KONA YA MAKENGEZA : Umaarufu wa marufuku na kuandamwa kwa maandamano

Muktasari:

  • Kwa wakuu wa chama twawala
  • kwanza kabisa (maana hakuna kwanza nusu), tunapenda kuwapongeza kwa ushindi wenu mnono wa mwaka juzi. Kweli kwa msemo wa yule Mrumi Juliasi Kaisari, mlikuja, mliona, mlishinda. Jinsi mlivyoshinda, sisi wengine hatukuwa na ubishi. Tubishe nini wakati sisi tuliwapatia silaha za kutushinda sisi wenyewe.

Watu wengine sijui akili zao zikoje. Ninafurahi sana kwamba wanawasifu wachapakazi wetu na hata wachapa wasiochapa kazi kwetu, lakini sifa zenyewe mmmh!

Kwa wakuu wa chama twawala

kwanza kabisa (maana hakuna kwanza nusu), tunapenda kuwapongeza kwa ushindi wenu mnono wa mwaka juzi. Kweli kwa msemo wa yule Mrumi Juliasi Kaisari, mlikuja, mliona, mlishinda. Jinsi mlivyoshinda, sisi wengine hatukuwa na ubishi. Tubishe nini wakati sisi tuliwapatia silaha za kutushinda sisi wenyewe.

Ieleweke wazi hapa, simwongelei mtu, wala sitaki kuangalia ukweli wa shutuma za kushoto na kulia uko wapi katika malumbano haya. Nasema tu kwamba huwezi kuwa na sera ya kulaani sura kwa miaka kadhaa kisha, kugeuza sura hiyohiyo kuwa sera yenyewe.

Yawezekana sura ni sura kwelikweli kushinda sura zote, lakini bado utaonekana kigeugeu na sera zingine zitapoteza sura moja kwa moja. Huwezi kubomoa msingi na kutegemea nyumba itasimama imara.

Ndiyo maana tuliishia kujitetea dhidi ya kejeli na bezo zenu. Badala ya kuweza kuuza sura bora za sera zetu tukabaki kutetea sura ileile tuliyoshambulia. Kweli lilikuwa janga letu.

Kwa hiyo, hata baada ya uchafuzi ule mkuu (na mnajua kwa nini tunauita uchafuzi) tulibaki tumesononeka, si tu kwamba tulishindwa, bali tulikuwa hatujui tujijenge vipi.

Sisi hatujawa mabingwa wa kunadi sera, bali kuona kasoro ndani ya sera zenu. Sasa tutajiandaaje na kuuza sera ambazo hatuna huku nyinyi mkionyesha nia thabiti ya kugeuza sera za sura ziwe sera za ukweli.

Ndipo hapo mmetusaidia na tunawashukuru kwelikweli. Kitu kimoja sisi Wabongo hatupendi kuona ni mtu akinyanyaswa hivihivi. Nadhani ni kasumba yetu tangu enzi za baba yetu.

Tukiona mtu ananyanyaswa, tayari tutaanza kumpenda na kumshabikia na hata kumfuata. Kwa nini anyanyaswe? Kwa hiyo, wanapokamatwa watu wetu na kutiwa ndani, kwa kutumia mbinu zote za kisheria (na nani hajui kwamba mbinu nyingine ni hila), kweli mmefanikisha azma yenu ya kutuswaga mahali pa mafichoni, lakini kufichwa ni kusahaulika? Wahenga walisema kwamba unaweza kushinda pambano lakini bado ukashindwa vita. Pambano la kuwatia watu ndani mmeshinda lakini vita mnao uhakika wa kushinda?

Mmeshinda pambano la kutunyamazisha tusiweze kukutana na wananchi tunavyopenda, lakini vita mmeshinda? Thubutu! Kinyume chake, tumeanza kurudisha umaarufu wetu kidogokidogo maana inaonekana waziwazi kwamba tunanyanyaswa.

Heko na pongezi kwenu na ingawa hatupendi kuona wenzetu wanatiwa kufuli, endeleeni vivyohivyo.

Aidha sisi Wabongo tunaweza kudanganywa na nadhani tumewahi kudanganywa mara nyingi, lakini hatupendi kudanganywa mchana kweupe.

