafiri wapungukiwe na usumbufu mkubwa wanaoupata hivi saa.

Lakini kwa ujumla mfumo mzima wa usafiri kwa hizi boti za mwendo wa kasi unafaa kufanyiwa mapitio ili kuhakikisha wasafiri hawateseki bila ya sababu za msingi.

Watanzania, huku wakielewa umuhimu wa kuhakikisha usalama wao katika

safari, wanayo haki ya kudai kutosumbuliwa bila ya sababu za msingi wanapofanya hizi safari za kati ya Zanzibar na Dar es Salaam.

Ni vizuri kwa wahusika katika taasisi za Serikali zinazohusika na usafiri wa bahari na utawala wa hizi boti kuangalia njia nzuri za kupunguza usumbufu usio wa lazima kwa abiria.

Umekuwa ukisisitiza Watanzania wa Bara na Visiwani kutembeleana na kufanya biashara kama mojawapo ya njia za kuimarisha Muungano.

Lakini, kwa mazingira yaliopo hivi sasa katika bandari zetu unaweza kusema kinachofanyika ni kumfanya mtu afikiri mara mbili kabla ya kuamua kufanya safari kwa njia ya bahari.

Tujifunze kutokana na makosa tuliyoyafanya siku za nyuma na tunayoendeleza hivi sasa, uzoefu tulioupata hapa kwetu na njia

wanazotumia wenzetu ili kupunguza matatizo yasio ya lazima wanayowakabili wasafiri hivi sasa.

Ni vizuri hata pakawekwa sanduku la maoni ya abiria au kuwepo fomu za abiria

kutoa malalamiko yao au ushauri wa njia gani zinafaa kutumika ili usafiri kati ya pande zetu mbili za Jamhuri ya Muungano uwe wa raha na

furaha badala ya karaha iliopo hivi sasa.

mwisho