KONA YA MAKENGEZA : Ukikubaliana na nia, lazima ukubaliane na njia

Muktasari:

  • Basi wakati nakaa hivyo na kufutafuta jasho kila baada ya dakika mbili, nikashtuka kumwona mtu amesimama mbele yangu. Alikuwa bonge ya mtu na alivyokunja uso, kwa kweli nilitishika kidogo. Niliangalia kushoto na kulia lakini niliona watu wanaendelea na shughuli zao kama vile hakuna kitu. Basi nikapiga moyo konde.

Juzi nilikuwa nimekaa nje ya nyumba yangu nikitafuta angalau kaupepo kadogo bila kulazimika kusikia jua kali utosini. Mmmh, jua la siku hizi ...halina hata huruma.

Basi wakati nakaa hivyo na kufutafuta jasho kila baada ya dakika mbili, nikashtuka kumwona mtu amesimama mbele yangu. Alikuwa bonge ya mtu na alivyokunja uso, kwa kweli nilitishika kidogo. Niliangalia kushoto na kulia lakini niliona watu wanaendelea na shughuli zao kama vile hakuna kitu. Basi nikapiga moyo konde.

‘Karibu ndugu yangu.’

‘Mimi si ndugu yako. Tena wewe hunifahamu lakini mimi nakufahamu.’

‘Karibu basi tufahamiane.’

‘Sina haja ya kufahamiana na wewe. Nakuambia hivi. Jina langu ni Musa Lendo na sifurahii makala zako hata kidogo.’

‘Sawasawa. Ni haki yako kupenda au kutopenda. Kwa nini huzifurahii?’

‘Naona kazi yako ni kukejeli tuuuuu, kukejeli tuuuuu kama vile hakuna kitu kizuri kinachofanyika ndani ya nchi hii.’

‘Si kweli. Najua kuna mambo mengi mazuri yanayofanyika ndani ya nchi yetu na wapo watu wengi wa kutosha kuyasifia huku mimi nikiunga mkono. Pili katika mambo mengine, kutoa mawazo mbadala ni katika kutaka yawe mazuri zaidi.’

‘Wewe ni nani?’

‘Mimi kama wewe. Kila mmoja ana haki ya kufurahia au kutofurahia, pamoja na kutoa mawazo yake.’

‘Wajitetea tu na uhalifu wako. Wewe ni nani kuhoji nia njema ya watu kuleta mabadiliko chanya?

‘Hapo ndiyo umekosea kabisa. Katika mambo mengine waweza kufurahia nia lakini si njia. Waweza kuona kwamba njia inayotumika inavuruga nia.’

‘Njia ... nia ... nia ... njia. Yote hali moja. Na sitaki kubishana na wewe maana utamwaga maneno ya asali, utachezacheza na maneno matamu hadi utanichanganya. Sitaki.’

‘Si tunabadilishana mawazo?’

‘Yako ni sumu, Sitaki. Si ajabu ni mbwia unga na wewe.’

‘Ohoo. Yaani ukitoa wazo tofauti tayari umekuwa mwanamihadarati?’

‘Tutajuaje?’

‘Na mimi nitajuaje kwamba wewe hujaleweshwa bangi pia?’

Jamaa alivyokunja ngumi nikajua nikitoka hapa bila ngeu moja, Mungu atakuwa ameninusuru. Lakini sikutaka kukaa kimya mbele ya vitisho vyake.

‘Sasa kama hutaki kubadilishana mawazo na mimi, kwa nini umenifuata?’

‘Ahaa. Swali zuri. Mimi na wenzangu tumeona kwamba unahitaji kusaidiwa?’

‘Kusaidiwa?’

‘Ndiyo. Sisi tunapenda sana nchi yetu ..’

‘Hata mimi napenda sana.’

‘Hebu nyamaza na kusikiliza. Sisi tunapenda nchi yetu. Tunapenda nchi yetu ipate sifa inayostahili. Tunaona kwamba hata nchi za nje, hata Marekani, zinapaswa kujifunza kutoka kwetu ...’

Nilifungua mdomo kujibu lakini yeye akafunga ngumi hivyo ikabidi ninyamaze. Akaendelea.

‘Kwa hiyo, nitakuwa ninakuletea makala ambazo sisi tumetengeneza na utaweka kama makala yako. Utakuwa Makengeza asiyekengeuka.’

‘Eti nini?’

‘Usinietinini! Umesikia vizuri. Sasa chukua makala hii na ole wako kama haitatoka wiki hii.’

Kufumba na kufumbua, jamaa alikuwa amepotea, ungedhani jini duh! Basi waishiwa wenzangu, baada ya kusoma makala yake, nikaona hakuna ubaya. Msingi wa mwanademokrasia ni kusikiliza pande zote, na kutumia akili yake kupambanua baini ya kweli na feki, bora na dhaifu, ya tija au ya teja. Kwa hiyo, karibuni kwenye makala ya Ndugu Musa Lendo.