Hatupendi kuambiwa kitu hakipo wakati kipo au kitu kipo wakati hakipo. Sisi wengine ni wazee wa enzi za baba yetu na tunakumbuka. Ikitokea shida, waheshimiwa walikuwa wanajaribu kuvungavunga, kutoa maelezo mwendo wa nyoka lakini tulikuwa tunakataa.

Ndiyo maana mara nyingi ilibidi baba yetu asimame na kutueleza hatua kwa hatua, hali halisi ikoje. Ndipo tukatulia maana tulielewa na kuridhika. Hata kama ukweli ulikuwa chungu, tulieleweshwa, hatukulazimishwa ukweli fulani.

Tena hali hii inanikumbusha mchapo mwingine wa baba yetu. Naomba ieleweke kwanza siongelei hali ya sasa. Najua leo hali ni ya ukame, si ya njaa na sote tunamwomba Mungu hali hii ya ukame iishe.

Tupo pamoja. Lakini bado naona mchapo huo wa baba wa Taifa unasaidia. Alienda nje kwenye mkutano fulani ambapo alimwambia Rais wa Marekani kwa unafiki wake huohuo ambao huyu mpya anaonekana anao. Baada ya mkutano, wale wenye majukumu ya kuangalia hali halisi ya chakula duniani walimwita baba yetu pembeni na kumtonya. “Mbona huchukui hatua yoyote wakati kuna njaa nchini?”

Baba alishangaa na kukataa. Kwa hiyo walimwonyesha picha zilizopigwa kutoka juu. Kuona hivyo, mwalimu aliporudi nyumbani akawaita wakuu wake wa maeneo na kuwauliza kuhusu njaa. Sasa sijui ni kwa sababu ya woga wa kuonekana hawafanyi kazi au hila au kiburi au kutojali, wakakataa katakata. “Hakuna shida baba. Watu wanakula na kusaza tunakwambia.”

Baba alitaka kupata uhakika. Aliwatuma vijana wake kufanya uchunguzi. Lakini wakuu wa maeneo nao si wajinga. Wakawadaka wale na kuwasisitizia kwamba kweli wanakula na kusaza, kisha wakawaonyesha maeneo ambayo bado yalikuwa mazuri. Basi vijana wakarudi na kutoa taarifa.

“Hakuna shida baba. Watu wanakula na kusaza.”

Mwalimu bado hakuridhika. Kwa nini wale waliomtonya wamdanganye? Ni hila za mabeberu? Nani msemakweli. Basi kawaita mapadre na wachungaji na masheikh na maimamu. Wakamwambia “baba, sehemu nyingine kuna njaa. Watu wanakula majani tu.” Ndipo baba alichukua hatua ya kuwanusuru watu.

Sasa tunajua kwamba leo ni tofauti. Tunajua kwamba shida ni uvivu wetu, utegemezi wetu, raha yetu ya kulala chini na kufungua mdomo chakula kidondoke kutoka juu.

Sisi ni watu ‘hopulesi’, lakini inawezekana kuna watu ambao tayari wana njaa. Sasa wakuu wa maeneo wakifanya vilevile walivyofanya enzi zile eti wanaogopa kutumbuliwa wasiweze kuendelea kutumbua, ni lazima sisi tuamke kutetea waishiwa dhidi ya waheshimiwa.

Na kwa kufanya hivyo, hata tukinyamazishwa, tutapendwa na waishiwa wenzetu kwa kadiri tunavyopondwa na waheshimiwa.

Tatu, tunashukuru kuambiwa maandamano basi. Hata sisi tulikuwa tunafikiria jinsi ya kuachana na maandamano maana kuna faida gani kumtangazia adui wako:

“Jamani ee, tutaandamana. Hata mkituandama, tutaandamana. Naam. Tutaanza mahali fulani na kupita maeneo mahali fulani na kuishia mahali fulani.”

Kwa njia hiyo, tulikuwa tunawarahisishia kazi wale wenye uchu wa kututwanga.

“Haya. Kazi ya kupiga. Saa nne. Mahali fulani. Mbele twanga!”

Tumetwangwa kweli. Ndiyo maana tulikuwa tumeshaanza kuona umuhimu wa kutafuta mbinu mbadala.