UCHAMBUZI: Ukatili dhidi ya wanawake, watoto ni vita vya jamii nzima

Muktasari:

Lakini, Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009, mtu yeyote haruhusiwi kusababisha mateso au kumpa mtoto adhabu ya kikatili au kumfanyia matendo yenye kumshushia hadhi na kumsababishia maumivu makali.

Vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto nchini vinaonekana kushamiri. Utafiti wa matukio ya vitendo vya ukatili dhidi ya wanawake na watoto ya mwaka 2011 unaonyesha asilimia 45 ya wanawake nchini wamekuwa wakitendewa ukatili wa kijinsia.

Lakini, Sheria ya Mtoto namba 21 ya mwaka 2009, mtu yeyote haruhusiwi kusababisha mateso au kumpa mtoto adhabu ya kikatili au kumfanyia matendo yenye kumshushia hadhi na kumsababishia maumivu makali.

Hii ni pamoja na mila na desturi zozote zenye kudhalilisha utu wa mtoto au zinazosababisha athari na maumivu ya mwili au ya akili kwa mtoto.

Licha ya sheria hizo kuwapo na wadau kukemea matukio hayo kila kukicha bado matukio hayo yanaendelea kushamiri, hali inayoendelea kumnyong’onyesha mwanamke na mtoto.

Pedro Guerra wa Shirika la Watoto Duniani (Unicef) anasema takribani watoto watatu kati ya 10 wamekuwa wakitendewa ukatili na ndugu au jamaa zao wa karibu.

Utafiti pia unaonyesha kuwa zaidi ya asilimia 13 ya watoto wa kike hufanyiwa ukatili kabla ya kufikisha umri wa miaka 18 na kwamba wapo baadhi ya watoto na wanawake waliopoteza maisha, huku wengine wakijeruhiwa kutokana na kipigo.

Kwa mujibu wa utafiti wa kitaifa kuhusu hali ya ukatili dhidi ya watoto nchini, uliofanyika mwaka 2009, asilimia 73.5 ya watoto wa kike na 71.7 ya watoto wa kiume hukabiliwa na ukatili ambao kwa kiwango kikubwa uhusisha vipigo.

Imekuwa kawaida kusikia taarifa za wanawake au watoto kupigwa, kuchomwa moto na kupewa adhabu nyingine ngumu zisizofaa huku ukatili kwa wanawake majumbani ukiendelea kuongezeka kwani kati ya wanawake watatu, wawili wanatendewa ukatili wa kijinsia na waume zao.

Huu ni muendelezo wa vitendo vya kikatili wanavyofanyiwa wanawake na watoto licha ya wadau na vyombo vya habari kujitokeza kukemea matukio ya namna hiyo.

Wataalamu wa afya wanasema kipigo kwa watoto ni hatari kwani kinaweza kuwasababishia madhara makubwa kiafya, kisaikolojia na kimwili.

Bila kujua kama kipigo kinamfunza au kumdumaza mtoto kiakili, jamii imejikuta ikiendelea kuwaadhibu watoto kwa kuwapiga wakati mwingine bila huruma.

Unapompiga mtoto kupita kiasi tarajia ataathirika kisaikolojia na kujikuta akishindwa kufanya vizuri darasani na mara zote atakuwa mnyonge hivyo wazazi, walezi au walimu wanaweza kutumia njia mbadala kuwakanya watoto wanapokosea ikiwamo kuzungumza nao kwa busara badala ya kuwapiga.

Magreth Mussai, Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Watoto, Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto anasema jitihada za makusudi kutoka kwa jamii na serikali kwa ujumla zinahitajika ili kukabiliana na changamoto hii.

Mussai anasema ni wajibu wa jamii kusimama kidete kukemea na kutokomeza vitendo vinavyoashiria kumuumiza, kumdhalilisha na kumuathiri kiakili na kisaikolojia mtoto na mwanamke.

Anasema Serikali kupitia hiyo, ipo mbioni kuanzisha mpango wa kitaifa wa kuhakikisha vitendo vya ukatili wa kijinsia vinamalizika.

Akizungumza kwenye semina iliyoandandaliwa na mashirika ya Umoja wa Mataifa; Unicef, UNFPA na UN-Women, Mussai anasema Serikali imeshafanya maandalizi ya awali ili kuanzisha mpango huo.

Anasema jitihada mbalimbali kwa kutengeneza sera zinachukuliwa, sheria na hata kusaini mikataba ya kimataifa ili kupinga vitendo hivi.

0714233929.