Umuhimu wa huduma ya unasihi kwa wanafunzi-2

Muktasari:

  • Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa nyakati tofauti, imekuwa ikitoa nyaraka zinazotoa maelekezo ya hatua za kuchukua katika kukabiliana na matatizo ya kijamii yanayoweza kuathiri maendeleo ya wanafunzi.

        Tumeona jitihada mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali katika kupambana na changamoto za kijamii zinazowakabili wanafunzi katika ngazi mbalimbali za elimu.

Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia kwa nyakati tofauti, imekuwa ikitoa nyaraka zinazotoa maelekezo ya hatua za kuchukua katika kukabiliana na matatizo ya kijamii yanayoweza kuathiri maendeleo ya wanafunzi.

Katika makala yaliyopita, tuliona mifano kadhaa ya jitihada hizi. Waraka wa Elimu namba 3 wa mwaka 2000, mathalani, ulilenga kuwajengea wanafunzi uwezo wa kujilinda na maambuzi ya Ukimwi.

Aidha, Waraka wa Elimu namba 11 wa mwaka 2002 ulianzisha huduma za malezi na ushauri nasaha kwenye taasisi za elimu.

Mpango huo hata hivyo, ulikabiliwa na changamoto ya kukosekana kwa wataalamu wa unasihi shuleni na vyuoni na hivyo mpango huo haukuweza kutekelezwa kama ilivyokusudiwa.

Utaratibu wa kuteua mwalimu mwenye majukumu mengine ya kufundisha, mwalimu asiye na mbinu na uzoefu wa unasihi na kumfanya kuwa mnasihi wa wanafunzi, ni kutarajia kisichowezekana.

Kwa kutambua upungufu huo, mwaka 2007, wizara kwa kushirikiana na mradi wa Kuzuia na Kuelimisha Wanafunzi kuhusu Virusi vya Ukimwi (PASHA), iliandaa mwongozo wa kuendeshea mafunzo ya unasihi kwa walimu shuleni.

Mwongozo huo, pamoja na malengo mengine, ulilenga kupanua uelewa wa walimu kuhusiana na mbinu za kufanya unasihi, afya ya uzazi, tabia hatarishi na elimu ya maisha kwa jumla.

Katika makala haya, tunaangazia maeneo muhimu ya maisha ya mwanafunzi yanayoweza kushughulikiwa kupitia huduma wa unasihi shuleni.

Kujitambua

Mwanafunzi anayejitambua anajua uwezo wake, anajua ndani yake kuna kitu gani, wajibu wake katika jamii ni upi. Kwa bahati mbaya, mitalaa yetu ya elimu, kwa jumla haishughulikii masuala haya ipasavyo.

Kupitia unasihi na ushauri, mwanafunzi huyu anaweza kusaidiwa kujitambua kwa maana ya kutambua wito wake maishani na kuelewa ndani yake kumelala nini kinachoweza kuamshwa.

Kuelewa wajibu wake

Malengo mapana ya elimu rasmi ni kumwezesha mwanafunzi kuelewa nafasi yake katika jamii. Hali halisi, hata hivyo, haionyeshi ni namna gani mfumo wetu wa elimu unawawezesha wanafunzi kutambua wajibu wao katika jamii.

Kutofikiwa kwa lengo hilo, kumefanya watu wetu wajifikirie wenyewe badala ya kujiuliza kile wanachoweza kukifanya kama mchango wao kwa jamii.

Kipimo cha mafanikio kimekuwa ni namna mtu binafsi anavyoweza kuwatumia watu wengine kutimiza mahitaji yake.

Unasihi unajaza ombwe hili. Kwanza, unasihi unamwezesha mwanafunzi kujitambua na hivyo kuwa na mtazamo mpana wa maisha.

Kupitia kujitambua, mwanafunzi anajengewa uwezo wa kuelewa ana kipi cha kufanya kinachoweza kuinufaisha jamii yake.

