Ukishindwa kilemba vaa kofia

Muktasari:

  • Awali ufungaji wa vilemba ulikuwa ukionekana zaidi misibani, makanisani na mashambani lakini sasa unaonekana kila mahali.
  • Hilo limetokana na wenzetu wa Nigeria walivyoamua kuendeleza utamaduni wao huo na kila kukicha kubuni mitindo mipya ya ufungaji wa vilemba.

Siyo wote tuna utaalamu wa kufunga vilemba licha ya kuwa tunapenda mtindo huo.

Awali ufungaji wa vilemba ulikuwa ukionekana zaidi misibani, makanisani na mashambani lakini sasa unaonekana kila mahali.

Hilo limetokana na wenzetu wa Nigeria walivyoamua kuendeleza utamaduni wao huo na kila kukicha kubuni mitindo mipya ya ufungaji wa vilemba.

Kama tulivyoona hapo awali si wote wenye uwezo wa kufunga vilemba hivi kwa ustadi ndipo wabunifu walipoongeza utaalam kwa kutengeneza kofia ambazo zinazofanana kabisa na kilemba.

Ukiangalia kwa haraka unaweza usitambue kama aliye mbele yako amefunga kilemba au amevaa kofia, hilo linatokana na namna zilivyotengenezwa kisasa.

Kofia hizi zipo katika mitindo na rangi mbalimbali, hii humpa fursa mtu kuchagua kulingana na matakwa yake.

Uzuri wa kofia hizi zinaweza kuvaliwa mahali popote na mvaaji akaendelea kuonekana wa kisasa tofauti na ilivyokuwa hapo awali.

Ilikuwa nadra kumkuta mtu kavaa suti na kofia. Mtindo huu wa kofia unakuruhusu kuipigilia na suti na bado utaendelea kuonekana nadhifu.

Unaweza pia kupiga suruali yako ya jeans na blauzi utakayopenda kisha juu ukatupia kofia yako kulingana na rangi ulizochagua.

Ukivaa nguo za vitenge ndiyo hasa mahala pake zinaendana mno na kofia hizi kama inavyoonekana pichani.

Ingawa kila mtu ana chaguo lake ila ukitaka kunoga zaidi ukivaa kofia hii uvae kiatu chenye kisigino kirefu kiasi.

Imeandaliwa na Elizabeth Edward