Umuhimu wa kubadilisha maji ya bwawa la samaki

Bwawa la samaki lililojengwa kitaalamu. Ili kupata tija ya ufugaji wa samaki, wafugaji wanalazimika kubadili maji bwawani kwa vipindi maalumu.

Kumekuwapo  changamoto kadhaa katika ufugaji wa samaki, hususani suala  la ubadilishaji wa maji katika bwawa la samaki.

Ukweli ni kuwa baadhi ya wafugaji hawajui kabisa ni muda au wakati gani ni sahihi kubadilisha maji na  kwa namna gani.

Maji yanayofaa kwa ufugaji wa samaki ni maji yasiyokuwa na klorini na ammonia, ambayo ni sumu kwa ufugaji wa samaki. Maji ya bomba mara nyingi huwekwa klorini na ammonia ili kuua vijidudu vya magonjwa kwa binadamu au mifugo.

Kwa mantiki hiyo, maji hayo hayana usalama sana kwa ufugaji wa samaki hasa yakitumiwa moja kwa moja.

Swali ni nini cha kufanya ili maji hayo yaweze kutumika katika ufugaji wa samaki? Maji haya yanaweza kutumiwa kwa ufugaji wa samaki kwa kuondolewa klorini na ammonia. 

Klorini na ammonia huondolewa kwa kutumia njia mbili ambazo ni kutumia dawa za kuondoa klorini na ammonia zinazotengenezwa viwandani. Au  kwa kuweka maji kwenye chombo kikubwa cha wazi kwa muda huku ukiyakoroga au kuyajaza kwenye bwawa na kuyaacha siku kadhaa ukiwa unayakoroga.

Kama unayabadili kiasi tu, yaweke kwenye chombo kwa siku mbili hadi tatu kabla ya kuyaweka kwenye bwawa

Badilisha maji

Wafugaji  wengi, wanafuga samaki kwa muda mrefu bila kubadilisha maji kutokana na kutojua umuhimu wa kubadilisha maji kwenye bwawa la samaki.

Ni lazima kutambua kuwa maisha ya samaki ni kwenye maji na kwa kuwa samaki wanatumia virutubisho asili vilivyomo ndani ya maji mfano madini na hewa, hivyo ni muhimu kubadili maji yaliyomo ndani ya bwawa.

Aidha, maji pia yanachafuliwa na vitu kama fosifeti, hewa ya kaboni, ammonia, naitreiti na protini zinazokusanyika kidogo kidogo ndani ya maji na kuathiri ukuaji wa samaki. Maji hupotea taratibu kadri siku zinavyokwenda

kama mvuke.

Unaweza kubadilisha maji mara baada ya kupima kwa kutumia vipimo maalumu vinavyoweza kubaini kiasi cha oksijeni kilichopo, uchafu wa maji, PH, ammonia na vitu vingine. Hivi vyote vikiwa katika viwango visivyokubalika,  ni muhimu kwa mfugaji kubadilisha maji katika bwawa la samaki.

Fuata taratibu hizi kubadilisha maji

Unaweza kubadili maji asilimia 10 tu endapo unabadili kila wiki, yaani unapunguza na kuongeza maji asilimia 10 tu ya maji yanayotakiwa kuwamo kwenye bwawa.

Kama unataka kubadili maji kila baada ya wiki mbili,  punguza na kuongeza asilimia 20 ya maji yanayotakiwa kuwamo ndani ya bwawa. Kama unataka kubadilisha kila baada ya wiki tatu,  punguza na kuongeza asilimia 30 tu ya maji yanayotakiwa kuwamo ndani ya bwawa la samaki.

Ni vizuri kubadili maji kidogokidogo kwenye bwawa la samaki ili kutoathiri

afya ya samaki kwa kusababisha mshtuko. Aidha, haijalishi ni utaratibu gani utakaochagua kutumia kubadilisha maji ndani ya bwawa la samaki,  lakini ni lazima ubadilishe maji kwa kupunguza na kuongeza asilimia 60 hadi 70 ya maji yanayotakiwa kuwa ndani ya bwawa lako mara tatu kwa mwaka.

Kwa maeneo ya baridi, mabadiliko haya makubwa ya maji yafanyike kipindi cha joto ili kuepuka kuongeza maji ya baridi kwenye bwawa lako.

Aidha, haishauriwi kubadilisha maji mengi mara kwa mara kama kuna maji ya kutosha kwani unaweza kuathiri afya ya samaki kutokana na mshtuko.

Utoaji wa maji yote huku samaki wakiwa kwenye bwawa haushauriwi kwa namna yoyote ile; ubadilishaji huu ufanyike tu pale ambapo unataka kuwavuna samaki wote bwawani.

Makala haya awali yalichapishwa katika mtandao wa mkulima mbunifu.Wasiliana na mtaalamu kwa namba 0718 986 328.