Umuhimu wa mfanyakazi wa ndani unaulinganisha na nini?

Muktasari:

  • Je, umeshawahi kushindwa kuwajibika vyema katika mihangaiko yako ya kutafuta riziki unapokosa mtumishi wa kazi za nyumbani.

Ni kwa vipi maisha yako yanaathirika unapokosa msaidizi wa nyumbani? Maisha yanakwenda kama kawaida au hubadilika ili kuchukua nafasi yake.

Je, umeshawahi kushindwa kuwajibika vyema katika mihangaiko yako ya kutafuta riziki unapokosa mtumishi wa kazi za nyumbani.

Mwananchi limezungumza na baadhi ya watu ambao wametoa maoni yao kuhusu umuhimu wa wafanyakazi wa nyumbani na wanavyoathirika pale wanapokosa wasaidizi.

Mkazi wa Mikocheni B, Hassan Ntalale anasema mfanyakazi wa nyumbani ni mmoja kati ya watu muhimu katika maisha yake kwa kuwa ndiye mlinzi wa familia.

“Huyu ananilindia nyumba ambayo nimeijenga kwa gharama kubwa, ananitunzia watoto na kubwa zaidi ndiye anayetuandalia chakula. Mfanyakazi wa nyumbani ndiye anayebeba uhai wa familia.

“Fikiria siku akiamua kuwawekea sumu, kuchoma nyumba au kuwadhuru watoto! Sioni ninachoweza kukifananisha na msichana wangu wa kazi nyumbani. Ni mtu muhimu sana.”

Carherine Andrew mkazi wa Ilala Bungoni anasema mfanyakazi wa nyumbani kwake ni muhimu katika kuwezesha maisha ndani ya familia hasa wa wanafamilia walioajiriwa au kujiajiri wenyewe mbali na makazi yao.

Anasema kwa kutambua umuhimu wake wa mfanyakazi huyo kwenye familia amekuwa na vigezo vyake vya kumpata ikiwamo kuhakikisha kuwa ni mwaminifu, mwenye upendo na mvumilivu.

“Katika mambo hayo niliyotaja kwangu ni kigezo kikubwa cha mfanyakazi ninaye mhitaji, napenda awe mwaminifu kwa sababu yeye anashinda nyumbani hivyo anasaidia pia kuhakisha usalama wa mali zetu kwa ujumla ikiwamo chakula,” anasema.

Anasema ni rahisi kwa mfanyakazi asiyemwaminifu kufanya jambo baya kwa familia, pia anapenda mwenye uvumilivu kwa sababu watoto wanatofautiana wapo wengine ni watundu na wasumbufu hivyo akikosa uvumilivu huishia kuwaadhibu na kuwatesa hatua ambayo huwaathiri kimwili na kisaikolojia kwa ujumla.

“ Hata ninavyoishi naye nami najitahidi kuhakikisha anafurahia kazi yake, sipendi kutumikisha kama mtumwa maana kuna wengine nimesikia wanawabagua na kuwanyanyapaa ikiwamo kuwanyanyasa kwenye vyakula huku wengine wakiwapa hadi nguo za ndani kuwafulia,” anasema Andrew.

Mratibu wa taasisi ya Wotesawa iliyopo mkoani Mwanza na Cecilia Nyangasi anasema mfanyakazi wa nyumbani ni mtu ambaye anatakiwa kuthaminiwa.

Anasema kama ilivyo kwa watu wengine wafanyakazi wa nyumbani wana haki sawa kulingana na haki za binadamu, hivyo wanapaswa kufanya shughuli zako kwa misingi ya haki za wafanyakazi.

“Katika kuhakikisha mfanyakazi wa nyumbani anatimiziwa haki zake za msing,ni jukumu la muajiri wa mfanyakazi huyo kuishi naye katika mazingira yaliyo salama kwa kufuata sheria za nchi zinavyosema,”anasema Nyangasi.

Anataja baadhi ya haki hizo kuwa ni pamoja na kutobaguliwa, haki ya kushiriki shughuli mbalimbali za kijamii,haki ya kulipwa ujira kwa wakati ,haki ya kutoa maoni, haki ya kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili na nyinginezo nyingi.

“Wafanyakazi wa nyumbani wanakumbana sana na ukatili kwa sababu ni kundi ambalo lipo pembezoni na watu wengi wanamtazamo hasi juu ya kundi hili, hivyo kujikuta wanatenda ukatili dhidi yao wengine kwa kukusudia lakini pia wengine kwa kutokujua sheria inasema nini kuhusu wafanyakazi wa wa nyumbani,”anasema.

Nyangasi anasema hivyo basi ili kuondoa unyanyasaji kwa wafanyakazi wa nyumbani ni vyema kutoa elimu kwa waajiri ,viongozi wa serikali na jamii kwa ujumla juu ya mambo yote muhimu yanayomuhusu.

“Ni vyema kutambua haki, wajibu na sheria zinazomlinda mfanyakazi wa nyumbani, kwa kufanya hivi kila mmoja atajua wajibu wake na kuweza kutekeleza ili kumlinda mfanyakazi wa nyumbani,” anasisitiza.

Kuhusu mishahara

Waraka wa Mishahara wa mwaka 2013 unaelekeza mfanyakazi wa kazi za nyumbani unabainisha viwango vya mishahara wanavyopaswa kulipwa.

Kiwango cha chini cha mshahara ambacho ni Sh150,000 iwapo mwajiri ni balozi ama mfanyabiashara mkubwa, Sh80,000 ikiwa mwajiriwa haishi kwenye nyumba ya mwajiri wake.

Mfanyakazi wa nyumbani anayeishi kwa mwajiri wake anapaswa kulipwa kiwango cha kuanzia Sh 40,000.

VOX POP

Kulwa George

“Ninapotoka nyumbani sina wasiwasi, kwani najua watoto wangu wapo katika hali ya usalama, najua wataoga, watakula, wataenda shule na kurudi salama, yani bila msichana wa kazi sijui maisha yangu yangekuaje” anasema.

…………………………………………………………………………

Bariath Hassani mkazi wa Tabata relini.

“Vuta picha muda huu nipo huku watoto wakiwa peke yao nyumbani! Kwa kweli kazi zisingefanyika. Mimi nashangaa wale wanaowanyanyasa wasichana wa kazi bila kujua kuwa wao wanakazi kubwa na ngumu kutunza watoto tuwapo mbali hivyo tunatakiwa kuwaheshimu,”.

……………………………………

Palanjo Boas

“Mimi nipo huku na mke wangu ana bishara zake mbali kidogo na nyumbani, kwa hiyo watoto wetu wanahudumiwa na msichana wa kazi muda wote kuanzia asubuhi hadi tunaporejea nyumbani. Kwa familia yangu ya watoto wanne bila msichana wakazi tusingeweza kwenda kazini au kama mimi ningeendelea na kazi basi mke wangu asingeweza kuacha watoto peke yao.

…………

Mfanyabiashara Godwin George mkazi wa Mabibo

“Jamii iwaone wasichana hawa kama watoto wao, wasiwanyanyase, wawahurumie kwa kuwasaidia kazi siku ambazo wanapumzika kwenda kazi. Ila nawashauri wasichana wa kazi nao wawe na heshima kwa watu wanaoishi nao kwani wapo baadhi yao wakifika mjini wanabadilika kitabia.”