Mwongozo wa maamuzi

Maisha ya mwanafunzi kama ilivyo kwa mtu mwingine yeyote, ni mfululizo wa maamuzi. Mwanafunzi anahitaji kuamua kwa mfano, nani anafaa kuwa rafiki yake, ushauri upi wa kuzingatia na upi wa kupuuza.

Malezi katika familia nyingi, yamejenga ufa kati ya watoto na wazazi. Hali hii inafanya iwe vigumu kwa watoto kujengewa uwezo wa kufanya maamuzi yanayojitegemea.

Huduma ya unasihi inaweza kujaza ombwe hili kwa kumsaidia mwanafunzi kufanya maamuzi yanayoongozwa na uelewa. Pia, unasihi unaweza kumsaidia mwanafunzi kutengeneza vipaumbele.

Hakuna mafanikio yasiyotegemea uwezo wa kupangilia kipaumbele. Kujua kipi ni muhimu na kipi si muhimu, kifanyike wakati upi na kipi kingoje, ni baadhi ya mambo yanayoweza kumsaidia mwanafunzi.

Uelekeo wa kitaaluma

Nakumbuka wakati nasoma, hatukuwa na mtu wa kutusaidia kuelewa tunaelekea wapi. Tulitegemea vigezo kama ufaulu kuamua tufanye nini baada ya kumaliza masomo.

Matokeo yake wengi tulisoma fani zisizolingana na malengo na vitu vilivyokuwa ndani yetu. Tulipokwenda vyuoni, wakati mwingine, ilikuwa kawaida kuona watu wakihangaika kubadili fani walizokuwa wamezichagua awali.

Pamoja na ukweli kwamba wakati mwingine kuna sababu nyingi zilizo juu ya uwezo na mipaka ya mwanafunzi mwenyewe, mara nyingi, maamuzi hayo yanafanyika bila kuongozwa na uelewa.

Unasihi kwa mukhtadha huu, una nafasi kubwa ya kumwongoza mwanafunzi kujua afanye nini kwa ngazi ya elimu inayofuata. Badala ya kuongozwa na ufaulu na matarajio ya jamii pekee, mwanafunzi aongozwe na vipaji, uwezo na wito wa kipekee alionao ndani yake.

Changamoto

Shule zetu hazina walimu wengi wenye utaalamu wa unasihi. Ingawa walimu husoma unasihi kama sehemu ya mafunzo yao ya ualimu, ufundishaji kama tulivyoona kwa kweli haukidhi mahitaji halisi katika mazingira ya shule zetu.

Kwa mfano, wakufunzi na wahadhiri wengi wanaopewa kazi ya kufundisha unasihi vyuoni, mara nyingi huwa ni watu waliosoma ualimu wa jumla. Pamoja na kubobea kwenye ualimu, wahadhiri hawa hukosa uelewa wa kina wa unasihi kama somo linalojitegemea.

Lakini kwa kuwa imejengeka dhana potofu kwamba kila mhadhiri aliyesoma ualimu anaweza kufundisha unasihi, matokeo yake somo hili huishia kufundishwa kinadharia.

Changamoto hizi kwa kiasi kikubwa, zinatokana na ukweli kuwa saikolojia na unasihi, ni fani mpya ambazo bado hazijatambuliwa vya kutosha katika jamii yetu.

Tunavyo vyuo vichache hapa nchini, kwa mfano, vyenye programu za shahada za awali, umahiri na uzamivu katika saikolojia na unasihi. Vyuo vingine vilivyobaki vinafundisha saikolojia na unasihi kama sehemu ya programu nyingine.

Ushauri

Kwa kuwa tunakubaliana kuwa unasihi una nafasi muhimu kwa mafanikio ya mwanafunzi, ni muhimu basi kutazama namna tunavyoweza kufanya unasihi kuwa huduma ya lazima katika mazingira ya shule zetu.

Katika kulifanikisha hilo, kama taifa, tunazo sababu za kutosha kuanzisha na kuimarisha programu zinazoandaa wataalamu waliobobea katika saikolojia, ili waweze kusaidia malezi ya watoto wetu.