Bongo ni Bongo na kama Bongo, tangu enzi za awamu ya kwanza, tumekuwa na mengi sana ya kufundisha, si Afrika tu bali dunia nzima. Shida ni kwamba mara nyingi dunia nzima inashindwa kutambua hiyo, ndiyo maana tumeamua kutoa makala za mara kwa mara ili kuielimisha dunia na hasa viongozi wa dunia jinsi ya kuendesha nchi zao.

Tumchukue huyu Rais mpya wa nchi ya kutamba daima. Serikali yake inamgharamia ndege kubwa ya fahari zote. Anaenda popote duniani raha mstarehe lakini imebidi kutumia mitandao ya jamii kulalamika eti tishu za ndege yake si laini vya kutosha. Kweli wananchi wake watamwelewa hivyo. Iwapo anataka kusikilizwa na kuheshimiwa na watu wake, si tu aachane na ulaini wa tishu zake. Aachane na safari kabisa. Kwa nini atumie hii ndege kuuuubwa kila wakati. Inagharamia kiasi gani. Tunajua alilelewa kitajiri hadi akalewa utajiri wake, si kama viongozi wetu ambao wamepambana na jembe kuanzia walipoacha titi la mama lakini suala la kwanza ni kuonesha kwamba uko pamoja nao ndipo watakufurahia sana hata ukitoa amri kumikumi zinazokera.

Ndipo hapo tunakuja kwenye somo la pili kwake. Ukishajenga umaarufu, ukishaonesha kwamba wewe ni mwenzao, ni rahisi sana kuwaziba mdomo wale zabizabina ambao wanataka kupinga. Kweli kabisa, tumeshangaa sana kuona kwamba kwanza watu wake wanaandamana kila siku. Hawana kazi hawa? Wafutwe kazi moja kwa moja kwa kufanya mambo ya kijinga saa za kazi. Sisi tumehakikisha waache hata kuangalia mambo ya siasa kwenye runinga saa za kazi (isipokuwa mambo muhimu ya kwetu) iweje waache kazi kabisa kwa ajili ya kupinga mipango yake mizuri. Halafu habari zinavuja utadhani ikulu ni kopo lililotobolewa kwa ajili ya kumwagilia bustani. Iwapo huyu Rais hajui jinsi ya kutumbua majipu, aje kwetu tumpe semina ya utumbuaji.

Sasa tatu, tunaona magazeti, vituo vya runinga na mitandao ya jamii vyote vinampinga na kuumbua kila siku. Tunaona kwamba anawasema vizuri na kuwaambia wanatakiwa kuchapisha nini lakini hii haitoshi maana ni uchochezi moja kwa moja.

Iwapo anajua alishinda kwa kishindo na wao bado wanang’ang’ania na uzabizabina kwamba mpinzani wake alipata kura lukuki kuliko yeye, afanye kwa vitendo si tu kuwatukana kila siku.

Yaani, anataka kuwa kuku mbele ya mwewe wakati yeye ni mwewe kabisa na wao ni kuku? Hakuna haja kubishana nao. Awafunge.

Awakamate vizabizabina na kuwashtaki kwa kuendeleza chuki dhidi yake yeye, tena bila hata dhamana. Uchochezi gani huo! Na kwa kuwa inaonekana huyu Rais mwenyewe ni mlevi wa mitandao ya jamii, badala ya kuwatumia watu wake, basi apige marufuku watu kubishana naye. Akishasema amesema. Vinginevyo kweli wachochezi watashinda na yeye ataporomoka.

Ndipo hapo nakuja kwenye masuala ya mwisho. Sisi kweli tunashindwa kuelewa iweje yeye kama Rais anatoa amri, serikali yake inaanza kutekeleza hiyo amri kisha wanasheria wanaibuka na kurukaruka kama kumbikumbi kwenda kuwatetea walewale ambao amewapiga marufuku.

Hapa kweli mawakili hao hawashirikiani na maadui wa taifa? Wakamatwe na wao kwa kusaidia maadui, tena magaidi. Awakamate hata na majaji wanaozuia amri yake. Yeye ni Rais, akishasema amesema, hawa wengine ni nani kumbisha? Potelea mbali vinadharia vya hovyohovyo vya mihimili mbalimbali sijui. Himili uko pale kumhimili yeye siyo kumtingisha na mhimili wake. Duh! Nadhani anapaswa kubadili katiba kabisa ili majaji wote hao wateuliwe na yeye ili waelewe vizuri kazi yao na wanamtumikia nani.

Kwa hiyo, Marekani acheni kiburi chenu cha kikaburu. Kubali kujifunza, kubali kujifunza kutoka kwetu.

Musa Lendo na kikundi chake maarufu cha kutoa elimu kote duniani.

Haya jamani ndiyo maneno ya yule mgeni wangu. Mnaonaje?