Ukimtegemea mwanamke, hesabu moja, mbili, tatu

Sunday October 29 2017

 

Asikwambie mtu, wanaume ndiyo viumbe tulioumbwa na mioyo ya uvumilivu zaidi ya kiumbe chochote hapa duniani. Wenyewe tuna uwezo wa kuhudumia kwa muda mrefu bila kuchoka hata kwa vitu ambavyo vinatuumiza.

Kwa mfano, unakuta nyumbani mnaishi na kaka wa mkeo asiyefanya kazi yoyote, na anakutia hasara kweli kweli, lakini hata siku moja huthubutu kunyanyua mdomo wako kulizungumza, linaishia huko huko tumboni, unafanya mambo yako mengine, siku zinaenda.

Sasa tukio hilo hilo liwe upande wa mwanamke, yaani mdogo wako asiyekuwa na kazi ndiyo awe anaishi nyumbani na anatia hasara pia. Wewe hesabu wiki mbili tu, ya tatu lazima utatafuta nauli na kwa kumpeleka kwa jinsi atakavyoshambuliwa kwa nyukilia za maneno na mkeo— wenzetu hawajui kuvumilia kabisa.

Na sio kwa kaka yako tu anayeishi nyumbani kihasara hasara — wanawake wana kawaida ya kukichoka kila kitu ambacho hakitoi faida ya kuonekana kwa jicho la kawaida, kitu ambacho kinafanana tabia na mzigo, yaani chenyewe hakina mbele wala nyuma, kinasubiri kubebwa na kuhamishwa kupelekwa pale, kurudishwa huku.

Ukifanikiwa kulifahamu hilo, unatakiwa pia ufahamu kwamba mwanaume anayemtegemea mwanamke, ni mzigo. Kwa hiyo kwa kuwa mwanamke ana kawaida ya kuichoka mizigo, hata wewe ni wa kujihesabia moja, mbili kisha tatu itakuja yenyewe bila kuitwa.

Kama hujabahatika kuona visanga vya mwanamke aliyeanza kumuona mwanaume ni mzigo unapaswa kupewa pole na hongera. Hongera kwa sababu utakuwa umepata bahati ya kuishi duniani bila kushuhudia matukio ya kusikitisha zaidi na pole kwa sababu umekosa somo muhimu mno kwa dunia hii ya sasa, ya wanawake wenye nguvu za kukaribiana na wanaume au kulingana kabisa.

Siku hizi utakuta kijana wa kiume ambaye hana shughuli ya maana ya kumuweka mjini, anakesha akiomba ashukiwe na anachokiita bahati, apate mwanamke mwenye fedha, amuhudumie.

Na ilivyo, kwa Mungu ukiomba unachokiona ni samaki, atakupa tu— mwanamke wa kukuhudumia utampata, atakupa chakula, nyumba ya kulala na vyote muhimu unavyovipenda.

Lakini sasa, ili kujua kwamba wanawake hawauwezi uvumilivu kama sisi, huwa hawamalizi hata miezi kumi na mbili, anayesaidiwa anaokana ni mzigo usio na faida, kwa hiyo ile hamu ya kubeba inakatika kabisa.

Nadhani vijana wa kisasa wanaopotezea muda wa kutafuta kulelewa walihitaji kupata ushuhuda toka kwa baba zao wa jinsi mama alivyokuwa akinuna bila sababu kipindi mzee hana ajira ya kueleweka.

Kwa kuanzia hapo wangeelewa, ikiwa baba aliyewahi kuwa na ajira alitendewa hivyo, mimi itakuwaje?

Advertisement